Mufti Issa Shaaban Simba
SHEIKH Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Bin Shaaban Simba, amesema taifa
linaelekea pabaya kutokana na kushamiri kwa vitendo vya ulipuaji wa
mabomu vinavyofanywa na watu kwa nia ya kulipiza visasi.
Alisema kutokana na hali hiyo, vitendo hivyo vinaonyesha wazi vina
lengo la kuchochea uhasama kwa viongozi wa dini na waumini wao ili
kuvuruga amani ya nchi.
Mufti Simba aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu.
Alisema matukio hayo yameendelea kutokea kwa sababu ya vyombo vya dola kutokuwa na ufuatiliaji wa kutosha.
“Taifa linaelekea pabaya, kinachosikitisha zaidi ni kwamba, vyombo
vya dola ambavyo vimepewa dhamana ya kusimamia vimeshindwa kufuatilia
pindi matukio haya yanapotokea.
“Kitendo hiki kimesababisha wanaofanya vitendo hivi kujaa kiburi kwa sababu kinawapa jeuri ya kuendelea kutimiza azma zao.
“Siwezi kutabiri moja kwa moja kuwa vitendo vya ulipuaji wa mabomu
vinavyoendelea kutokea nchini vinahusiana na masuala ya kisiasa au la,
isipokuwa hali ninayoiona ni mpango wa watu wachache wa kuvuruga amani
ya viongozi wa dini na nchi kwa ujumla,” alisema Mufti Simba.
Alisema kama watu hawa wangekuwa wanakamatwa na kuchukuliwa hatua zinazostahili, matukio ya aina hii yangepungua.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona mambo ya dunia yanageuzwa kama sehemu ya kulipiza kisasi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia.
Alisema ipo siku watu wanaofanya unyama huo Mungu atawaumbua tu.
“Sisi viongozi wa dini hatupendi vitendo hivi viendelee kutokea
kwenye jamii yetu, kwani tunaumia mno kuona taifa linachafuliwa na watu
wachache wenye chuki za malipizi kwa watu wasiokuwa na hatia.
“Lakini hata kama ni kulipa visasi, basi isiwe kurushiana mabomu na
kujeruhi, kwani viongozi wa dini hawana uhasama wowote na hawahusiki na
mambo ya siasa, kwa hiyo wanachotakiwa ni kutubu na kumrudia muumba wao
katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
“Naomba vyombo vya dola vifanye kazi zake kwa umahiri na kuhakikisha
vinawakamata wahusika wote na kuwatia nguvuni ili kukomesha matukio ya
aina hii,” alisema Mufti Simba.
DK. SLAA
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.
Wilbrod Slaa, amelitaka Jeshi la Polisi kuwafikisha mahakamani viongozi
wa chama hicho waliodai wana ushahidi wa mtu aliyelipua bomu kwenye
mkutano wao mkoani Arusha.
Itakumbukwa tukio hilo lilitokea kwenye Uwanja wa Soweto Arusha Juni 16, mwaka jana na kujeruhi watu kadhaa.
Kauli ya Slaa imekuja siku moja baada ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai (DCI), Yesaya Ngullu, kudai kuwa viongozi hao hawana
ushahidi wa mtu aliyerusha bomu kwenye mkutano huo.
Alisema baada ya kutokea kwa tukio hilo, aliwaita viongozi hao na
kuzungumza nao kuhusu suala hilo, lakini mpaka sasa hakuna hata kiongozi
mmoja aliyetoa ushahidi.
Akizungumza na MTANZANIA mjini Dar es Salaam jana, Dk. Slaa alisema
polisi wanajua sheria na taratibu kwa mtu anayetoa ushahidi wa uongo
hadharani, baada ya kuwaona wamesema hivyo walipaswa kuwafikisha
mahakamani ili wachukuliwe hatua za kisheria.
“Kama wanajua tumesema uongo kwanini wasitupeleke mahakamani ili
tuchukuliwe hatua za kisheria, mbona walishindwa kuchukua taarifa zetu
zozote badala yake wakaamua kumwita mwenyekiti wetu, Freeman Mbowe
akajieleza,” alisema Dk. Slaa.
MBATIA
Kwa upande wake, Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia ameitaka Serikali
kuacha kulala usingizi wa pono katika kushughulikia matukio ya mabomu
yanayoendelea kugharimu maisha ya Watanzania.
Ameitaka Serikali na vyombo vyake vya dola kuingia kazini kwa
kuhakikisha usalama unarejea kwani damu za majeruhi katika milipuko ya
mabomu hayo zina athari kubwa kwa taifa katika siku zijazo.
Akizungumza jijini hapa jana, Mbatia aliyejitambulisha kuwa ni
mtaalamu wa majanga, alisema mtu mwenye jukumu la kwanza kuhakikisha
anawalinda raia wa nchi ni yule aliyeapa kulinda Watanzania na mipaka
yake.
“Nimetembelea eneo la tukio hali inasikitisha kabisa, yaani mwenye
mgahawa hajui lolote yupo yupo analalamika,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Hatuhitaji Serikali ambayo itakuwa inaweka maisha yetu rehani,
Serikali makini lazima ijue kesho kutatokea kitu gani sio bomu
linalipuka wewe umelala au unaenda kwenye kikao cha barabara.”
Alisema Serikali yoyote duniani kipaumbele chake cha kwanza huwa ni ulinzi na usalama wa wananchi wake na sio barabara.
MAJERUHI
Hadi kufikia jana majeruhi sita wa mlipuko huo wa bomu waliokuwa
wamelazwa katika Hospitali ya Selian jijini Arusha walisafirishwa
kuelekea jijini Nairobi kwa ajili ya matibabu zaidi.
Taarifa kutoka kwa jamaa za majeruhi zilibainisha kwamba, majeruhi
hao waliondolewa hospitalini hapo jana jioni kwa gari la kubebea
wagonjwa huku majeruhi wawili wakiendelea kupatiwa matibabu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tiba na Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali
ya Selian, Dk. Paul Kisanga, alithibitisha kupewa ruhusu kwa wagonjwa
hao sita huku akibainisha kuwa majeruhi aliyekatwa mguu bado anaendelea
na matibabu hospitalini hapo.
“Majeruhi sita wamepewa ruhusa ila mpaka sasa tunao majeruhi wawili
Deepack Gupta (25) na Prateek Jaley ndio wanaoendelea na matibabu.”
Taarifa hii imeandaliwa na Oliver Oswald, Patricia Kimelemeta, Grace Shitundu na Eliya Mbonea (Arusha).
Mtanzania
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment