Rais Kikwete akiendesha kikao cha baraza la Mawaziri siku za hivi
karibuni. Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake
Rais Jakaya Kikwete, imeanza kuwahoji mawaziri waliotajwa ni ‘mzigo’ kwa
Serikali.
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake
Rais Jakaya Kikwete, imeanza kuwahoji mawaziri waliotajwa ni ‘mzigo’ kwa
Serikali.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye,
jana alilithibitishia gazeti dada la Mwananchi, The Citizen juu ya
kuanza kwa kikao cha Kamati Kuu (CC), lakini hakuwa tayari kuingia kwa
undani kuhusu ajenda.
Hata hivyo, habari za ndani zilieleza kwamba
miongoni mwa ajenda kuu za CC ni kuwahoji mawaziri wanaolalamikiwa na
wananchi, kwamba wameshindwa kutekeleza majukumu yao.
Wakiwa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Nape
aliwatupia lawama mawaziri wakati akielezea changamoto zinazowakabili
wakulima ambao ni asilimia 80 ya Watanzania, huku mawaziri husika
wakikaa kimya.
Mawaziri waliotajwa mzigo ni Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa; Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Christopher Chiza na Naibu wake, Adam Malima, kwamba
wameshindwa kazi na alipendekeza wang’olewe.
Hata hivyo, gazeti hili jana lilishuhudia mawaziri
kadhaa wakifika na kuingia kwenye mkutano wa CC, taarifa zingine
zilisema mawaziri waliofika kwenye kikao hicho walihojiwa na wajumbe wa
CC.
Kuhojiwa na CC
Mawaziri waliohojiwa na CC hadi kufikia saa 8:00
mchana jana walitajwa kuwa ni Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza. Mkuya ndiye
ambaye kwa sasa anaisimamia Wizara Fedha kutokana na Waziri wa Fedha, Dk
William Mgimwa kulazwa nchini Afrika Kusini akisumbuliwa na maradhi
ambayo hayajatajwa.
Waandishi wa gazeti hili jana waliwashuhudia
takriban mawaziri 10 wakiingia katika ofisi za makao makuu ya CCM,
Dodoma, maarufu White House, huku baadhi wakiwa si wajumbe wa CC.
Habari zilizotufikia jioni ziliwataja wengine kuwa
ni Dk David Mathayo David (Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi),
Hawa Ghasia (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa-Tamisemi), Dk Kawambwa, Celina Kombani (Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma).
Dk Kawambwa wakati akitoka kwenye kikao cha CC
aliulizwa na waandishi wa habari kilichotokea na yeye alijibu kwa
kifupi; “Mawaziri mizigo ndiyo tunatoka.”
Mawaziri ambao si wajumbe wa CC ni Mkuya, Chiza,
Dk Kawambwa, Hawa Ghasia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
anayeshughulikia Utawala Bora, George Mkuchika ambaye naye taarifa
zilidai alihojiwa.
Azimio la Bunge
Tayari Bunge limepitisha azimio la kumtaka Ghasia
pamoja na naibu mawaziri wake wawili, Aggrey Mwanry na Majaliwa Kassim
Majaliwa, kupima na kutafakari kama bado wanatosha kusimamia wizara
hiyo.
Kiini cha Bunge kupitisha azimio hilo ni taarifa
ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kubainisha kuwapo wizi,
ubadhirifu na mtandao wa ufisadi ndani ya Tamisemi, Halmashauri na
Hazina.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye baadhi ya
wabunge wamemtaja kama waziri mzigo namba moja, amesema yuko tayari
kuachia ngazi kama Rais ataamua kumwondoa katika wadhifa huo.
Pinda alitoa kauli hiyo juzi bungeni mjini Dodoma
wakati akijibu swali la papo kwa hapo kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalumu,
Rukia Ahmed (Cuf) aliyetaka aeleze anajisikiaje kuitwa mzigo namba
moja.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema yeye anasimamia
wizara 20, hivyo kama wapo watakaomhukumu kwa sababu ya wizara moja ama
mbili kutofanya vizuri basi watu hao watakuwa hawamtendei haki.
Alisema kama Rais atamwona ameshindwa kuwajibika
yuko tayari kuachia ngazi na endapo Rais hatafanya hivyo na wabunge bado
wakaona ipo haja hiyo, wampigie kura ya kutokuwa na imani naye.
Kauli ya CCM
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye,
mbele ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, alisema kuwa
mawaziri hao wameshindwa kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia Watanzania.
Alisema kuwa Waziri Chiza na Malima wamebaki
wakifunga tai na kuvaa suti mjini wakati wakulima wa Ruvuma na mikoa
mingine ya Tanzania wakiteseka.
Nape alisema Waziri Kawambwa naye anatakiwa
kuchukuliwa hatua kwa kuingia mkataba na kampuni ya ujenzi ya
Progressive iliyopewa zabuni ya kutengeneza barabara ya Namtumbo hadi
Tunduru wakati mkandarasi huyo hana uwezo wa kuijenga na matokeo yake
amefukuzwa kazi.
Dk Kawambwa ametupiwa lawama hizo kutokana na
kuipa kazi kampuni hiyo wakati akiwa Waziri wa Miundombinu pamoja na
kushindwa kusimamia elimu.
“Katibu Mkuu (Kinana), nilimuuliza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Chiza
na Malima wamefika lini kusikiliza matatizo ya wakulima wa tumbaku,
korosho na mahindi, alinijibu hakumbuki kama wamefika mkoani hapa.
Nikafuatilia na kubaini si yeye tu hata Waziri aliyetangulia Profesa
Jumanne Maghembe naye hakuwahi kufika. Najiuliza sababu nini, hakuna
majibu,” alisema Nape.
Alisema anasikitishwa na kitendo cha mawaziri hao
waliopewa dhamana kushindwa kutambua wajibu wao na kwamba umefika wakati
wa kuhojiwa na Kamati Kuu (CC) ya CCM, ili wachukuliwe hatua kwani bila
kufanya hivyo aibu itarudi kwa chama chake.
Wabunge wajitosa
Kikao hicho cha CC kinafanyika huku kikiwa na
taarifa kwamba wabunge wa chama hicho tawala wameanza kukusanya saini za
wabunge, ili kushinikiza kuitishwa kwa kikao cha wabunge hao au Party
Cocas.
Uchunguzi wa gazeti hili, uliofanywa kwa siku
kadhaa mjini hapa, umebaini kuwa wabunge wa CCM zaidi ya 160 wametia
saini katika fomu hiyo wakiwamo mawaziri zaidi ya 10.
Chanzo kimoja cha kuaminika kilisema kuwa fomu
hiyo iliwasilishwa katika ofisi ya katibu wa wabunge wa CCM, ikiambatana
na barua inayotaka kuitishwa kwa kikao kitakachowakutanisha.
“Tuliwaomba waitishe kikao cha wabunge wa CCM ili
mawaziri ambao tunawaona hawatimizi majukumu yao kikamilifu waweze
kuhojiwa lakini wakawa wanasuasua,”kilisema chanzo hicho.
“Lakini mmoja wetu akasema kwa kuwa wamepiga
chenga ya kukiitisha basi kuna nafasi ya kikanuni ya kukusanya saini za
wabunge zaidi ya nusu kushinikiza kuitishwa kwa kikao,”alisema mbunge
huyo.
Taarifa ya ziada na Habel Chidawali
Mbunge mwingine wa CCM alisema katika kikao hicho
wabunge walitaka kukutanishwa kwa pamoja kati yao, mawaziri wanaoonekana
kuwa mzigo na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
“Kikao hicho tulitaka kiwe Desemba 12 mwaka huu
ili tuanze kuwahoji mawaziri kabla ya CC lakini Mwenyekiti (Mizengo
Pinda), amekuwa akipiga danadana hadi leo (jana) inapokutana”alisema.
Habari zaidi zilisema baadhi ya wabunge wa CCM
walikutana faragha na Kinana juzi jioni na kumtahadharisha kama mawaziri
hao wasipowajibishwa, CCM kitakuwa na wakati mgumu.
Vuguvugu linaloendelea hivi sasa ndani ya wabunge wa CCM,
liliwahi kujitokeza Bunge la Aprili mwaka jana na kumlazimisha Rais
Kikwete kupangua Baraza lake Mawaziri Mei 4,2012.
Kung’olewa kwa mawaziri sita waliokuwa
wakishinikizwa na wabunge wajiuzulu kulitokana na taarifa za kamati za
kudumu za bunge na za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG).
Katika baraza lake hilo jipya, Rais aliwatosa
mawaziri waliokuwa wakishinikizwa kujiuzulu akiwemo Waziri wa Fedha,
Mustafa Mkullo na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami.
Wengine waliotoswa kwa shinikizo hilo lililoungwa
mkono na kambi ya upinzani ni wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, wa
Nishati na Madini, William Ngeleja na wa Uchukuzi, Omar Nundu.
Pia Naibu Waziri wa Uchukuzi wa wakati huo, Dk
Athuman Mfutakamba naye alitoswa sambamba na Waziri wa Afya, Dk Haji
Hussein Mponda na Naibu wake, Dk Lucy Nkya.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment