MTIKISIKO mkubwa umeikumba serikali huku Rais Jakaya Kikwete
akibanwa pande zote kutokana na mvutano mkubwa unaodaiwa kuibuka baina
ya mawaziri na viongozi waandamizi wa CCM.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi,
zimebainisha kuwapo kwa kutoelewana na kusukumiana lawama miongoni mwa
watendaji wa serikali, kuhusu kile kilichoitwa ‘kusalitiwa’ kwa
makubaliano yaliyofikiwa juu ya msimamo wa chama hicho, kuhusiana na
suala zima la mabadiliko ya Katiba.
Katika msuguano huo, baadhi ya vigogo ndani ya CCM wamekaririwa
wakisukuma lawama kwa Mwenyekiti wao, Rais Kikwete kwa kukubali haraka
kusikiliza hoja za wapinzani huku akijua kuwa walifikia uamuzi wa pamoja
kama chama na kukubali kupeleka muswada huo bungeni unaotokana na maoni
ya wanachama.
Mmoja wa vigogo hao alikaririwa akisema Jumamosi ya wiki iliyopita
kuwa hakutegemea kama Rais Kikwete angekiuka makubaliano hayo, kwa
sababu yamewapa ‘kichwa’ viongozi wa vyama vya upinzani.
“Tumejimaliza wenyewe bila sababu. Hakukuwa na haja ya kurejea
mazungumzo na hawa watu (wapinzani) kwa sababu, kila kitu kilitendeka
kisheria na wao ndio waliosusia mjadala.
“Tunawakatisha tamaa wanachama wetu, na hawataweza kutuelewa wala
kutupokea tena tutakapowaendea na jambo jingine, kwa sababu tunaamua
hivi na kutenda vile,” alikaririwa akizungumza mmoja wa viongozi wa
chama hicho katika mazungumzo yasiyo rasmi yaliyowakutanisha viongozi
watano waandamizi katika moja ya hoteli za kitalii jijini Dar es Salaam.
Mbali na msuguano huo, baadhi ya watendaji wa serikali kwa upande wao
wamesigana vikali, wengine wakiwasukumia lawama wenzao wanaodaiwa kutoa
matamshi kuhusiana na madai ya wapinzani ya kutaka kuwepo meza ya
mazungumzo.
Mawaziri, Stephen Wassira na Mathias Chikawe, walikaririwa hivi
karibuni wakisema kuwa hakuna nafasi kwa Rais Kikwete kukutana na
wapinzani katika jambo lililopitishwa kisheria na Bunge.
Wassira kwa upande wake alikwenda mbali zaidi na kutoa kauli ya kejeli
kwamba, rais hana muda wa kukutana na wapinzani waliokuwa na hamu ya
kwenda kunywa juisi Ikulu.
Mmoja wa mawaziri anayedaiwa kuchukizwa na kauli za watendaji wenzake,
inadaiwa amekuwa akihaha kuwashawishi wenzake kumshauri Rais Kikwete
awatimue ama awaombe mawaziri Wassira na Chikawe wajiuzulu ili kulinda
heshima yao, ya serikali na chama kutokana na kauli zao.
Hata hivyo, kuna habari kuwa baadhi ya vigogo wa CCM wameanza kuingiwa
hofu baada ya kuwapo taarifa za mipango ya kuungana kwa wapinzani
katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Hata hivyo, uchunguzi wa Tanzania Daima Jumatano umebaini kuwa hadi
sasa hakujafanyika mazungumzo yenye mwelekeo wa kuungana kwa vyama hivyo
katika suala la kumsimamisha mgombea mmoja wa urais ama kushirikiana na
kuweka mtu mmoja katika nafasi za ubunge.
Msimamo wa wapinzani
Wakati hali ikiwa hivyo, Umoja wa Vyama vya Upinzani vya
NCCR-Mageuzi, CUF na CHADEMA, umetangaza kusitisha maandamano ya kisiasa
yaliyokuwa yafanyike kesho.
Kusitishwa kwa maandamano hayo kumetokana na kauli ya Rais Jakaya
Kikwete kupitia vyombo mbalimbali vya habari kwamba atakutana nao kati
ya Oktoba 13 au 15 ili kuzungumzia madai ya kasoro walizoziona kwenye
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013
yaliyopitishwa bungeni hivi karibuni.
Lengo la maandamano hayo ilikuwa kumshinikiza Rais Kikwete asisaini
marekebisho ya sheria hiyo iliyopitishwa na wabunge wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kwa kuwa vipengele vingi vimewekwa kwa masilahi yao
badala ya taifa.
Akitoa tamko hilo kwa waandishi wa habari kwa niaba ya wenyeviti
wenzake, Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),
Profesa Ibrahim Lupumba, alisema umoja huo kupitia Kamati yake ya Ufundi
umesitisha maandamano hayo baada ya Ikulu kutoa taarifa kwamba ipo
tayari kukutana nao.
“Tumesikia kupitia vyombo vya habari ambavyo navyo vimenukuu taarifa
kutoka Ikulu kwamba Rais Kikwete amepanga kukutana na viongozi wa
upinzani kuanzia Oktoba 13 hadi 15 ili kujadili na kupata muafaka wa
suala la Katiba kwa vipengele tunavyovipinga.
“Tunaamini kuwa taarifa hizi ni sahihi kabisa, hivyo tumeamua
kusitisha maandamano yetu yaliyolenga kushinikiza nguvu ya umma kuungana
nasi katika kudai mchakato wa kuipata Katiba shirikishi na kushinikiza
rais kutosaini kabisa muswada huo wa Katiba kwa kuwa una upungufu,”
alisisitiza.
Alisema kutokana na nia aliyoionesha Rais Kikwete ya kulipatia
ufumbuzi suala hilo, vyama hivyo havina budi kusitisha kwanza mchakato
mzima wa maandamano na mikutano hiyo ya hadhara hadi pale mazungumzo na
rais yatakapokamilika na kutoa dira ya kinachoendelea.
“Pamoja na kusitisha maandamano haya tunapendekeza huo mkutano
ulioahidiwa na rais ufanyike mapema ili mchakato wa Katiba unaosuasua
kwa sasa uendelee kwa ufanisi na kuwezesha kupatikana kwa Katiba
iliyoandaliwa na Watanzania wote,” alisema.
Alisema madai ya umoja huo ni kuwapo kwa mchakato wa Katiba
shirikishi, utakaoheshimu matakwa ya Watanzania wote wa Bara na Visiwani
ili kuweza kupata Katiba iliyotengenezwa na wananchi wenyewe.
Hata hivyo, pamoja na umoja huo kuyasitisha maandamano hayo, tayari
Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Suleiman Kova, alishayapiga marufuku, kwa madai kuwa
yatasababisha usumbufu kwa wasafiri wengine na kupendekeza wafuasi wa
vyama hivyo wakutane katika viwanja vya Jangwani bila maandamano.
0 comments:
Post a Comment