Waziri mkuu nchini Iraq Nouri al Malik
Msemaji wa chama cha waziri mkuu nchini Iraq ameimbia BBC kwamba Nouri al Malik anajaribu kubuni serikali itakayoshirikisha kila mmoja ikiwemo watu wa dhehebu la kisunni walio na msimamo wa kadri.

Zuhair al Nahar amesema kuwa waziri mkuu alitaka kufungua awamu mpya katika siasa za iraq lakini akasistiza kuwa hatazungumza na kundi lolote lenye silaha ambalo linakabiliana na serikali.
Msemaji huyo ameongezea kuwa bwana Al Malik ana jukumu kubwa mbeleni na kwamba hatajiuzulu.
Kuhusu kampeni dhidi ya wanamgambo wa kisunni ,bwana Al Nahar amesema kuwa ana matumaini kuwa mashambulizi ya angani ya Marekani yatapunguza makali ya wapiganaji wa ISIS huku vikosi vya serikali vikiwakabili waasi hao.
Wapiganaji wa kisunni wa kundi la ISIS
Wakati huo huo, shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch, limesema kuwa kundi la wanamgambo wa kiislamu la ISIS huenda limewaua kati ya wanajeshi mia moja sitini na mia moja tisaini, wa Iraq, kufuatia hatua yao ya kuuteka mji wa Tikrit mapema mwezi huu.

Shirika hilo limesema haya kufuatia uchunguzi wao wa picha za satelaiti na pia picha za mitaro miwili iliyojaa miili ya binadamu.
Shirika hilo bado halijatembelea mji huo kuthibitisha madai hayo lakini limekubali kuwa idadi ya waathiriwa yaweza kuwa kubwa zaidi.

Kundi la ISIS liliweka picha hizo kwenye mtandao.
BBC
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top