UAMUZI uliofikiwa na viongozi wa vyama vya siasa na Rais Jakaya
Kikwete umemweka katika wakati mgumu Mwenyeki wa Bunge Maalumu la
Katiba, Samuel Sitta kuahirisha au la vikao vya Bunge hilo.
Hii inafuatia Rais Kikwete na viongozi wa Kituo cha Demokrasia
Tanzania (TCD), kukubaliana kusitisha Bunge la Katiba Oktoba 4 tofauti
na ratiba ya Sitta ambayo inaonyesha vikao vitaendelea hadi Oktoba 31
atakapomkabidhi rais katiba iliyopendekezwa.
Vilevile kwa tafsiri ya uamuzi huo, Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) watakuwa wameibuka kidedea kwani tangu mwanzo walikuwa wanataka
Bunge hilo liahirishwe hadi maridhiano yapatikane.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mwenyekiti wa
TCD, John Cheyo, alisema katika makubaliano ya kikao chao na rais
kilichofanyika juzi Ikulu ndogo mjini hapa, walikubaliana kwa pamoja
kuwa Bunge la Katiba liendelee hadi Oktoba 4.
Kwa mujibu wa ratiba iliyokuwa imetolewa mara baada ya awamu ya pili
ya Bunge la Katiba kuanza Oktoba 10 hadi 21, ndiyo wajumbe wa Bunge hilo
walitarajiwa kuanza kupiga kura ili kupitisha sura mbalimbali za rasimu
hiyo na kupata Katiba inayopendekezwa.
Alisema kuwa baada ya Bunge hilo kusitishwa, mabadiliko madogo katika
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 yatafanyika.
Alisema kuwa katika marekebisho hayo, sheria ya uchaguzi itafanyiwa
marekebisho ili kuwezesha nchi kufanya uchaguzi ulio huru na wa haki.
“Pamoja na kazi ya msingi inayofanywa na Bunge Maalumu la Katiba,
inaonekana kuwa mchakato huo unaoendelea sasa hauwezi kutupa Katiba
itakayotumika katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, muda hautatosha kukamilisha
mchakato na kufanya mabadiliko yatakayohitajika,” alisema Cheyo.
Alisema kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya Katiba, mwisho wa
mchakato huo ni kura ya maoni iliyotarajiwa kufanyika Aprili 2015.
“Kama itabidi kura irudiwe kwa mujibu wa sheria italazimika kura ya
maoni ifanyike Juni au Julai 2015, muda ambao Bunge la Jamhuri ya
Muungano linatakiwa livunjwe kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 2015,”
alisema mwenyekiti huyo.
Alisema hatua ya kura ya maoni haitafanyika tena kwa sababu itaingiliana na uchaguzi mkuu ujao.
Hata hivyo, alisema ili Katiba mpya ipatikane na kutumika katika
uchaguzi mkuu ujao, ni lazima uhai wa Bunge na Serikali uongezwe zaidi
ya mwaka 2015, jambo ambalo alidai kuwa haliungwi mkono na TCD.
Cheyo alieleza kuwa mchakato wa kupata Katiba mpya ambao utasitishwa Oktoba 4, utaendelea baada ya uchaguzi mkuu mwakani.
Alisema kwa vile uchaguzi mkuu utafanyika kwa kutumia Katiba ya sasa,
wamekubaliana kwa pamoja mambo ya msingi yafanyiwe mabadiliko ndani ya
Katiba hiyo.
Mambo yatakayorekebishwa kwenye Katiba ya 1977
Mambo yatakayorekebishwa kwenye Katiba ya 1977 ni pamoja na Tume Huru
ya Uchaguzi na mshindi wa uchaguzi wa nafasi ya rais ashinde kwa zaidi
ya asilimia 50.
Mambo mengine ya kuingizwa kwenye Katiba ni pamoja na matokeo ya
urais kupingwa mahakamani na kuruhusu mgombea binafsi katika uchaguzi.
Alisema kuwa vyama vya siasa ambavyo vinapenda kupendekeza mambo
mengine ya kufanyiwa marekebisho katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano
1977, vimeombwa kufanya hivyo mapema kwa kuwa muda uliobaki ni mdogo.
“TCD kupitia vikao vyake itakaa kujadili mapendekezo hayo na kuyapeleka serikalini kwa hatua nyingine,” alisema Cheyo.
Mkakati wa Sitta
Mara tu baada ya awamu ya pili ya Bunge Maalumu la Katiba kuanza,
marekebisho ya kanuni yalifanyika ambapo muda wa Bunge hilo uliongezwa.
Kutokana na marekebisho hayo, hatua ya kupiga kura ili kupitisha
ibara mbalimbali za Rasimu ya Katiba, ilitarajiwa kuanza Oktoba 10 hadi
21.
Baada ya siku moja ya kufanya marekebisho kanuni, kamati za Bunge
hilo zilikaa kwa siku 17 kupitia sura 15 za Rasimu hiyo zilizokuwa
zimebaki baada ya awamu ya kwanza ya Bunge hilo kupitia sura ya kwanza
na ya sita.
Ratiba hiyo ilionyesha kuwa kazi ya kamati kupitia sura hizo ilitakiwa kukamilika Agosti 27, mwaka huu.
Kati ya Agosti 28 hadi Septemba mosi, kamati hizo zilitakiwa kukamilisha kazi ya kuandaa taarifa ya sura zote walizozijadili.
Kwa mujibu wa ratiba, Septemba 2 hadi 8 kamati hizo ndipo zilifanya
kazi ya kuwasilisha taarifa zao ndani ya Bunge Maalumu ili zianze
kujadiliwa.
Baada ya kazi hiyo kukamilika juzi, jana wajumbe wa Bunge hilo
walianza mjadala wa kuchagia kwenye sura zilizowasilishwa, kazi
iliyotarajiwa kufanyika kwa siku 15 hadi kufikia Septemba 29.
Majadiliano yakimalizika Kamati ya Uandishi itaanza kazi ya kuandika
upya ibara za sura zote za Rasimu ya Katiba kazi itakayofanyika kwa muda
wa siku tano, Septemba 30 hadi Oktoba 6.
Oktoba 9, Kamati ya Uandishi ilitarajiwa kuwasilisha taarifa yake
katika Bunge Maalumu kuhusu rasimu hiyo ili iweze kupigiwa kura na kazi
hiyo ya kupiga kura ndipo itaanza Oktoba 10.
Kati ya Oktoba 22 hadi 28, wajumbe wa Bunge hilo walitarajiwa kupitisha masharti ya mpito.
Ratiba hiyo inaonyesha kuwa Oktoba 29 na 30 ni siku ambazo Katibu wa
Bunge atakamilisha Katiba inayopendekezwa kwa ajili ya kuwasilisha kwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar.
Ratiba hiyo inaeleza kwamba Oktoba 31 ni siku ya Mwenyekiti wa Bunge
Maalum, Sitta kuwasilisha Katiba inayopendekezwa kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano na Rais wa Zanzibar.
BBC
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment