Mkutano wa Rais Kikwete na viongozi hao kutoka
vyama vyenye wabunge na kimoja kinachowakilisha vyama visivyokuwa na
wawakilishi bungeni, unajadili kwa undani mustakabali wa uchaguzi mkuu
ujao, hali inayoashiria kwamba suala la Katiba Mpya siyo tena kipaumbele
cha sasa katika siasa za nchi.
Kamati ndogo iliyoundwa na TCD chini ya Mwenyekiti
wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia itawasilisha mapendekezo ya majawabu ya
hoja zilizopendekezwa katika mkutano wa awali uliofanyika Agosti 31,
mwaka huu katika Ikulu ya Kilimani, Dodoma na baadaye kuhitimishwa na
kikao cha faragha cha viongozi wa vyama hivyo katika Hoteli ya St
Gaspar.
Mbali na Mbatia wajumbe wengine ni wale wanaotoka
kwenye vyama ambavyo viko kwenye mvutano kuhusu Bunge Maalumu wakiwamo
wale wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa upande mmoja na CCM kwa
upande mwingine.
Hao ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba,
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa wakati CCM kinawakilishwa na
Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana ambao kwa pamoja watawasilisha
mapendekezo ya kumaliza mvutano uliopo pamoja na mwafaka kuhusu namna
bora ya kuendesha uchaguzi mkuu ujao.
Taarifa ambazo gazeti hili lilizipata zinasema
miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakisukumwa kwa nguvu na Ukawa hata
walipokutana na Rais mara ya kwanza ni kusitishwa kwa Bunge Maalumu kwa
maelezo kwamba Katiba Mpya siyo tena kipaumbele cha nchi na kwamba fedha
zinazotumika zingeelekezwa katika mambo mengine muhimu ya nchi.
Ukawa unaoundwa na vyama vya NCCR- Mageuzi, CUF na
Chadema, wajumbe wake katika Bunge Maalumu walisusia vikao vya Bunge
hilo tangu Aprili 16, mwaka huu kwa maelezo ya kwamba hawaridhishwi na
mambo yanavyoendeshwa na baadaye kuanza kushinikiza kusitishwa kwake.
Hata hivyo, suala la kusitishwa kwa Bunge Maalumu
limekuwa gumu kutokana na kutokuwapo kwa mwanya wowote wa kisheria
unaomruhusu Rais Kikwete kuchukua hatua hiyo, lakini habari zinasema
‘mlango pekee uliobaki’ ni Oktoba 4, 2014 ambayo ni siku ya mwisho
iliyotajwa kwenye tangazo la Serikali.
“Nadhani hata mheshimiwa Rais ameshaombwa asitoe
GN (tangazo lingine) ya kuongeza siku za Bunge Maalumu kama wajumbe wa
Bunge wanavyotaka, kwa hiyo kama atakubali ni dhahiri kwamba Bunge
litakoma tarehe 14 mwezi ujao (Oktoba),” kilisema chanzo chetu kutoka
serikalini.
Ikiwa Rais ataamua kutobadili tangazo lake, basi
Bunge Maalumu litasitisha shughuli zake, kwani tayari lilishapanga
ratiba inayoonyesha kuwa litaendelea hadi mwishoni mwa Oktoba wakati
Mwenyekiti wake, Samuel Sitta atakapokabidhi Katiba inayopendekezwa kwa
Rais Kikwete.
Tarehe ya mwisho
Licha ya tarehe ya mwisho ya Bunge hilo ambayo ni
Oktoba 4, 2014 kutangazwa na Rais Kikwete Julai 28 mwaka huu na kuchapwa
kwenye Gazeti la Serikali (GN) namba 254 la Agosti 1, 2014, Bunge
Maalumu lilibadili kanuni zake, hatua ambayo ilitaja siku sitini
zilizotolewa na Rais kwamba ni za kazi tu.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Awali katika azimio lake la Aprili 4, mwaka huu, Bunge Maalumu
liliipitisha Jumamosi kuwa moja ya siku zake za kazi kwa kuongeza
kipengele cha nne katika Kanuni ya 14. Sehemu ya Kanuni hiyo inasomeka:
“Bunge Maalumu kwa siku za Jumamosi litakutana kuanzia saa tatu asubuhi
hadi saa saba mchana…..”.
Hata hivyo, Agosti 5, 2014 Bunge hilo lilipitisha
azimio lingine ambalo lilirekebisha kanuni hiyo ya 14 (4) na kuifuta
Jumamosi katika siku zilizotajwa kuwa za kazi. Sitta aliwaambia wajumbe
wa Bunge hilo kwamba Rais Kikwete alikuwa tayari ameridhia kwamba siku
60 alizotoa hazitajumuisha Jumamosi, Jumapili na siku za sikukuu.
Baada ya mabadiliko hayo, Katibu wa Bunge Maalumu,
Yahya Khamis Hamad aliandika barua serikalini akitaka ufafanuzi wa
kisheria kuhusu suala hilo, lakini hadi sasa barua hiyo haijajibiwa.
Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue wiki hii
aliliambia gazeti hili kwamba Rais Kikwete alikuwa amepokea maombi ya
Bunge Maalumu ili arekebishe tangazo lake la awali na kwamba bado
yanafanyiwa kazi huku akisisitiza kuwa uamuzi wa Rais lazima utazingatia
sheria.
Sefue alitoa kauli hiyo huku akisema Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alikuwa sahihi katika tafsiri
aliyowahi kuitoa akisema kwamba siku zinazotajwa kwenye gazeti la
Serikali kwa ajili ya Bunge Maalumu ni za kikalenda na siyo za kazi kama
ilivyotafsiriwa na uongozi wa Bunge hilo.
Mwanasheria katika Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu, Harold Sungusia akizungumzia suala hilo jana alisema kifungu
cha 28 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ndicho kinachoelekeza jinsi
nyongeza ya siku inavyopaswa kufanyika wakati kifungu cha 27 (3) cha
sheria hiyo pia kinalipa Bunge Maalumu uwezo wa kutunga kanuni za jinsi
ya kuendesha mambo yake.
“Sheria iko wazi na hapa tafsiri sahihi ya siku
zilizoongezwa inaweza kutolewa na mahakama kwani Mwanasheria Mkuu wa
Serikali hana nafasi katika Bunge hili na hapo ndipo tatizo lilipo
kwamba kuna watu wanadhani kwamba hili ni Bunge la kawaida, sivyo hata
kidogo,”alisema Sungusia.
Hoja ya kutaka Bunge Maalumu kusitishwa mapema
kama ilivyo kwenye tangazo la Serikali inatokana na ukweli kwamba ratiba
yake ya sasa inaingiliana na ratiba za vikao vya Bunge la Muungano
ambalo limepangwa kuanza Novemba 4, 2014 na Baraza la Wawakilishi ambalo
limepangwa kukutana kuanzia Oktoba 22 mwaka huu.
Kwa upande wa Bunge la Muungano, Katibu wake Dk
Thomas Kashililah alisema kuna kamati za kisekta zinapaswa kuanza vikao
vyake Oktoba 10 kwani kuna miswada mingi ya Serikali inayopaswa
kufanyiwa kazi mapema.
Rais na TCD
Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo aliliambia gazeti
hili mjini Dodoma siku chache zilizopita kwamba mazungumzo baina yao na
mkuu huyo wa nchi yanalenga mambo muhimu ya kuwezesha kuwa na mazingira
bora ya uchaguzi mkuu wa 2015 na siyo vinginevyo.
“Tuna mambo muhimu na hayo diyo tumekuwa
tukizungumza, mambo ya Tume Huru ya Uchaguzi, mambo ya mgombea binafsi,
kuhojiwa kwa matokeo ya urais, hayo ndiyo mambo tunayozungumza kuona
jinsi gani tutaweza kuwa na mwafaka wa pamoja maana hata kama Katiba
Mpya ikipitishwa leo haiwezi kutumika kwenye uchaguzi mkuu,” alisema
Cheyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa UDP.
Baada ya mkutano wa Agosti 31 mwaka huu katika Ikulu ya
Kilimani, Dodoma na baadaye katika Hoteli ya St Gaspar pia ya mjini
humo, viongozi wote walitoa tamko la pamoja ambalo pamoja na mambo
mengine lilitaja kuundwa kwa kamati ndogo ili kuzifanyia kazi hoja
kadhaa zilizowasilishwa kwenye kikao hicho.
Habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam
zinasema kamati hiyo ilifanya vikao vyake jijini Dar es Salaam na leo
wajumbe wake watasafiri hadi Dodoma kwa ajili ya mkutano wa awamu ya
pili na Rais Kikwete.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment