KATIBU wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Dar es
Salaam, Henry Kilewo, jana alihojiwa kwa muda na maofisa wa Jeshi la
Polisi kutoka makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam,
akihusishwa kutishiwa maisha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
(CHADEMA).
Kilewo aliwasili katika makao makuu ya jeshi hilo jana majira ya saa
06:03 mchana, akiwa ameongozana na wanasheria wawili pamoja na Diwani wa
Ubungo, Boniface Jacob, huku waandishi wa habari waliopiga kambi katika
eneo hilo la makao makuu ya Polisi kwa ajili ya kufuatilia
kinachoendelea wakilazimishwa kuondoka.
Baada ya kuwasili, Kilewo na wanasheria wake walifika katika eneo la
mapokezi na kujitambulisha, ambapo askari aliyekuwa na cheo cha
sajenti aliwaelekeza idadi ya watu wanaoruhusiwa kuingia katika chumba
cha mahojiano kuwa ni Kilewo mwenyewe na mwanasheria wake.
Hata hivyo maelekezo hayo ya polisi yalipingwa na wanasheria wa
Kilewo, John Malya, ambaye alishinikiza waingie wote kwa ajili ya
kusikiliza kile alichoitiwa mteja wao, hali iliyozua mabishano ya muda
kabla ya baadhi ya maofisa wa polisi kuridhia matakwa ya wanasheria hao
kuingia wote kwa ajili ya mahojiano.
Mara baada ya kuingia ndani, Kilewo na wanasheria wake walikaa kwa
zaidi ya saa mbili kabla ya kutoka, ambapo mwanasheria wake, Malya,
alizungumza na waandishi wa habari na kuelezea kile kilichosababisha
mteja wake kufika katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.
Malya alisema mteja wake alipata wito wa polisi kupitia simu ya
kiganjani kuwa anahitajika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya
mahojiano huku akiwa hajafafanuliwa ni mahojiano ya namna gani na
yanahusu jambo lipi.
Alisema baada ya wito huo wa njia ya simu walifika jana kuitikia wito, huku wakitaka kujua kilichosababisha mteja wao kuitwa.
“Kiutaratibu hawakufuata sheria, kwa kuwa hawakutoa hati ya wito au
ya kukamatwa na zaidi hakuna mtu aliyefungua mashitaka dhidi ya mteja
wangu,” alisema.
Aliongeza kuwa walipofika polisi waligundua kuwa mtu aliyefungua
malalamiko ya kutishiwa maisha na mteja wake kutakiwa kutoa maelezo
katika fomu ya onyo ya Jeshi la Polisi ni Zitto Kabwe.
Alisema hali ya kutakiwa kuweka maelezo katika fomu ya onyo ilizua
mjadala baada ya kutaka kujua kosa linalosababisha mteja wake kuhojiwa.
“Tuliwaambia wabadilishe fomu ya maelezo isiwe ya onyo, itumike ile
ya ripoti nao wakakataa, tukakubaliana pale panapoandikwa kosa la
mhusika papigwe mstari, kwa kuwa hawakutuambia mteja wetu anashitakiwa
kwa kosa lipi,” alisema Malya.
Alisema maelezo ya polisi waliyoyatoa kwao ni kuwa wanafanya
uchunguzi juu ya taarifa zilizoandikwa katika gazeti la Majira juu ya
Zitto Kabwe kutishiwa maisha na kwamba mteja wake alitoa maelezo na
kisha kujidhamini mwenyewe.
Kilewo atoa kauli
Akizungumza baada ya kutoka katika mahojiano, Kilewo
alisema Jeshi la Polisi linapaswa kubadilika na kufuatilia masuala ya
msingi na liache kujiingiza kwenye masuala ya siasa.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona polisi wanakuwa wa kwanza
kuwafuata wanasiasa huku wakishindwa kuainisha hatua waliyofikia katika
matukio ya kutekwa na kisha kujeruhiwa kwa mwandishi wa habari, Absalom
Kibanda, tukio la kutekwa na kuteswa kwa Dk. Stephen Ulimboka na
wengine.
“Nchi inakabiliwa na mambo makubwa, kuna uhalifu unaotishia maisha ya
Watanzania, badala ya polisi kuhangaika na hivyo wao wanageuka kuwa
wanasiasa,” alisema Kilewo.
Kwa upande wake Msemaji wa Jeshi la Polisi, SSP Advera Senso,
alikanusha kuwa wito wa katibu huyo wa CHADEMA hautokani na malalamiko
ya Zitto, bali ni utaratibu wa kawaida kwao kumuita mtu yeyote na
kuongea naye pale wanapoona kuna haja ya kufanya hivyo.
Kuhusu waandishi kufukuzwa katika eneo la polisi, Senso alisema
polisi haikuwa na haja ya kuita vyombo vya habari katika tukio hilo, na
kama mhusika aliviita, waandishi wa habari walipaswa waende katika ofisi
yake.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment