Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema atafurahi akiondolewa madarakani kwa kuwa kazi anayoifanya ni sawa na kubeba Msalaba mzito.
Pinda aliongeza kuwa iwapo anaonekana mzigo, Rais Jakaya Kikwete
anaweza kutengua uteuzi wake na akishindwa wabunge wana fursa ya kupiga
kura ya kutokuwa na imani naye.
Kauli hiyo aliitoa jana bungeni alipokuwa akijibu swali la papo kwa
papo, aliloulizwa na mbunge wa viti maalum, Rukia Kasim Mohamed (CUF),
aliyetaka kujua msimamo wake baada ya kutajwa ni mzigo namba moja katika
serikali.
“Tulipokuwa tukijadili taarifa za kamati mbalimbali mbunge mmoja wa
CCM alinukuu kauli ya Katibu Mkuu wa CCM kuwa wapo mawaziri
mizigo….mbunge huyo alisema wewe Waziri Mkuu ni mzigo namba moja, je
unaisemaje kauli hii?” alihoji.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema anasimamia zaidi ya wizara 20 hivyo
kumuita mzigo kwa sababu ya kutofanya vizuri kwa wizara moja au mbili
ni kutomtendea haki.
“Huwezi kuwa mzuri katika kila sehemu, inawezekana mbunge alikuwa na
mawazo yake lakini angeweza kuniambia mimi sikupendi kwa sababu ya moja
mbili tatu hapo mimi nafikiri ningeweza kujua nifanye nini,” alisema.
Pinda alisema anaweza kuondoka madarakani iwapo Rais Kikwete, ataamua
kutengua uteuzi wake lakini akishindwa wabunge wana fursa ya kufanya
hivyo kwa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.
Aliongeza kuwa kama ikitokea Bunge likapiga kura hiyo yuko tayari
kuwekwa kiti moto (kujieleza) na kama ikibidi ataondoka madarakani kwa
kuwa kazi hiyo ni kujitwisha Msalaba.
“Dada Rukia kama utafikia mahali unaona mimi sifai na ukaungana na
wabunge wote kuniondoa ……nitafurahi kwelikweli maana angalau nitapumua
kidogo kazi hii ni nzito sana; tunaibeba kama msalaba,” alisema.
Pinda aliongeza kuwa yeye na mawaziri wenzake wamekuwa wakifanya
jitihada kubwa kuyatimiza majukumu waliyonayo lakini kwa kuwa binadamu
si wakamilifu makosa hujitokeza.
Alisema uwaziri mkuu usiwasumbue wabunge kwa sababu kazi hiyo
haiombwi bali ni uteuzi wa Rais anayeona nani anafaa kuishika na akiona
mhusika haifanyi vizuri humuondoa.
Wiki iliyopita mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alisema mchawi
wa maendeleo ya nchi ni Waziri Mkuu Pinda na pia ni mzigo namba moja kwa
sababu amezidisha upole katika kuwasimamia mawaziri na watumishi
wanaofanya ufisadi.
Lugola alimtaka Pinda na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia, wajiuzulu mara
moja.
Shutuma za baadhi ya mawaziri kuwa mizigo zimekuwa zikitolewa mara
kwa mara ambapo hivi karibuni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana,
Katibu wa Itikadi na Unezi, Nape Nnauye, walisema Kamati Kuu (CC) ya
chama hicho itawahoji mawaziri hao.
Viongozi hao wa CCM wakiwa katika mikoa ya Mtwara, Mbeya, Njombe na
Ruvuma walisema baadhi ya mawaziri hawawajibiki ipasavyo hali
inayowafanya wananchi waichukie serikali.
Migiro aapishwa
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha-Rose Migiro,
jana alikula kiapo cha utii baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete
kuwa mbunge.
Migiro alipokelewa na kina mama wa CCM huku baadhi ya wabunge
wakipiga vigelegele pamoja na makofi na baadaye alisema kazi ya ubunge
ni utumishi kama ulivyo utumishi mwingine hivyo ni wajibu wa kila mbunge
kuwatendea haki wananchi.
“Mbunge ni sawa kama mtumishi mwingine, haijalishi ni mbunge wa jimbo
au wa kuteuliwa, cha msingi ni kufanya kazi na kila mtu bila kujali
itikadi ya chama chako,” alisema.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment