Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
LIGI
kuu soka Tanzania bara inatarajia kuendelea kesho na keshokutwa, huku
mechi kubwa yenye uzito wa hali ya juu ni kati ya Yanga dhidi ya JKT
Ruvu na ile ya Ashanti United na Mbeya City.
Kesho
jumamosi zitapigwa mechi mbili ambapo wauza mitumba wa Ilala
watawakaribisha Mbeya City katika dimba la Azam Complex, Chamazi, nje
kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Mechi hii itakuwa na mvuto wake kutokana na mazingira ya timu zote mbili katika msimamo wa ligi hiyo.
Mbeya
City wapo nafasi ya tatu wakiwa wameshuka dimbani mara 23 na
kujikusanyia pointi 45, pointi moja nyuma ya mabingwa watetezi Yanga
waliopo nafasi ya pili kwa pointi 46 baada ya kucheza mechi 22.
Kocha
Juma Mwambusi ataingia kesho kwa lengo la kutafuta ushindi ili
kujiongezea pointi katika harakati zake za kuwania ubingwa wake wa
kwanza msimu huu.
Mbeya
City ni timu pekee iliyofanya vizuri na kuwashangaza wapenzi wa soka
kati ya klabu tatu zilizopanda ligi kuu msimu huu unaoelekea mwishoni.
Wenzao,
Ashanti United na Rhino Rangers wapo katika hatari ya kushuka daraja,
lakini maafande wa Tabora wanaonekana kwa asilimia kubwa wameshashuka
daraja.
Ashanti
wameshuka dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 21 katika nafasi ya
12, wakati Rhino Ranger ndio wanaoburuza mkia kwa kuwa na pointi 13
katika nafasi ya 14 baada ya kucheza mechi 23.
Katika
mchezo wa kesho, kocha mkuu wa Ashanti United, Abdallah Kibadeni
hahitaji matokeo mengine yoyote zaidi ya ushindi kwasababu akipoteza
mchezo atazidi kujiweka mazingira magumu zaidi ya kubakia ligi kuu.
Lakini
atahitaji kuwa na mipango mizuri zaidi mbele ya Wagonga nyundo,
kwasababu umoja walio nao na uwezo wa kikosi chao, wanaweza kuibuka na
ushindi.
Kule
Kaitaba kutakuwa na mchezo mmoja kesho jumamosi ambapo wenyeji Kagera
Sugar watakuwa wanachuana na Simba sc ya jijini Dar es salaam.
Simba sc wanaingia katika mchezo wa kesho wakiwa hawana cha kupoteza, kwasababu hawahitaji ubingwa wala nafasi ya pili.
Hata hivyo ushindi ni muhimu kwao ili kulinda heshima yao inayozidi kupotea siku za karibuni.
Wataingia
uwanjani wakiwa wamepoteza mechi mbili zilizopita dhidi ya Coastal
Union na Azam fc, hivyo kupoteza mechi ya kesho ni kuwatonesha zaidi
kidonda mashabiki wao.
Simba mpaka sasa wapo nafasi ya 4 katika msimamo baada ya kucheza mechi 23 na kujikusanyia pointi 36.
Kagera Sugar wao wanahitaji nafasi ya tatu au nne msimu huu, hivyo kesho wataingia kutafuta pointin tatu muhimu.
Kagera kwasasa wapo nafasi ya 5 wakiwa na pointi 33 baada ya kucheza mechi 22.
Ligi
hiyo itandelea tena jumapili (aprili 6) ambapo mechi kali ni baina ya
mabingwa watetezi, Yanga dhidi ya JKT Ruvu uwanja wa Taifa.
Umuhimu wa ushindi kwa timu zote mbili ndio sababu ya mchezo huo kuwa na mvuto kwa mashabiki wa soka.
Yanga wanahitaji matokeo kwa njia zote ili kupunguza pengo la pointi na vinara Azam fc wenye pointi 53 kileleni.
Wanajangwani
hao wameshuka dimbani mara 22 na kujikusanyia pointi 46 katika nafasi
ya pili, na nyuma yao wapo Mbeya City wenye pointi 45.
Yanga
wanahitaji kutetea ubingwa wao walioweka rehani mbele ya Azam fc, hivyo
kushinda kesho ni muhimu zaidi kwasababu mechi iliyopita walifungwa
mabao 2-1 na Mgambo JKT Kule Tanga.
Nao
JKT Ruvu chini ya kocha mkuu Fredy Ferlix Minziro wanahitaji pointi
tatu muhimu ili kuendelea kujiimarisha katika mazingira mazuri ya
kubakia ligi kuu.
Kwasasa wapo nafasi ya 9 kwa pointi 28 baada ya kucheza mechi 23, hivyo ushindi katika mechi hiyo utakuwa na maana kubwa kwao.
Matokeo yamekuwa magumu kuyatabiri kwa sasa, timu yoyote inaweza kushinda bila kujali ubora na majina ya wachezaji kutofautiana.
Mechi nyingine za jumapili ni kati ya Coastal Union dhidi ya Mgambo uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Vibonde
JKT Oljoro watakuwa na kibarua muhimu na maafande wa jeshi la Magereza
kutoka jijini Mbeya, Tanzania Prisons `Wajelajela` katika dimba la Shk.
Amri Kaluta Abeid jijini Arusha.
Rhino
Ranger waliopoteza matumaini ya kubakia ligi kuu watawakaribisha,
Mtibwa Sugar kutoka Marogoro kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini
Tabora.
Mechi
ya Ruvu Shooting na Azam iliyotakiwa kupigwa jumapili imesogezwa mbele
mpaka aprili 9 mwaka huu kwasababu wachezaji wengi wa Azam fc wameondoka
na kikosi cha timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro
Heroes.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment