KATIBU Mkuu wa Chama cha Alliance for Change and Transparance (ACT-Tanzania), Samson Mwigamba 
 KATIBU Mkuu wa Chama cha Alliance for Change and Transparance (ACT-Tanzania), Samson Mwigamba, ameweka hadharani dhamira ya chama hicho kuongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.

Ingawa Mwigamba hakutaja jina la Zitto moja kwa moja, jana aliwaeleza wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Community Centre mjini Kigoma kuwa wao wanamsafishia njia yule ajaye na kwamba mtu huyo atatoka katika mkoa wa Kigoma.

Akitumia mifano ya vitabu vya Mungu, Mwigamba alisema wanawajibika kusafisha njia ili atakayekuja kuongoza asiwe na vikwazo vingi ikiwa ni pamoja na kukosa uongozi kutoka ngazi ya chini.

Katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na waliyokuwa viongozi wa CHADEMA mkoa wa Kigoma, ambao walitangaza kujiunga rasmi na ACT-Tanzania, Mwigamba alisema watashirikiana na yeyote mwenye dhamira ya kweli ya kuwaondoa CCM madarakani.

Alisema katika vyama vilivyopo sasa kuna baadhi ya watu ni wazalendo na kwamba wananyimwa fursa katika vyama hivyo.

Awali katika ufunguzi wa matawi ya chama hicho, wafuasi wa CHADEMA na ACT-Tanzania walijikuta katika vita vya kugombea ofisi ya kata ya Gungu jimbo la Kigoma Kaskazini na kuwafanya polisi kuzuia kupandishwa kwa bendera ya ACT-Tanzania katika ofisi hizo.
Tanzania Daima

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top