Kuna makundi manne makuu ya vidonda vya tumbo ambayo leo tutawafahamisha.

Lakini kabla ya kuelezea makundi hayo ifahamike kuwa tafiti zimeonesha kwamba karibu asilimia 70 mpaka 90 ya vidonda vya tumbo husababishwa na aina ya vimelea vya bakteria wajulikanao kama Helicobacter pylori.

  Makundi hayo ya vidonda vya tumbo ni haya yafuatayo:- Mosi, kuna vidonda vinavyotokea kwenye mfuko wa kuhifadhia chakula yaani tumbo (Gastric ulcers).

Pili, vidonda vinavyotokea kwenye sehemu ya kwanza ya utumbo mdogo (Duodenal Ulcers).

Tatu, vidonda vinavyotokea kwenye koo (Oesophageal ulcers).

 Nne, vidonda vijulikanavyo kama Merckel’s Diverticulum Ulcers.

Zipo sababu zinazofanya mtu awe na vidonda vya tumbo. Moja ya sababu kubwa ni mtu kuwa na maambukizi ya bakteria aina ya Helicobacter pylori.

Imeonekana kuwa zaidi ya asilimia 50 ya watu duniani wana vimelea hivi katika utumbo.

Mbaya zaidi ni kwamba karibu asilimia 80 huwa hawaoneshi dalili yoyote ya kuugua ugonjwa wa vidonda vya tumbo mwanzoni.

Aina hii ya vimelea vya bakteria husababisha karibu asilimia 60 ya vidonda vinavyotokea kwenye tumbo (gastric ulcers) na zaidi ya asilimia 90 ya duodenal ulcers.

Hali hii husababishwa zaidi na kushindwa kwa mfumo wa kinga mwilini kuwaua na kuwaondoa kabisa vimelea hawa ndani ya mwili.

Matokeo ya kushindwa huku husababisha kuwepo kwa uambukizi wa kudumu katika kuta za tumbo (chronic active gastritis), uambukizi ambao huharibu mfumo na uwezo wa kuta za tumbo kutunza homoni ya Gastrin, ambayo ni muhimu katika kuhakikisha mazingira ya tumbo yanakuwa na kiwango salama cha tindikali.

Kwa kawaida, kazi ya gastrin ni kuchochea utolewaji wa tindikali (gastric acid) kutoka kwenye seli za ukuta wa tumbo zijulikanazo kama Parietal cells. Iwapo bakteria hawa watashambulia na kuharibu ukuta wa tumbo, mfumo wa gastrin pia uharibika, na hivyo kusababisha gastrin kuzalishwa kwa wingi hali ambayo pia huchochea uzalishaji wa gastric acid kwa wingi.

Tindikali hii inapotokea tumboni husababisha kuzalishwa kwa wingi hivyo kusababisha kuchubuka kwa ukuta wa tumbo na vidonda vya tumbo kutokea.

Matumizi ya baadhi ya dawa za kutuliza maumivu za jamii ya Non Steroid Anti-inflamatory Drugs  kama aspirin au diclofenac huweza kusababisha au kuongeza uwezekano wa kupata ugonjwa huu.

Kuna dhana iliyozoeleka kuwa vidonda vya tumbo huathiri zaidi mfuko wa kuhifadhia chakula yaani tumbo (stomach). Dhana hii si kweli kwani sehemu inayoathiriwa zaidi na tatizo hili ni sehemu ya kwanza ya utumbo mdogo ijulikanayo kitaalamu duodenum.
Chanzo: GPL
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top