Yahya Khamis Hamad
Wakati umesalia mwezi mmoja na siku 10 kabla ya Bunge Maalumu la
Katiba kuanza tena vikao vyake mjini Dodoma kuendeleza mchakato wa
Katiba Mpya itakayowaongoza Watanzania kwa zaidi ya miaka 50 ijayo,
Mtendaji Mkuu wa Bunge hilo amesema kuwa bila kundi la Ukawa kurejea na
kushiriki hatua zote haitawezekana kupata Katiba Mpya.
Maandalizi ya Mkutano wa Pili wa Bunge Maalumu la
Katiba tayari yameanza na kikao cha kwanza kikitarajiwa kufanyika Agosti
5, huku ofisi ya Bunge hilo ikiwa na matumaini kuwa kundi la Ukawa
litarejea na kushiriki vikao vyote kwa manufaa ya taifa.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti
hili mjini Zanzibar, Katibu wa Bunge hilo Yahya Khamis Hamad, alisema
kuwa kukwama kwa mchakato huo kutatokana na kutotimia kwa idadi ya
wajumbe katika upigaji kura.
“Kikwazo kitabaki katika upatikanaji wa theluthi
mbili za uamuzi wa vikao vya Bunge hilo kwa mujibu wa kanuni
zilizopo,”alisema Hamad.
Kauli hiyo imekuja huku juhudi za watendaji wa
Bunge hilo kuwashawishi viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani
zikiendelea kwa kuwasihi waruhusu wabunge wao kurejea na kushiriki vikao
vya Bunge Maalumu la Katiba ili taifa lipate Katiba Mpya mwakani.
Hamad alisema kuwa ikiwa hali ya kukosekana
theluthi mbili itajitokeza, hakuna njia nyingine mbadala zaidi ya Katiba
ya mwaka 1977 kuendelea kutumika na kwamba hata mfumo wa Serikali
utabaki uleule.
Kwa nyakati, siku tofauti na mara kadhaa juhudi
zimefanyika kuwashawishi Ukawa kurejea bungeni bila mafanikio, huku
viongozi wa vyama vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi wakionekana kuweka
ngumu na kutoa masharti kwa Serikali, ndipo waafiki ombi hilo na kurejea
bungeni.
Msimamo huo wa Ukawa unatajwa kuendelea kuliweka
taifa pabaya ukiondoa matumaini ya kupatikana kwa Katiba Mpya baada ya
inayotumika sasa kutimiza miaka 50 na kuonekana kuwa ipo haja ya kufanya
mabadiliko.
Katibu wa Bunge Maalumu, Hamad anatoboa siri
akisema: “Pamoja na juhudi za Bunge kuwarejesha bungeni, bado
haijafahamika kama wabunge wa kundi la Ukawa watarejea au la.”
Akitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na ofisi
yake Hamad anasema ni pamoja na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel
Sitta kukutana na viongozi wa vyama hivyo kwa nyakati tofauti akiwamo
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad (Katibu Mkuu
wa CUF) mwenye ushawishi mkubwa kwenye kundi la Ukawa.
CUF ndicho chama chenye wawakilishi wengi katika
Bunge la Katiba kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wabunge na wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi.
Kwa mujibu wa Hamad, Sitta akiwa Zanzibar pia
alikutana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuzungumzia suala
hilo akihimiza na kuwataka wajumbe hao kurejea na kuhitimisha ngwe
iliyobaki.
Hata hivyo, Katibu huyo wa Bunge Maalumu la Katiba alisema kuwa kuendelea kwa Ukawa kubaki nje ya Bunge kama si njia mwafaka ya kufikia suluhisho, badala yake anaamini kuwa kila jambo gumu huweza kuzungumzika na kufikia tamati.
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Hata hivyo, Katibu huyo wa Bunge Maalumu la Katiba alisema kuwa kuendelea kwa Ukawa kubaki nje ya Bunge kama si njia mwafaka ya kufikia suluhisho, badala yake anaamini kuwa kila jambo gumu huweza kuzungumzika na kufikia tamati.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment