Hatima ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuendelea kushiriki vikao vya Bunge au kutoendelea inatarajiwa kujulikana leo. 
 
Wakati wajumbe hao, wengi wao kutoka vyama vya upinzani wakitarajiwa kuamua ama kususa au kubaki ndani ya vikao, kuna uwezekano wa kuteuliwa baadhi yao katika Kamati ya Uongozi kutokana na majadiliano yaliyofanyika jana baina ya pande hizo mbili.
Majadiliano ya kamati hiyo, yalifanyika kutokana na kujiuzulu kwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba baada ya kuteuliwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao cha uongozi wa Ukawa jana zilieleza kuwa baada ya mjadala, viongozi walikubaliana kutosusia Bunge hilo.
“Ingawa wajumbe wengi walitaka tuondoke sote leo (jana) baada ya kuchoshwa na ukandamizaji unaofanywa na CCM, lakini tumeamua kwanza kesho (leo) kuendelea na Kikao, alisema mmoja wa wajumbe hao.
Mjumbe huyo alisema kwa mazingira ambayo CCM wameyajenga katika Bunge hilo, si rahisi tena wajumbe wa Ukawa kuendelea na Bunge , kwani ni wazi maamuzi mengi yatakayopita ni ya CCM.
“Kama wenyeviti wa kamati zote za Bunge ni zao, kamati za kanuni, uandishi wa rasimu ni zao huwezi kupitisha hoja ndio sababu wengi wetu wanataka tuondoke,” alisema mjumbe huyo.
Hata hivyo, katika kikao cha Uwaka, Mjumbe Tundu Lissu alionekana kuwataka wajumbe kutochukua maamuzi ya haraka kutokana na hali ambayo inajionesha bungeni kwani kunaweza kufanyika mabadiliko ya kanuni.
Kaimu Katibu Mkuu wa Ukawa, Julius Mtatiro baada ya kuulizwa jana kutokana na maamuzi hayo ya Ukawa alikataa kukanusha wala kukubali kwa maelezo kuwa yatatangazwa rasmi katika kikao cha jioni.
“Tumemaliza kikao cha uongozi cha Uwaka, sasa maamuzi tutayafikisha tena kwa wajumbe ili nao waamue,” alisema Mtatiro.
Mjumbe mwingine wa kamati ya uongozi wa Uwaka, Emmanuel Makaidi alisema, baada ya kikao chao kama viongozi, walitarajia jana jioni kuwaeleza maamuzi wajumbe wengine.
Wakati huohuo, Baadhi ya wajumbe kutoka Ukawa, huenda leo wakateuliwa katika kamati ya uongozi ya Bunge hilo, baada ya kukamilika mabadiliko ya kanuni.

“Tumejadili suala la uteuzi kama tunaweza kuongeza wajumbe kutoka huko Ukawa, nadhani kesho tunaweza kufikia maamuzi kwani hakuna ambaye anapenda Bunge hili kuwa na mivutano,” alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Uongozi.
Suala la Kamati ya Uongozi ya Bunge la Katiba kusheheni sura za vigogo wa CCM jana liligeuka ‘habari kubwa’ ya Bunge hilo baada ya wajumbe kuhoji uhalali wake bila kuwa na uwiano mzuri wa pande mbili za Muungano, vyama vya siasa wala makundi maalumu.
Vile vile uteuzi wa wajumbe watano kuingia katika kamati hiyo uliofanywa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta nao ulihojiwa kwamba haukuzingatia uwiano huo wa kitaifa.
Mwanyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alikoleza mjadala huo baada ya kukataa uteuzi wake kuwa miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo, akisema, “Sitaweza kuingia katika kamati ya uongozi na sipo tayari kutumiwa kama chambo.”
Kujitoa kwa Lipumba kulipokea kwa ndelemo kutoka kwa baadhi ya wajumbe, ambao walisema kuwa ni uamuzi wa hekima uliofanywa na mtu makini.
Kabla ya Lipumba kujitoa, baadhi ya wabunge akiwamo Kangi Lugola (CCM), Habib Mnyaa (CUF), John Mnyika (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) na Vicent Mzena (201) walioomba mwongozo na kuonyesha kutoridhishwa na uteuzi au muundo mzima wa kamati hiyo.
Profesa Lipumba, aliweka wazi kuwa hataki kutumiwa na hayuko tayari jina lake litumiwe kwa maslahi ya CCM.
Awali, Mwenyekiti Sitta alitangaza majina ya wajumbe watano wanaoungana na wenyeviti waliochaguliwa juzi kuunda Kamati ya Uongozi wa Bunge.
Kamati hiyo ndiyo yenye majukumu ya kutengeneza ratiba na miongozo mingine ya uendeshaji wa Bunge hilo.
Walioteuliwa ni Profesa Lipumba (CUF), Mary Chatanda (CCM), Fakharia Shomari (CCM), Hamid Abuu Juma (CCM) na Amon Mpanju (201).
Aliomba kutoa maoni yake, Lipumba alisema, “Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukuheshimu sana, lakini naomba niseme kuwa sitaingia katika kamati hiyo kwani nikiingia nitakuwa chambo cha kusema kiongozi wa upinzani yupo humo,” alisema Lipumba.
Aliongeza: “Mimi siyo Mwenyekiti wa Ukawa (Umoja wa Katiba ya Watanzania) kama ulivyosema, kama nia ilikuwa ni hivyo basi angechaguliwa Mheshimiwa Mbowe (Freeman) ambaye ni Mwenyekiti wa Ukawa.”

