Tundu Lissu
MNADHIMU wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu,
amesema kuwa watapima kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu muswada wa
sheria ya mabadiliko ya katiba, watakapokutana leo katika Kamati ya
Katiba, Sheria na Utawala.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Lissu
alisema kuwa Rais Kikwete katika hotuba yake kwa taifa juzi alisema kuwa
suala hilo linazungumzika.
“Mimi ninataka kuona leo kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala
liwepo suala hilo katika ratiba kati ya mambo yatakayojadiliwa tayari
kwa ajili ya kurejesha muswada bungeni.
“Kama suala hilo halitakuwepo, basi hotuba ya rais itakuwa ni porojo
za Magogoni (Ikulu). Rais asiposaini muswada huo ataonyesha nia nzuri
aliyokuwa nayo, na hayo tuyaone katika ratiba ya kamati,” alisema.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) na msemaji
mkuu wa kambi hiyo kwa Wizara ya Katiba na Sheria, alieleza mshangao
wake kwa Rais Kikwete kuhutubia taifa kwa habari za kuambiwa, kuelezwa
na kufahamishwa bila yeye kujiridhisha.
Alisema kuwa rais alimtuhumu kwa kumuita “mzushi na muongo mtupu
mwenye kauli za kinafiki, fitina na uzandiki wa hali ya juu”, lakini
akahoji ni kwanini anawataka wapinzani wakae mezani wazungumze naye
wakati ni waongo.
“Hoja zangu zilihusu Zanzibar kutokushirikishwa katika mchakato wa
kuboresha muswada wa mabadiliko ya sheria, nilisema hakuna mdau hata
mmoja au mtu binafsi aliyeonana na wajumbe wa kamati.
“Kwa upande wa bara kulikuwa na wadau 22, ukijumlisha na vyama vya
siasa 22, hivyo bara peke yake tulisikiliza wadau 44. Je, fitina,
uzandiki na uongo anauosema Kikwete upo wapi?” alihoji.
Lissu alitaja baadhi ya taasisi za bara walizokutana nazo kuwa ni
Ongeza Elimu ya Juu, vyama vya siasa na watu binafsi mfano Jaji Mkuu
mstaafu, Barnabas Samatta na Prof. Issah Shivji.
Alisema kuwa kwa Zanzibar walipewa ratiba ya kutembelea miradi ya
Tasaf, ofisi ndogo ya Bunge na ofisi ya Makamu wa Rais, na kwamba
walilalamika kubadilishiwa ratiba hiyo wakiwa Zanzibar.
“Tuliambiwa na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah tungepewa fedha
za kukaa Zanzibar hata kwa wiki nzima, na tulilipwa fedha nyingi tofauti
na tunavyolipwa kwa utaratibu wa kawaida,” alisema.
Lissu alisema kuwa Kikwete aliwahakikishia Watanzania kuwa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar ilishirikishwa, lakini Waziri wa Sheria wa Zanzibar
alisema kuwa walipelekewa muswada na Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Wiliam Lukuvi na kuwataka
watoe maoni siku hiyo hiyo.
Kwamba Wazanzibari waliona mambo manne waliyopelekewa katika muswada
wa mabadiliko ya sheria hayakuwa na shida wakasema sawa, lakini muswada
uliopelekwa bungeni ulikuwa na mambo zaidi ya 11.
“Je, hapa kuna uzandiki? Unafiki uko wapi? Je, na waziri huyo wa Zanzibar naye ni mwongo?” alihoji.
Aliongeza kuwa Rais Kikwete katika hotuba yake alisema ‘ameambiwa’,
‘ameelezwa’ na ‘amefahamishwa’, maneno ambayo ameyatamka mara tisa, na
hivyo kuhoji inakuwaje rais anahutubia taifa kwa maneno ya kuambiwa
ambayo kisheria hayana nguvu?
“Rais ana uwezo wa kukataa muswada na ana mamlaka ya kukataa mambo ya
kijinga yanayopitishwa na wabunge. Tunaomba asisaini muswada huo.
“Rais wetu afanye kama Obama aliyenukuliwa siku za hivi karibuni
akisema wabunge wakipitisha mambo ambayo hayana tija kwa taifa
hatasaini,” alisema.
Akizungumzia athari za haraka kama rais atasaini muswada huo, Lissu
alisema nchi itapata katiba mbovu ya hovyo na matukio ya vurugu kama ya
Zimbabwe na Kenya yatajitokeza Tanzania.
Alisema kuwa nchi hizo zilifikia hapo baada ya serikali kujidai
inahodhi muswada wa katiba, ikijipendelea yenyewe badala ya kusikiliza
wananchi waseme.
Kuhusu wadau ambao waliwasilisha majina halafu rais akateua kadiri
alivyoona bila kuteua majina hayo, Lissu alisema hayo hayakuwa mawazo
yake, bali aulizwe mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki, Dk.
Charles Kitima na Mchungaji Rohho wa CCT.
Kwa wawakilishi wa Shirikisho la Vyama Vya Wenye Ulemavu (Shivyawata),
Lissu alidai kuwa walisema kuwa Alshaymar Kweygir, rais ndiye anajua
alivyomteua kwani hawakumpendekeza.
0 comments:
Post a Comment