Asema alipogombea 2005 alibaini kwamba mbali na rekodi
ya utendaji, kuna mambo mengine yanayohitajika katika kinyang’anyiro
hicho.
Waziri Mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim amesema hana mpango na hafikirii tena kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti
hili nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam jana, Dk Salim alisema
alipowania nafasi hiyo mwaka 2005, hakuwa na ufahamu mzuri kuhusu
mchakato huo lakini baadaye alibaini kwamba, mbali na rekodi ya
utendaji, kuna mambo mengine yanayohitajika katika kinyang’anyiro hicho
na kwamba hata watu wanaomfikiria na kutaja jina lake miongoni mwa
wanaoweza kuwania tena nafasi hiyo, wanakosea.
“Sifikirii tena, hii ni zamu ya kizazi kingine.
Ila nitaendelea kuisaidia nchi yangu katika nyanja mbalimbali kadri ya
uwezo wangu,” alisema.
Dk Salim ambaye mbali na uwaziri mkuu amewahi
kushika nafasi nyingine mbalimbali kitaifa na kimataifa, alisema uzoefu
alioupata katika kinyang’anyiro cha urais unatosha.
Alipoulizwa kama uzoefu huo ni mbaya au mzuri kwake, alisema ni mchanganyiko.
Dk Salim aliwahi kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa (UN) na kushindwa kutokana na kura ya veto ya
Marekani, pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za
Afrika (OAU), sasa Umoja wa Afrika (AU). Pia aliwahi kuwa Rais wa Bunge
Kuu la UN mwaka 1979 na 1980.
Licha ya kujitokeza mara moja kuomba uteuzi wa CCM
kuwania urais 2005, nyota yake katika nafasi hiyo ilianza kuwaka tangu
mwaka 1985 akiwa Waziri Mkuu pale aliposhindanishwa katika Kamati Kuu ya
CCM na aliyekuwa Waziri Mkuu, Rashidi Kawawa pamoja aliyekuwa Makamu wa
Rais wakati huo, Ali Hassan Mwinyi ambaye alipitishwa kiitifaki na
kushinda kiti hicho.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Makamu
mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa alisimulia jinsi Mwinyi
alivyopita, kwa sababu alikuwa Makamu wa Rais, hivyo wajumbe wa Kamati
Kuu walikosa hoja na sababu za kumwacha na kumchukua Waziri Mkuu
aliyekuwa chini yake kiitifaki.
“Makamu wa Rais ukimruka maana yake hatoshi, wakaona hawana maelezo hayo, ikabidi wamteue Mwinyi,” alisema Msekwa.
Sifa za viongozi
Katika hatua nyingine, Dk Salim alisema kuna
umuhimu mkubwa wa kuandaa viongozi hasa mtu anayekwenda kushika nafasi
ya urais atakayekwenda sambamba na mahitaji ya kizazi cha sasa
alichokiita cha ‘dot com’.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
“Hapa sizungumzii viongozi wa CCM au wa Chadema au chama
kingine, nazungumzia viongozi wa nchi watakaoweza kufanyia kazi matatizo
ya Watanzania.
“Ni vizuri viongozi wakaandaliwa, isiwe mtu
anaibuka tu anagawa hela halafu anashinda. Anatakiwa mtu atakayeweza
kushughulikia matatizo hayo. Watanzania ni wapole na wavumilivu lakini
wanazungumza. Hivyo anahitajika kiongozi atakayesikiliza mahitaji yao na
kutoa suluhisho, si kutoa ahadi za uongo,” alisema. Dk Salim alisema
katika kipindi hiki, anahitajika kiongozi atakayekuwa juu ya tofauti za
kisiasa, kidini, asili.
“Unajua hapa nchini kama ilivyo mahali pengine,
ukiingiza mgawanyiko wa kidini wakati familia nyingi zina watu wa dini
tofauti, wote wataathirika.”
Viongozi na rushwa
Akizungumzia tatizo la rushwa, Dk Salim alisema ni kubwa na kadri linavyoongezeka, linakuwa adui wa uwajibikaji, demokrasia.
Alisema katika enzi za utumishi wake nje ya nchi,
alikuwa akiona rushwa ilivyokithiri katika nchi mbalimbali, lakini hapa
nyumbani pakiwa salama hadi akawa anasema Tanzania ina bahati, kauli
ambayo hawezi kuisema sasa.
Dk Salim alibainisha kuwa uongozi unaoingia
madarakani kwa rushwa hauwezi kuwa mzuri kwa nchi na athari zake
zinaonekana hadi ngazi ya chini katika huduma za jamii kama mahakamani,
polisi na hospitalini.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment