Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba ameibua madudu yanayofanywa na Bodi za Mashirika na Taasisi za Serikali na kudai kwamba wakurugenzi wake wamekuwa wakifuja mamilioni ya fedha za umma kwa kufanya mikutano nje ya nchi.
 
Alisema kutokana na hali hiyo, Serikali imejipanga kuzuia matumizi yasiyokuwa na tija, ikiwamo fedha zinazotumika katika mikutano hiyo.
Akizungumza wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge zilizotolewa wakati wa kuchangia Muswada wa Fedha kwa mwaka 2014/15, alisema hali hiyo inatokea katika taifa ambalo wanafunzi wanakaa chini, dawa hakuna, maji shida na Serikali haina fedha hata za kuwapa mikopo wanafunzi.
“Hivi mnajua baadhi ya bodi zinafanya mikutano nje ya nchi? hivi mnajua baadhi ya mashirika, timu nzima ya watendaji wake wanakata tiketi za ndege daraja la kwanza na la pili, kwenda kufanya semina nje ya nchi mwezi mzima?” alihoji.
Alisema Serikali inataka Mlipaji Mkuu (Hazina) kuyakataa malipo ya aina hiyo ili bodi hizo zifanye vitu vyenye manufaa kwa taifa.
Aidha, aliziagiza taasisi, mashirika, idara na wakala wa Serikali, mikoa, manispaa, majiji na halmashauri zianze kutumia mfumo wa kielektroniki ili mapato yajulikane sambamba na matumizi.
“Hatuwezi tukawabana wafanyabiashara wadogowadogo kutumia mashine za kielektroniki wakati ofisi za serikali zinaendelea kutumia risiti za kuandika na kughushi wakati hazitoi sura halisi ya matumizi,” alisema.
Mwigulu alitangazia vita dhidi ya wakaguzi watakaopeleka serikalini madeni yenye shaka, akiwataka kutafuta kazi nyingine mara tu watakapobainika.
“Watendaji wa Serikali wanatakiwa kutambua kuwa kuna vijana wengi waliomaliza vyuoni lakini kazi hawana. Ni lazima tudhibiti matumizi ya fedha ili kila mtu aheshimu fedha za umma,” alisema. Akizungumza kwa ukali, Nchemba alimtaka Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, kupeleka mabadiliko ya sheria bungeni, ili kuruhusu kuwatimua kazi watumishi watakaobainika kupitisha madai hewa.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alisema kuwa Serikali itaendelea kufanya tathmini kuhusiana na misamaha ya kodi na ile isiyokuwa na tija.
Alisema wameanza na wataendelea kufanya tathmni kwa misamaha ambayo haitaathiri uwekezaji nchini na kwamba zoezi la kufuta misamaha hiyo litakwenda hadi kufikia asilimia moja ya pato la taifa.
Kuhusu miswada ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Usimamizi wa Kodi, Mkuya alisema miswada hiyo itawasilishwa katika vikao vya Bunge vinavyotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.

Akizungumzia maboresho ya huduma za bandari, alisema kuna changamoto bandarini lakini huduma zimeendelea kuboreshwa.
Alisema wameongeza muda wa kufanya kazi ambapo sasa wanafanya kazi saa 24 na kuongezeka kwa bandari kavu kutoka 12 hadi 16 na hivyo kupunguza msongamano.
Mkuya alisema kwa kuboresha huduma za forodha, ushuru wake umeongezeka kutoka shilingi bilioni moja kwa mwaka wa fedha 2008/2009 hadi kufikia Sh2.97  bilioni kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Kuhusu kodi za uchakavu, Mkuya alisema kuwa gari ambalo limetengenezwa chini ya miaka mitano halitatozwa kodi ya uchakavu.
Akichangia katika muswada huo, Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, aliisifia Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Andrew Chenge lakini akaitaka kuacha kulalamika.
Alisema kamati hiyo inaweza kulizuia jambo lolote hukohuko bila kuleta bungeni ikiona Serikali haisikii ama ni kiburi.
Halima alisema badala ya Serikali kutoza katika eneo la bandari imeacha kufanya hivyo kama ilivyoshauriwa na wabunge na badala yake kuendelea kutoza katika maeneo yaleyale ya kila mwaka.
“Kamati inalalamika tangu mwaka jana, mwaka huu, Serikali inakosa mabilioni, tunakuja tunatoza kodi feki, viroba, lipstiki na wanja. Hivi hii ni akili?”alihoji.
Alisema kuwa kamati hiyo iliyosheheni wataalamu ambao wamekuwa wakikaa kwa muda mrefu katika vikao lakini ukweli ni kwamba hawatalisaidia Taifa kama hawatalisaidia Bunge.
Halima aliuponda uamuzi wa kamati kuhusu Waziri wa Fedha kujivua madaraka ya kusamehe kodi ambapo kamati hiyo ilitaka arejeshewe madaraka hayo.
Alisema uamuzi huo ni aibu kwa kamati yenyewe na Bunge zima kwa kukataa njia ambayo Serikali imeona inafaa katika kuliletea Taifa maendeleo.
Mwananchi

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top