Akijibu hoja hiyo, Sitta alisema ni hiyari ya mtu kukubali au kuukataa uteuzi ambao amepewa na kuwa kufanya hivyo hakuwezi kuchukuliwa kuwa ni kosa kwa aliyekataa.
Muungano kwanza
Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Bunge, Ezekiel Olouch amewasilisha hoja binafsi ya kutaka Bunge kuanza kujadili hoja ya muundo wa Muungano kabla ya mambo mengine ili kupata mwafaka wa pamoja.
La sivyo, Oluoch amependekeza ikishindikana kuafikiana ni busara Bunge kuahirishwa na kurudi kwa wananchi ili wapige kura ya maoni juu ya Muundo wa Muungano na ikitokea maoni yakawa tofauti na rasimu, Tume ya Warioba ibadilishe rasimu yake.
“Tukishindwa kuelewana katika hili, tumuombe Rais avunje Bunge, turudi nyumbani kusubiri kura ya maoni ya wananchi, kisha turudi hapa kuendelea na mchakato wa Katiba,” alisema Olouch.
Akizungumza na Mwananchi jana, Olouch alisema hakuna namna yoyote ya kuanza mjadala wa Rasimu ya Katiba, bila kupata muafaka juu ya muundo wa Muungano.
“Tayari nimepeleka hoja binafsi juu ya hili, hatuwezi kuanza kujadili rasimu bila kujadili kwanza vifungu 64 kati ya 271 vya rasimu vinavyozungumzia muundo wa serikali tatu. Bila muafaka kwa suala hili, sidhani kama tunaweza kufika mbali katika kupitia vifungu vya rasimu,” alisema.
Hoja ya Oluoch imeungwa mkono na mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Chris Peter Maina aliyesema rasimu yote ya Katiba imebebwa na muundo wa serikali tatu, hivyo watakaopendekeza muundo wa serikali mbili wanatakiwa kutambua kuwa idadi kubwa ya mambo yaliyomo katika rasimu hiyo yatabadilika.
“Kazi ya Bunge la Katiba siyo kubadilisha kila kitu, kazi yao ni kuiboresha rasimu ya Katiba. Tatizo ni kwamba wanadhani wao wanaweza kubadili kila kitu,” alisema.
Aliongeza kuwa wajumbe wa Bunge hilo wanatakiwa kutambua kuwa wajumbe wakibadilisha tutapata Katiba mbaya na sidhani kama wanaotaka serikali mbili wanalijua jambo hili.
“Ukichomoa nati moja sehemu, ni wazi kuwa kitu husika hakitakaa kama kilivyokuwa awali ni lazima kitapwaya. Ni lazima wakubaliane na hilo na hoja zilizomo kwenye rasimu,” alisema Profesa Maina.
 Chanzo: Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top