Jaji Joseph Sinde Warioba
HATIMAYE Rais Jakaya Kikwete ameivunja rasmi Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyokuwa chini ya Mwenyekiti Jaji Joseph Warioba.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam
na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, imeeleza kuwa Machi 18,
mwaka huu, Warioba aliwasilisha rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu na
Machi 19 Rais Kikwete aliivunja tume hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kutokana na hatua hiyo na kwa mujibu wa
kifungu cha 31 cha sheria ya mabadiliko ya Katiba, rais alivunja rasmi
tume hiyo Machi 19 kwa tangazo la Serikali namba 81 la Machi 21, mwaka
huu.
Rais Kikwete aliunda tume hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 5 na 6 cha
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 kwa tangazo la Serikali namba
110 la mwaka 2012.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa tume ilikusanya maoni na kuandaa rasimu
ambayo imewasilishwa kwenye Bunge Maalumu na kwamba kwa mujibu wa
kifungu cha 31 cha sheria ya mabadiliko ya Katiba, Sura ya 3, rais
amepewa mamlaka ya kuvunja Tume hiyo baada ya Rasimu ya Katiba
kuwasilishwa bungeni.
Warioba aliwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu, M achi 18
ambapo katika hotuba yake alisema kuwa mfumo wa Serikali tatu
unaopendekezwa na tume hauepukiki.
Alibainisha kuwa Serikali ya Muungano itakuwa na mambo saba ambayo ni
Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri
ya Muungano, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje,
Usajili wa Vyama vya Siasa, Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi
yatokanayo na Mambo ya Muungano.
Wakati akiwasilisha rasimu ya pili, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alisisitiza kuwa mapendekezo ya serikali
tatu katika Muungano ni ya wananchi na taasisi mbalimbali, na wala si
matakwa ya tume yake.
Jaji Warioba alieleza kuwa nusu ya wananchi waliotoa maoni yao kuhusu Muungano walitaka uwepo wa serikali tatu.
Kati ya wananchi 38,000 waliotoa maoni yao kuhusu muungano visiwani
Zanzibar, 19,000 walizungumzia suala la muundo, huku zaidi ya nusu
wakitaka marekebisho ya kikatiba yatakayowezesha uwepo wa serikali tatu.
Warioba alisema kwa upande wa Bara asilimia 61 ya waliotoa maoni juu ya Muungano walipendekeza muundo wa serikali tatu.
Hata hivyo wiki iliyopita Rais Kikwete wakati akizindua Bunge alisema
muundo wa serikali tatu hautekelezeki na akasisitiza msimamo wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) ni serikali mbili.
Chanzo: Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment