KAULI ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, kwamba
atamkata kichwa mbunge mwenzake, David Kafulila, wa Kigoma Kusini
(NCCR-Mageuzi), imeibua maswali mengi.
Je, Werema ana uzoefu wa kukata vichwa? Je, anataka kujifunzia kwa
Kafulila? Je, anataka kumkata kwa mikono yake mwenyewe au kwa kutumia
"Vijana wake?"
Je, hii ndiyo kauli inayopaswa kutolewa na kiongozi mwandamizi wa
Serikali? Kauli hii inaakisi hulka ya Werema au ya Serikali ya awamu ya
nne? Je, Werema anatambua nafasi yake katika Bunge na Serikali?
Je, wangapi wamekatwa vichwa kimya kimya kabla ya sakata hili la
Kafulila na Werema? Je, watakakwa wengine wangapi kabla ya mwaka huu
kuisha?
Je, kauli yake ni msimamo wa Serikali? Kama siyo, mbona wakubwa wa
Werema hawajamchukulia hatua yoyote? Je, kuna uwezekano kwamba Rais
Jakaya Kikwete atamwajibisha Werema kwa gadhabu yake hii inayotia doa
Serikali nzima?
Na hii ilikuwa kauli yake ya pili ndani ya wiki moja. Maana wiki hii
hii, Werema huyu huyu ndiye alimuita mbunge mwenzake "tumbili."
Na hii ilikuwa baada ya Kafulila kutaka mwongozo Bungeni kuhusu
hatua zilizochukuliwa na Serikali dhidi ya watuhumiwa wa wizi wa fedha
ya ESCROW ipatayo bilioni 200, katika sakata la kampuni ya kufua umeme
ya IPTL.
Ajabu, aliyesimama kutoa kauli ya Serikali ni Werema, ambaye ni mmoja
wa watuhumiwa wa wizi huo. Kafulila alipomtaka atangaze maslahi katika
sakata hilo, jibu la Werema lilikuwa ni kumuita Kafulila kuwa ni
tumbili. Ndipo na Kafulila akagadhibika na kumwita Werema mwizi.
Sakata jipya linaanza. Werema akasema anakwenda kumpiga Kafulila;
akainuka kwenda kumchapa Kafulila. Wabunge wenzake wakamzingira,
wakamzuia.
Katika hali ya kawaida, nia ya Werema kutishia kumchapa mbunge
mwenzake ni kosa la jinai. Tunapofika mahali ambapo kiongozi mwandamizi
wa Serikali, tena Mwanasheria Mkuu, anataka kupigana hadharani, na
mamlaka zilizo juu yake hazikemei, nani atasimamia haki kwa raia wa
kawaida wasio na madaraka?
Hata bila ya kauli ya nyongeza ya kukata kichwa cha Kafulila, wakubwa
wa kazi wa Werema walipaswa kuwa wamemuonya au wamemchukulia hatua
kali.
Serikali ile ile ambayo kila mara viongozi wake, wanapobanwa na vyombo
vya habari wanakimbilia kuhimiza waandishi wazingatie "maadili" ya
kazi yao, inawafunza nini Watanzania kwa kunyamazia tabia hii ya
Werema?
Na dalili za kuinyamazia tayari zimeanza kuonekana. Ni juzi tu, Spika
wa Bunge, Anna Makinda, amemtetea Werema waziwazi, akisema Kafulila
ndiye mwenye makosa, eti alimchokoza na kimkasirisha Werema!
Huu ni utetezi wa hovyo kutoka kwa kiongozi wa hadhi ya Spika wa
Bunge. Lakini hili limetufikirisha zaidi na kutukumbusha kauli za Rais
Jakaya Kikwete na Waziri. Mkuu Mizengo Pinda.
Rais Jakaya Kikwete aliwaamuru wana CCM kujichukulia sheria mkononi
dhidi ya wapinzani wao wa kisiasa. Alitoa kauli hii mwaka huu katika
kikao kikuu cha chama chake, akidai kuwa wameishiwa uvumilivu.
Inawezekana kauli na tabia hizi za kibabe anazoonyesha Werema zina
baraka za Rais Kikwete? Inawezekana utetezi wa Makinda ni sehemu ya
ukamilisho wa kauli ya Rais Kikwete, kwamba Werema aliishiwa uvumilivu?
Lakini hata kama kungekuwa ni kuishiwa uvumilivu, Kafulila angeweza kutamka neno "mwizi" kama Werema asingetamka "tumbili?"
Kati ya Kafulila na Werema, nani angeweza kudai kwa haki kwamba ameishiwa uvumilivu? Nani alimchokoza mwenzake?
Katika mwendelezo huo huo wa ubabe wa viongozi wa Serikali, hata Waziri
Mkuu Mizengo Pinda aliwahi kutamka Bungeni, kwamba wapinzani "wapigwe
tu!"
Ni kauli ya kikatili, hasa ikizingatiwa cheo na dhamana ya kiongozi
aliyeitoa. Ni sawa na kauli aliyowahi kutoa huko nyuma, wakati wa
sakata la mgomo wa madaktari uliokuwa unaongozwa na Dk. Steven
Ulimboka.
Pinda alisema, "liwalo na liwe!" Na kweli, lilikuwa. Muda mfupi
baadaye, Dk. Ulimboka aliokotwa msituni akiwa amepigwa, amefanyiwa
unyama usiomithilika.
Je, yawezekana ubabe wa Rais Kikwete na Waziri Mkuu wake Pinda ndio
umempa Werema jeuri ya kutamka haya hadharani bila haya, na bila hofu
ya kukemewa?
Anafanya hivyo kwa kuwa anajua hakuna anayeweza kumkemea? Anafanya hivyo kwa kuwa anajua hawezi kufukuzwa kazi?
Hasira yake inatokana na nini hasa? Ni sababu ya ukweli wa kauli ya Kafulila? Ni woga?
Amefanya jambo baya ambalo hana uzoefu nalo, na sasa anaona kama
Kafulila amemuumbua? Hasira zake hizi zinaakisi usafi wake katika sakata
la ESCROW?
Ni Werema huyu huyu ambaye huko nyuma aliwahi kubanwa kwa hoja na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Aliposhindwa kujibu hoja, akatoa kauli nyingine ya kihuni. Akasema,
"Mungu ametupatia vichwa ili tufikiri, lakini naona wengine wanatumia
vichwa kufuga nywele!"
Hakukemewa. Hakurejeshwa katika hoja. Hii ndiyo taswira ya Serikali
yetu? Ndiyo maana ya kauli mbinu yao "tumethubutu, tumeweza, tunasoma
mbele?"
Hata hivyo, wanatusaidia kujiuliza tena kwa msisitizo: Ubabe na gadhabu ya Werema vinalenga kuficha nini?
Ndiyo, kauli imetolewa na Werema, lakini wananchi wanamtolea macho Rais Kikwete! Naye anataka kichwa cha Kafulila?
Ni hivi, kama Rais Kikwete atataka kichwa cha Kafulila, Werema
atakikata tu, mithili ya Herode na kichwa cha Yohane Mbatizaji.
Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
1 comments:
Pumbavu kabisa werema.
Post a Comment