Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba
WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema uzee na ujana siyo
sifa za mtu anayestahili kuwa Rais wa Tanzania atakayepatikana baada ya
Uchaguzi Mkuu ujao. Warioba aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na
gazeti hili kufafanua habari iliyoandikwa na gazeti moja la kila siku
(si MTANZANIA), ikimkariri akisema rais ajaye anapaswa kuwa kijana.
Akifafanua, Warioba, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, alisema ameshangazwa na namna suala la uzee na ujana
lilivyogeuzwa na kufanywa kuwa sifa mama ya mtu anayepaswa kuwa rais
ajaye kinyume na kile alichokizungumza wakati akihojiwa na gazeti hilo.
Jaji Warioba alisema anaamini jambo lililosababisha kukuzwa kwa
ajenda hiyo ya uzee na ujana kwa sasa ni kukithiri kwa makundi ya urais.
“Umefika wakati sasa Watanzania wafikirie sifa za mtu anayefaa kuwa
kiongozi bora, badala ya kuendelea na ajenda ya uzee na ujana.
“Niliwaambia (waliokuwa wananiuliza maswali) kwa nini sisi
tuliokwishastaafu tuingizwe huko (kwenye kugombea urais), wananchi wapo
wanaona nani anafaa, siyo kwenda na kuwaambia. Wao wanaona, tukazanie
sifa za mtu anayefaa kuongoza,” alisema Warioba.
Alisema kauli yake wakati alipozungumzia suala hilo ilitokana na
swali aliloulizwa kuwa yeye pamoja na Dk. Salim Ahmed Salim wamekuwa
wakitajwa na baadhi ya watu na kuwaomba wawanie nafasi hiyo.
“Nashangaa kwanini hili suala liwe issue, najua yote ni kwa sababu ya
makundi, kauli yangu ilitokana na swali nililoulizwa kuwa kumekuwa na
watu wakitufuata na kuniomba mimi na Dk. Salim tugombee. Nikasema nini
kimelikumba taifa hili mpaka sisi tuliokwisha ng’atuka tugombee tena,
kwa hiyo hoja ilikuwa ni sisi personal (binafsi),” alisema.
Akizungumzia urais, alisema ni vyema sasa Watanzania wakafikiria sifa
za mtu anayefaa kuwa kiongozi bora, badala ya kuendelea na ajenda ya
uzee na ujana. Katika siku za karibuni kumekuwapo na makundi ndani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo yamekuwa na msuguano mkali hadi
kufikia hatua ya makada wake kupewa onyo kali.
Alipoulizwa ni athari gani anazoziona kutokana na makundi hayo,
Warioba alisema; “Hakuna jipya, nimekwisha sema sana lakini kwa sasa
haya mambo ya siasa naomba mtuache.”
Jaji Warioba alisema sifa za kuwa kiongozi alishazisema hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1995.
Katika hotuba ambayo Mwalimu aliitoa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa
CCM waliokuwa wamekutana katika ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma mwaka
1995 kuchagua mgombea wa urais, alitaja sifa za mtu anayefaa kuwa
kiongozi bora ambazo mpaka leo zimekuwa zikitumiwa na wanasiasa na watu
wa kada mbalimbali kupima viongozi wao.
Mwalimu alitaja sifa nne kuu za kiongozi aliyekuwa akimtaka, moja
ikiwa ni mtu ambaye angeweza kupambana na rushwa, ya pili ilikuwa ni
kumpata mtu aliyekuwa anafahamu nchi ya Tanzania bado ni nchi ya
wakulima na wafanyakazi ambao bado ni masikini. Sifa ya tatu aliyoitaja
Mwalimu Nyerere ni mtu ambaye angepambana na udini pamoja na ukabila.
Suala la vijana kugombea nafasi ya urais na kutaka umri wa kuwania
nafasi hiyo upunguzwe, lilianza kupigiwa chapuo na baadhi ya wabunge
kuanzia mapema mwaka 2012.
Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba, ambaye pia ni Naibu Waziri
wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Mbunge wa Kigoma Kaskazini
(Chadema), Zitto Kabwe, walikuwa mstari wa mbele kutaka umri huo
upunguzwe kutoka miaka 41 sasa hadi 35.
Hoja hiyo iliingizwa hata wakati wa mchakato wa kuandikwa Katiba
mpya, lakini Tume ya Jaji Warioba haikuingiza suala hilo kwenye Rasimu
ya Katiba ambayo kwa sasa inajadiliwa na Bunge Maalumu la Katiba.
Wakati wa vuguvugu hilo la kupigia chapuo hoja hiyo, wakizungumza
kwenye Kongamano la Katiba na Vijana lililoandaliwa na Taasisi ya Femina
HIP, Dar es Salaam, Zitto na Makamba pia walitaka umri wa kupiga kura
uanzie miaka 16 badala ya 18.
Akichangia hoja, Makamba alisema ili kugombea urais katika nchi
nyingi za Afrika Mashariki, raia husika anatakiwa kuwa na umri wa miaka
35. “Hatutakuwa tumeanza sisi kwa sababu nchi nyingi duniani nafasi ya
urais inagombewa kuanzia miaka 35, kwa hiyo vijana tuangalie suala hilo
katika mchakato wa Katiba Mpya inayokuja,” alisema.
Makamba alisema Katiba Mpya inayokuja iwawezeshe vijana kupiga kura
wakiwa na umri wa miaka 16 badala ya 18: “Umri wa kuanzia miaka 16
unatosha kabisa kuchanganua ni kiongozi wa aina gani anafaa
kuchaguliwa.”
Kauli ya Makamba iliungwa mkono na Zitto, ambaye alizitaja nchi za
Kenya, Uganda na Burundi kuwa urais unagombewa kuanzia miaka 35.
Mtanzania
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment