Kinda Shomary Kapombe Jr ambaye anasemekana kukodolewa jicho na klabu ya Yanga ili kuinasa saini yake msimu ujao, viongozi wa Simba wanasema mpaka amebadili nambari ya Simu   Niyonzima 3 
Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima anasemekana kuwaniwa na Simba,na wamekiri dhahiri kuwa ni mchezaji muhimu lakini hawajazungumza naye ila kama anataka anakaribishwa MAZOEZI 
 Mazoezi-ya-Yanga 
Jalamba la Yanga Zanzibar

Na Baraka Mpenja
 
Wakati wapenzi wa soka ama kandanda nchini Tanzania wakisubiri kwa hamu pambano kali la watani wa jadi “Dar es salaam Derby” baina ya mabingwa wa msimu huu wa ligi kuu soka Tanzania bara, wanajangwani Dar Young Africans dhidi ya “Taifa kubwa” wekundu wa msimbazi Simba mei 18 mwaka huu uwanja wa taifa, timu hizo zinazidi kupigana mkwara mzito huku joto kwa mashabiki likizidi kupanda.
 
Hapo jana mwenyekiti wa kamati ya usajili, mjumbe wa kamati ya utendaji na mratibu wa timu katika mashindano, Keptein Zacharia Hans Hoppe alishtushwa na uamuzi wa TFF kubadili mwamuzi wa mchezo huo ghafla na kuwa Martin Saanya kutoka Morogoro badala ya Israel Nkongo aliyepangwa awali.
 
“Hizi ni njama za Yanga, tunawataka TFF watoe sababu za msingi kwanini wamebadili mwamuzi bila kuongea na sisi, kamati ya utendaji tutakaa kuangalia hilo”. Alisema Hoppe.
 
Hoppe alisema watani zao wana mchecheto mkubwa sana kufuatia kikosi cha Simba kuimarika zaidi huku makinda wakionesha kabumbu safi.
 
“Lazima tuwafunge Yanga na kuwatibulia sherehe za ubingwa wao, timu iko vizuri na inaandaliwa kwa umakini mkubwa na siku ya jumamosi watakiona cha moto uwanja wa taifa”. Alisema Hoppe.
 
Wakati Hoppe akitamba kuwafunga Yanga, Katibu mkuu wa Yanga ambao ndio mabingwa, Lawrence Mwalusako amesema kikosi kipo vizuri na wanajiandaa vizuri kuibuka na ushindi katika mechi hiyo.
 
“Nafikiri wakati wa siasa na maneno umekwisha, acha tuweke akili yetu kwa ajili ya mechi ya jumamosi, muda ukifika itafahamika nani mkali zaidi”. Alisema Mwalusako.
 
Mbali na tambo za maandalizi ya mechi hiyo, viongozi hao pia wameendelea kupigana vikumbo kuhusu usajili wa wachezaji wa msimu ujao.
 
Hoppe alisema viongozi wa Yanga wanamsumbua sana mchezaji wao Shomary Kapombe mpaka amebadili nambari ya simu ili kuepukana na usumbufu huo wakati huu muhimu wa kuisadia timu yake.
 
Hoppe alisisitiza kuwa kila kukicha Yanga wanamhitaji Kapombe ila watambue kuwa bado ana mkataba na Simba hivyo ni mchezaji halali na watamuongezea tena.
 
“Sisi Kapombe ni mchezaji wetu, lakini ikifika wakati wa kuondoka ataondoka kwani sisi ndio njia ya kwenda nje kucheza soka la kulipwa, simba soka lipo bwana”. Alijigamba Hoppe.
 
Pia alisema Ngasa wamemuongeza mkataba na ataendelea kuchezea Msimbazi msimu ujao wa ligi.
 
Pia hakusita kufafanua suala la Haruna Niyonzima “Fabrigas”, ambapo alikanusha taarifa kuwa wamefanya mazungumzo naye kuhusu kumsajili ingawa anakiri kuwa mchezaji huyo ni mzuri na kama atakuwa tayari kucheza Simba anamkaribisha sana.
Wakati Hoppe akisema hayo, katibu wa Yanga Mwalusako yeye amesema suala la kumsumbua Kapombe hawezi kulizungumzia kwa sasa.
 
“Mambo ya Kapombe kwa sasa hayana nafasi, acha tuangalie mechi ya jumamosi baada ya hapo tutaongea mambo ya usajili”. Alisema Mwalusako.
Kuhusu Niyonzima, Mwalusako amewaondoa hofu wana Yanga kuwa ni mchezaji halali wa Yanga na atabaki yanga, hivyo msimu ujao ataichezea klabu hiyo kwa sababu anaipenda sana.
Hilo ndio joto la pambano la watani wa jadi, tusubiri jumamosi tuone itakuwaje.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top