Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akitangaza kuwaondoa
wakurugenzi mbalimbali wa wizara yake mbele ya waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam, jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amewaondoa
katika nyadhifa zao, Wakurugenzi mbalimbali kwa sababu zilizoelezwa
kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Hatua ya Nyalandu imekuja ikiwa ni utekelezaji wa
azimio la Bunge la Desemba 22, 2013 lililotaka Mkurugenzi wa Idara ya
Wanyamapori kuwajibishwa kutokana na tuhuma za uzembe na ukiukwaji wa
haki za binadamu katika Operesheni Tokomeza.
Nyalandu alisema: “Namwondoa Prof Alexander
Songorwa (Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori) na kumteua Paul Sarakikya
kukaimu nafasi hiyo.”
Alisema pia kuwa amemwondoa Mkurugenzi Msaidizi wa
Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Profesa Jafari Kidegesho kwenye
nafasi hiyo na Dk Charles Mulokozi ameteuliwa kushika wadhifa huo.
Mwingine aliyeteuliwa ni Julius Kibebe kuwa
Mkurugenzi Msaidizi Uzuiaji-Ujangili, nafasi iliyoachwa wazi na
Sarakikya wakati Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo, Utafiti na Takwimu,
Nebbo Mwina anabaki kwenye nafasi yake.
Nyalandu alisema Herman Keiraryo anaendelea kuwa
Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji wa Wanyamapori na kwamba
waliotangazwa kuondolewa kwenye nyadhifa, kazi zao mbadala zitatangazwa
baadaye.
Waziri Nyarandu alitoa siku 30 kwa Wakurugenzi
Wakuu wa kila Idara, Shirika na Taasisi za Wizara ya Maliasili na
Utalii, kutengeneza viashiria vya utendaji kazi (Key Performance
Indicators) na kuvikabidhi kwake.
Alisema hatua hiyo itafanikisha kufikiwa malengo
ya wizara hiyo, kwani uwajibikaji na ufanisi wa kazi za kila siku
utapimwa katika hali ya uwazi ili mikakati ya wizara itekelezwe katika
mifumo inayopimika na hatimaye kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Waziri huyo aliagiza kila mtumishi akiwamo yeye
mwenyewe, kutekeleza majukumu yaliyopangwa kwa kuzingatia kanuni za
mwenendo (code of conduct), zitakazopendekezwa na kupitishwa na Baraza
la Wafanyakazi la wizara hiyo.
Chanzo: Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment