Hali ya wasiwasi iligubika eneo kinapofanyika kikao cha Kamati
Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilichoanza Dar es
Salaam jana.
Ulinzi mkali wa walinzi wa Chadema (Blue Guard),
uliimarishwa katika ukumbi wa Ubungo Plaza kinapofanyika kikao hicho
ambacho kinatarajiwa kumalizika leo, huku kukiwa na maagizo
yaliyoashiria kuwapo kwa mambo mazito.
Maazimio ya kikao hicho yanasubiriwa kwa hamu na
wafuatiliaji wa mambo ya siasa nchini kwani kinafanyika katika kipindi
ambacho chama hicho kikuu cha upinzani nchini kinapita katika misukosuko
na hasa ya malumbano baina ya makamanda wake wa juu.
Maelekezo ya ulinzi
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwasili
ukumbini hapo saa 5.20 asubuhi na baada ya kuingia, wapiga picha
waliruhusiwa kuingia kuchukua kumbukumbu ya tukio hilo kwa dakika moja
tu.
Waandishi wa habari hawakutakiwa kuingia na badala yake walielezwa kuwa wangepewa taarifa baadaye.
Wakati wapiga picha wakiwa ndani, mmoja wa wajumbe
wa mkutano huo alitoka na kutoa maelekezo kwa walinzi wa Chadema
akiwataka kuwa makini kutekeleza kazi yao watakapopewa amri ya kumwondoa
mjumbe yeyote mkutanoni.
“Kama mkipewa amri ya kuondoa mtu ingieni na
mtekeleze amri hiyo mara moja,” alisisitiza mjumbe huyo na kuingia ndani
haraka. Walinzi hao zaidi ya 10, walipokea maelekezo hayo kwa kutikisa
kichwa kuashiria kukubaliana na amri hiyo.
Kikao kufunguliwa
Kikao hicho ambacho kilifunguliwa dakika nane baada ya Mbowe kuwasili, kilipangwa kujadili mambo matatu jana.
Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo ambaye hakutaka
kutajwa jina lake alisema kingepitia taarifa za vikao viwili vya Kamati
Kuu vilivyopita.
Suala jingine ambalo lilipangwa kujadiliwa jana ni
ushiriki wa Chadema katika uchaguzi mdogo wa Mjumbe wa Baraza la
Wawakilishi Jimbo la Kiembesamaki, Zanzibar na kupitia taarifa ya fedha.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Leo moto
Ajenda zinazotarajiwa kujadiliwa leo ni pamoja na
ripoti ya utekelezaji wa Kampeni ya ‘Movement For Change’ (M4C) na hali
ya siasa.
Ajenda hiyo inatazamiwa kugusa matukio ya hivi
karibuni ndani ya chama hicho. Hayo ni pamoja na malumbano kati ya Naibu
Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
kuhusiana na masuala ya posho, kusimamishwa kwa Mwenyekiti wa Chadema wa
Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kuvunjwa kwa uongozi wa Mkoa wa Mara
na pia kuondolewa kikaoni kwa Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda.
Zitto na Lema waliingia katika vita ya maneno mwanzoni mwa Novemba kuhusiana na masuala ya posho ya vikao.
Vita hiyo ilianzishwa na Lema katika kikao cha wabunge wiki iliyopita aliposema kuwa Zitto anafanya unafiki kukataa posho.
Lema alimtuhumu Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini
kwamba anakataa posho za vikao bungeni, lakini anapokea posho nyingi
kutoka mashirika mbalimbali ya kijamii nchini.
Lema aliweka tuhuma hizo kwenye Mtandao wa Jamii
Forum huku akisema suala hilo halihitaji vikao vya chama kulijadili
isipokuwa vyombo vya habari na hususan, mitandao ya kijamii kwani hata
Zitto hutumia mitandao hiyo.
Akijibu hoja hizo, Zitto alisema tangu siku nyingi
alikwishapiga marufuku kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC) kupokea posho kutoka taasisi au mashirika yanayosimamiwa na kamati
hiyo.
Alisema tangu alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), alipiga marufuku posho na
pia aliwahi kuwashtaki Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru)
wabunge wanaochukua posho kutoka taasisi za Serikali.
Zitto pia alipata msukosuko mwingine baada ya
kusambazwa ripoti inayoitwa ‘Taarifa ya Siri ya Chadema’ iliyomtuhumu
kuwa alikuwa anashirikiana na CCM na viongozi wa Idara ya Usalama wa
Taifa kuhujumu chama hicho.
Ripoti hiyo inayodaiwa kuwa iliandaliwa na Idara
ya Upelelezi ya Chadema, ilieleza kuwa Zitto alikuwa akipokea fedha
kutoka kwa maofisa wa usalama na kuzisambaza kwa makada wengine wa chama
hicho ili wafanye kazi ya kukihujumu. Hata hivyo, Chadema kupitia kwa
Mnyika ilitoa taarifa kupinga vikali suala hilo.
CAG kukagua ruzuku
Pia, Zitto aliingia katika malumbano na chama chake baada ya kutuhumu vyama vya siasa kuwa hesabu zake hazikaguliwi na CAG. Chadema ilipinga vikali madai hayo na kueleza kuwa imekuwa inatumia taasisi binafsi kufanya kazi hiyo.
Pia, Zitto aliingia katika malumbano na chama chake baada ya kutuhumu vyama vya siasa kuwa hesabu zake hazikaguliwi na CAG. Chadema ilipinga vikali madai hayo na kueleza kuwa imekuwa inatumia taasisi binafsi kufanya kazi hiyo.
Suala jingine linalotazamiwa kujadiliwa katika
kikao hicho ni kusimamishwa kwa Mwigamba na Baraza la Uongozi Kanda ya
Kaskazini ambako kulizuka vurugu kiasi cha kunyang’anywa kompyuta
mpakato (laptop) baada ya kudaiwa alikuwa anasambaza taarifa za kuhujumu
chama hicho.
Suala lake linasubiri uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu kama lile la kuvunjwa kwa uongozi wa Chadema wa Mara.
Pia kitendo cha Baraza la Kanda ya Ziwa Mashariki
kumtimua Shibuda kwa madai kwamba halina imani naye nacho kina uwezekano
mkubwa wa kujadiliwa.
Zitto na Mnyika wakosekana
Zitto na Mkurugenzi wa Uenezi wa chama hicho, John Mnyika walikuwa miongoni mwa wajumbe walioshindwa kuhudhuria jana.
Zitto yuko na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC) huko Sudan Kusini na Mnyika pia yuko katika ziara ya
kibunge Uturuki.
0 comments:
Post a Comment