Andrew Chenge
HATIMAYE
Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Andrew Chenge, imeutosa kwa muda
muswada wa kufuta baadhi ya misamaha ya kodi na ule wa kodi kwa madai
haijapata muda wa kuipitia kwa undani zaidi.
Dalili za kamati hiyo kukwamisha muswada huo zilianza kusikika kwa
takriban wiki moja sasa baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa wafanyabiashara
wamewarubuni wajumbe wa kamati hiyo kwa kuwaeleza madhara ya kufuta
misamaha hiyo, ili wasikubaliane nao.
Juzi, Tanzania Daima liliandika juu ya uwepo wa hatihati ya
kufikishwa bungeni kwa muswada huo kutokana na mvutano mkubwa
uliojitokeza katika vikao vilivyokuwa vikifanyika baina ya Waziri wa
Fedha, Saada Mkuya Salum, wataalamu wa wizara hiyo na wajumbe wa Kamati
ya Bajeti.
Katika kikao hicho, serikali ilikuwa ikishikilia msimamo wa muswada
huo ufikishwe bungeni kabla ya Julai Mosi, ili uanze kufanya kazi
Januari mwakani, huku Kamati ya Bajeti ikitaka ipate muda zaidi wa
kuzungumza na wadau husika kabla ya kuupeleka bungeni.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, jana alitangaza kutokuwapo kwa muswada
wa kodi na ule wa VAT kwa kuwa Kamati ya Bajeti imeshindwa kuifanyia
kazi kwa sababu ilikuwa ikishughulikia bajeti ya serikali kwa mwaka
2014/2015 iliyopitishwa wiki iliyopita.
Makinda alisema Kamati ya Bajeti pia ilikuwa ikishughulikia muswada
wa sheria ya fedha uliopaswa ukamilike juzi, lakini kutokana na
marekebisho mengi ulikamilika jana asubuhi.
Kiongozi huyo wa Bunge pia alikemea tabia ya uzushi na kutuhumiana
kuhusu upokeaji rushwa zinazotolewa na wabunge dhidi ya wenzao waliopo
kwenye Kamati ya Bajeti.
Makinda alisema miswada ya VAT na kodi ni mizito na inapaswa
iwashirikishe wadau mbalimbali, hivyo Kamati ya Bajeti inahitaji muda
mrefu na kuwasikiliza wahusika, ili itakapofanya uamuzi uwe na manufaa
kwa taifa.
“Si tabia njema kuzua maneno… waandishi habari nao wanafanya jambo
hilo hilo mnalolifanya baadhi yetu, kuwasikiliza wadau ni jambo la
kawaida kabisa… sasa mnaposema Kamati ya Bajeti imehongwa na
wafanyabiashara ni majungu tu.
“Majungu hayajengi nchi, tukiendelea nayo tutaendelea kuwa wadogo na
wafinyu wa mawazo… majungu yenu ni hatari. Kamati ya Bajeti inaketi
mpaka usiku wa manane kututengenezea mambo tutakayojadili kwa urahisi na
ufanisi, tumeona kwenye bajeti ilivyokuwa,” alisema Makinda.
Alisema hakuna ubaya kwa wafanyabiashara kuwashawishi wajumbe wa
Kamati ya Bajeti au wabunge, lakini kibaya ni wabunge kuamua jambo kwa
kufuata masharti ya wafanyabiashara au wadau waliowasikiliza bila
kuchekecha vichwa vyao na kuangalia maslahi ya taifa.
“Ushawishi upo, si dhambi, hata sisi humo ndani tunafanya hivyo, sasa
kusema wafanyabiashara wameishika Kamati ya Bajeti si sahihi, ni
majungu, sisi humu ndani si wataalamu wa kila eneo, ndiyo maana wakati
mwingine tunalazimika kukutana na wataalamu husika na wengine tunatumia
fedha za Bunge kuwagharimia,” alisema.
Mwigulu amgomea Makinda
Baada ya maelezo hayo ya Makinda kuhusu miswada hiyo, Naibu Waziri wa
Fedha, Mwigulu Nchemba, aliomba mwongozo wa spika akionyesha
kutoridhika na sababu iliyotolewa dhidi ya miswada husika.
Mwigulu alisema miswada hiyo ilipitia kwenye wizara husika, makatibu
wakuu wa wizara mbalimbali kwa kushirikiana na wataalamu sekta tofauti
waliifanyia kazi na kujua haitokuwa na athari kwa taifa.
Alisema baada ya makatibu wakuu kumaliza kazi yao, miswada hiyo
ilikwenda kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri linaloongozwa na Rais
Jakaya Kikwete, kilichoridhia ipelekwe bungeni.
“Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, maoni ya
wapinzani, kamati mbalimbali kwa muda wa miaka minne zimekuwa
zikilalamikia misamaha ya kodi inavyoliumiza taifa, sasa leo serikali
imeuleta mnaanza kuleta maneno maneno na kuukwamisha.
“Tatizo letu ni kutochukua hatua mapema, Jiji la Abuja limechukua
ramani ya hapa Dodoma, wao wamelijenga jiji hilo na wanaishi, sisi mpaka
leo hii hatujafanya hivyo… kisa kuchelewa kuchukua hatua, serikali
imetambua kosa hilo, wabunge tunakwamisha,” alisema Mwigulu.
Watakaoumia
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Bunge, Mwigulu alisema
uamuzi wa spika utaathiri bajeti ya mwaka 2014/2015 na Wizara ya Fedha
imeamua kurejesha kodi kwenye mafuta, nondo, bati na saruji ambazo
zilikuwa zimeondolewa kodi.
Alisema katika bajeti ya mwaka huu waliamua kuondoa kodi kwenye
bidhaa hizo kwa kuwa walijua fedha zitapatikana katika misamaha ya kodi
watakayoifuta au kuipunguza.
“Tumesikitishwa sana na kilichotokea bungeni, lakini sisi tutarudisha
kodi tulizofuta kupitia muswada wa sheria ya fedha maana bila hivyo
hatuwezi kutoa maji, kujenga barabara, reli na huduma nyinginezo za
kijamii,” alisema.
Nje ya Bunge
Baada ya kuahirishwa kwa Bunge, Mbunge wa Nkasi, Ally Keisy, alisema
ni vema Bunge likavunjwa kwa kuwa rushwa imetawala kiasi cha kukwamisha
miswada yenye masilahi kwa taifa.
“Sote tunajua kukwama kwa miswada hiyo ni nguvu ya fedha za
wafanyabiashara wasiotaka kulipa kodi, hivi kila kundi lingekuwa
linakuja hapa kujitetea kama walivyofanya wafanyabiashara kwenye Kamati
ya Bajeti, serikali ingepata wapi kodi?” alihoji.
Bunge kuahirishwa mapema
Tanzania Daima lilidokezwa kuwa kuna uwezekano wa Bunge kuahirishwa
kabla ya Julai Mosi kama ilivyokuwa imepangwa kwa kuwa miswada ya VAT na
utawala wa kodi haitajadiliwa hivi sasa.
Baadhi ya wabunge waliozungumza na Tanzania Daima, walionyesha
kukasirishwa na miswada hiyo kutofika bungeni, huku wakidai kuwa hakuna
sababu za Bunge kuendelea hadi Julai Mosi.
Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment