Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo
Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu walimu waliomaliza masomo yao na kutopangiwa vituo vya kazi kuwa muda wa kufanya hivyo bado.
 
Akizungumza nje ya Viwanja vya Bunge jana mjini Dodoma, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema kuwa Serikali haijawasahau wala kushindwa kuwaajiri walimu waliomaliza masomo yao.
“Ni kweli wengi hawajapangiwa vituo vya kazi, lakini ndugu zangu Watanzania hebu muwe mnakumbuka kuwa ni muda gani huwa tunawapangia ajira walimu, mbona muda bado,”alihoji Mulugo.
Alisema kuwa muda wa kuwapangia walimu huwa ni kati ya Februari Mosi hadi Machi 30 mara baada ya wizara kupata vibali kutoka Utumishi.
Kuhusu walimu kupangwa na wengine kuachwa, alisema inatokana na bajeti ambayo wanakuwa wamepewa kutoka utumishi ambayo lazima inakuwa na ukomo wa idadi ya watu wanaotakiwa.
Hata hivyo alisema kuwa walimu ambao walimaliza na wana sifa za kufundisha wanapaswa kuwa na subira kwani kumbukumbu zao zipo na kwa vyovyote lazima Wizara itawaangalia.
Kuhusu taarifa iliyotolewa kuwa wako wanafunzi wa darasa la saba, ambao hawajui kusoma Kingereza kwa kiwango cha darasa la pili, alikataa kuzungumza kwa mada ni kuwa hana taarifa na utafiti huo.
“Siwezi kuzungumzia jambo ambalo utafiti wake umefanywa na watu wengine kwa malengo yao wenyewe, naomba wazungumze wao,” alisema.
Mjini Morogoro, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya elimu, bado kuna changamoto nyingi ikiwamo ya upungufu wa vifaa vya kutosha vya kujifunzia na kufundishia kama vitabu vya kiada.
Dk Kawambwa aliyasema hayo wakati akifungua kikao cha kazi cha Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri nchini na kuwa changamoto zilizopo zinahitajika kutatuliwa ili kiwango cha elimu kiendelee kukuwa na kuongeza uelewa kwa wanafunzi. 

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni ufaulu mdogo katika masomo ya sayansi, hisabati na lugha unaosababishwa na upungufu wa walimu, madarasa ya awali na msingi.
Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top