MAZUNGUMZO
yanayoendelea kuhusu jinsi ya kunasua mchakato wa katiba mpya kati ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA), yanaelekea kukwama kwa sababu yameingiliwa na hila,
Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya taarifa, kikao cha mwisho kilivunjika
bila muafaka kutokana na CCM kuleta mapendekezo yasiyotekelezeka, kama
njia ya kuondoa wajumbe kwenye hoja kuu.
Miongoni mwa mapendekezo mapya yaliyoletwa mezani, ni pamoja na
kutaka wajumbe wajadili maeneo mengine ya sheria ambayo CCM haiyataki,
na kutaka wajumbe wengine waongezwe katika mjadala huo ili idadi iwe
kubwa zaidi.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, wajumbe wa UKAWA
walikataa mapendekezo hayo kwa misingi kwamba hoja ya kwanza
ingesababisha warudi kwenye hoja nyingine inayohoji jinsi Rais Jakaya
Kikwete alivyoteua baadhi ya wajumbe wa kundi la 201, ambao imekuwa
inadaiwa kwamba wengi wao ni mawakala wa CCM walioongezwa makusudi ili
kukuza idadi kwa ajili ya kuongeza kura katika hatua ya uamuzi.
“Katibu Mkuu wa CCM alipoleta hoja hiyo, wenzetu wakamwonyesha kwamba
kupanua maeneo yenye ugomvi ni kufungua Pandora box ambalo CCM
tusingelipenda, kwa mfano kuanza kuhoji upya idadi na utaratibu wa
kupata wajumbe wa kundi la 201. Hoja hiyo ikafa,” kilisema chanzo chetu
kilicho karibu na kiongozi huyo.
“Ndipo alipopendekeza kuwa ingekuwa vema waletwe wajumbe wengine
kwenye mazungumzo, ambao ni wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, hoja
ikapingwa pia na wajumbe wa UKAWA kwa maelezo hao ni sehemu ya
waliosababisha mazungumzo kuvunjika.”
Chanzo chetu kiliongeza: “UKAWA walisema kwamba hao ndio waliokimbiwa
bungeni, na kwamba kuwaleta kwenye mjadala kungesababisha mabishano
zaidi badala ya kutafuta usuluhishi.
“Mjumbe mmoja alizungumza kwa ukali, kwamba hiyo ni non-starter,
kwamba UKAWA wametoka kwa sababu ya wajumbe hao hao, hivyo kuwaleta
kwenye mazungumzo haya kungekuwa sawa na kuongeza watu walewale halafu
kutarajia matokeo tofauti.”
Kwa mantiki hiyo, mjumbe mmoja aliyeshiriki mjadala huo, huku
akikataa kuingia kwa undani, amekiri kwa kusema kwamba “mazungumzo
hayaendi kokote.”
Hata hivyo, baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na timu
yake kukataliwa mapendekezo yao mawili kwa sababu hizo, wajumbe wa UKAWA
walitoa pendekezo jipya, ambalo kwa ujumbe wa CCM lilionekana kuwa zito
na gumu zaidi.
“Walipomaliza kupangua mapendekezo yetu, ndipo nao wakapendekeza
kwamba badala ya watu walewale, sasa ni vema waitwe marais wawili –
Jakaya Kikwete wa Muungano na Dk. Ali Mohamed Shein wa Zanzibar, ambao
ndio viongozi wa mihimili ya dola,” alisema mtoa habari huyo na
kuongeza:
“Nani akubali? Hapo katibu mkuu (Kinana) na timu yake waliruka kama
wameona joka kubwa, kwa sababu tunajua rais akikutana na wapinzani
anaweza kuwasikiliza. Imeshatokea huko nyuma, na hatutaki itokee sasa,
maana rais akishakubali hoja zao, kama chama tutalazimika kufuata
ushauri atakaotoa, nao watakuwa wameshinda.”
Hoja ya UKAWA kutaka kujadiliana na marais wawili ililenga kumpa
fursa Rais Kikwete kurejesha nyuma msimamo wake kuhusu rasimu ya pili ya
katiba, maana siku alipozindua Bunge la Katiba, aliweka msimamo ambao
ndio umekuwa ukifuatwa na wajumbe wote wenye maslahi na CCM.
Mara kadhaa, baadhi ya watu mashuhuri na taasisi zimesema kwamba kama
Rais Kikwete asingeleta msimamo wa chama chake bungeni, ingejadiliwa
rasimu ya tume, na UKAWA wasingetoka.
Miongoni mwa watu maarufu waliokiri kwamba rais alikosea ni pamoja na
Msajili ya Vyama vya Siasa mstaafu, John Tendwa, ambaye alikiri kwamba
rais aliteleza.
Jumuiya ya Wakristo Tanzania (CCT) ilitoa waraka wake kusisitiza hoja
hiyo, kwamba kauli ya rais ndiyo ilivuruga mchakato, na kwamba ili
Bunge liendelee kwa amani inabidi wajumbe wote wajielekeze kwenye rasimu
ya pili ya katiba iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Mara kadhaa, viongozi wa UKAWA wametamka wazi kwamba iwapo mjadala wa
Bunge hilo hautajikita katika rasimu hiyo, hawatarejea bungeni.
Serikali imekuwa inafanya jitihada za chini chini, na za wazi
kuhakikisha wajumbe wa UKAWA wanarudi bungeni, lakini wao wanadai kwamba
hawawezi kurudi kujadili rasimu ya CCM badala ya rasimu ya wananchi
iliyowasilishwa na Jaji Warioba.
Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment