Nyalandu: Tutaanika wafadhili ujangili 
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema kuanzia sasa serikali itawataja hadharani wanaofadhili ujangili bila kujali nyadhifa zao.

Kauli hiyo aliitoa mwishoni mwa wiki mkoani hapa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhutubia mahafali ya 10 ya Chuo cha Musoma Utalii.

Waziri Nyalandu, alisema vita ya kupambana na ujangili nchini inahitaji ujasiri na kufuata sheria, hivyo yeye atawataja vigogo wote watakaokamatwa kwa kufadhili au kujihusisha na ujangili.

Aliongeza kuwa miongoni mwa mikakati mipya aliyonayo hivi sasa, ni kutangaza wamiliki wa magari yanayokamatwa yakiwa yamepakia nyara za serikali.

“Mimi niseme tu kwa sasa mipango niliyoweka kwa kushirikiana na watendaji wangu, polisi, jeshi la JWTZ na wadau wengine ni kuhakikisha wahusika wote wananaswa na kutajwa majina bila ya hofu wala kuoneana haya, hata kama ni kigogo wa serikali nitamtaja jina,” alisema.

Aliongeza kuwa amedhamiria kuhakikisha hali ya mazingira na maliasili za taifa zinatunzwa sanjari kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Waziri Nyalandu, alisema amepanga kukutana na uongozi wa halmashauri zote nchini kuweka utaratibu wa utunzaji wa mazingira.

Aliongeza kuwa watu wanaoshiriki biashara ya uchomaji mkaa, magogo na kukata miti kinyume na utaratibu uliowekwa watakumbana na mkono wa sheria kama inavyofanyika kwa majangili.

“Niseme tu hawa wanaofanya biashara ya mkaa, kuvuna magogo na kukata miti hovyo na hata wale wafugaji wanaoingiza mifugo yao kwenye hifadhi na wao pia nawaona kama majangili tu, adhabu yao ni sawa na majangili wa meno ya tembo,” aliongeza.

Alisema akiwa Tabora amekutana na kamati ya ulinzi na usalama mkoa na kuna mambo kadhaa kama serikali wamejadili ikiwemo kuacha kufanya mchezo wa siasa katika kulinda rasilimali za taifa.

Waziri Nyalandu alisema Operesheni Tokomeza Ujangili na Operesheni Kimbunga zitaanza muda si mrefu mara baada ya mipango kukamilika.

Kuhusu utalii wa ndani, waziri huyo alisema kama wizara wamejipanga kuweza kuongeza idadi ya watalii nchini kutoka watalii milioni moja hadi kufikia 2012/2013 na kufikia watalii milioni mbili kwa mwaka 2013/2014.

Aliongeza kuwa mipango hiyo ni pamoja na kuutangaza utalii wa nchini kwenye vyombo vya habari vya kimatifa vikiwemo CNN, BBC na Aljazeera.
Chanzo: Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top