Rais Jakaya Kikwete
HATIMAYE Rais Jakaya Kikwete amekata mzizi wa fitina kuhusu
muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba unaopigiwa kelele na vyama
vya siasa na wadau, akiwataka warudi mezani kujadiliana na serikali.
Rais Kikwete alitoa rai hiyo jana katika hotuba yake ya mwisho wa
mwezi uliopita akisema: “Kama dhamira yetu ni kutaka kupata katiba mpya
kwa mujibu wa katiba na sheria, ushauri wangu na rai kwa ndugu zetu wa
CHADEMA, CUF na NCCR-Maguezi ni kuwa waachane na mipango ya maandamano
na kufanya ghasia.”
Badala yake aliwataka watumie njia halali zinazotambulika kikatiba na
kisheria kujenga hoja za kufanya marekebisho wanayoyaona wao yanafaa
kuboresha sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba.
“Tukifanya hivyo tutakuwa tunajenga badala ya kubomoa. Tutaliponya taifa. Sisi katika serikali tuko tayari,” alisema.
Katika hotuba hiyo, pia aligusia masuala mbalimbali kama vile
operesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu nchini, shambulio la kigaidi
nchini Kenya na mafanikio ya ziara yake nje ya nchi.
Alisema kuwa hivi sasa tume inaandaa mapendekezo ya rasimu ya pili ya katiba itakayopelekwa kwenye Bunge Maalumu.
Kwamba baada ya tafakuri zake, Bunge Maalumu litatoa rasimu ya mwisho
ya katiba ambayo itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya uamuzi wa mwisho
kupitia kura ya maoni.
Alisema kuwa baada ya Bunge la Novemba, 2011 kupitisha sheria ya
mabadiliko ya katiba, kulikuwepo na madai ya kutaka sheria hiyo
iboreshwe kutoka vyama vyote vya siasa vikiwemo vyama vya upinzani na
chama tawala.
“Majadiliano yalifanyika baina ya serikali na vyama hivyo pamoja na
shirikisho la asasi za kiraia. Makubaliano yalifikiwa kuwa marekebisho
yafanyike kwa awamu,” alisema.
Kwa mujibu wa rais, awamu ya kwanza ilihusisha Tume ya Mabadiliko ya
Katiba kisha hapo yafanyike marekebisho yanayohusu Bunge Maalumu na
mwisho kura ya maoni.
Alisema kuwa kama ilivyokuwa kwa mabadiliko yaliyohusu Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, safari hii nayo vyama vya siasa vilitoa
mapendekezo yao.
Kwamba yalifanyika mazungumzo kati yao na serikali na maelewano
kufikiwa kuhusu maeneo ya kufanyiwa marekebisho. Serikali ilitayarisha
rasimu ya muswada na kuuwasilisha kwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitoa mapendekezo yake na ushauri
kwenye maeneo mawili. Kwanza kwamba uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu
ufanywe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na
kuafikiana na Rais wa Zanzibar.
“Pili walishauri kwamba kama Bunge Maalumu litashindwa kufikia
maamuzi ndani ya siku 70 zilizopendekezwa, liweze kuongezwa muda hadi
kufikia siku 90,” alisema.
Alisema kwa kuzingatia utaratibu wa kutunga sheria, serikali
ilifikisha muswada kwa Spika wa Bunge ambaye nae aliuwasilisha kwenye
Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala.
Kama ilivyo ada, kamati hiyo ilifanya vikao na wadau na kupokea maoni
yao kuhusu muswada. Kwamba aliambiwa kulikuwa na mjadala wa kina na
mapendekezo mazuri yalitolewa na wadau.
Alisema kisha wajumbe wa kamati walikaa wenyewe kujadili muswada,
wakiwepo pia wabunge ambao si wajumbe wa kamati walioshiriki kwa vile
kanuni zinaruhusu.
“Nimeambiwa pia kwamba mjadala ulikuwa mpana na wa kina zaidi.
Mapendekezo kadhaa yalitolewa na wajumbe kuhusu vifungu mbalimbali vya
muswada,” alisema.
Rais aliongeza kuwa alifahamishwa kuwa wabunge wa vyama vyote
walichangia, na kwamba baadhi ya nyakati mambo yalipokuwa magumu mawazo
mazuri ya baadhi ya wabunge wa upinzani yalisaidia kupata ufumbuzi.
Alisema kuwa aliambiwa pia kwamba wajumbe wa kamati na upande wa
serikali walikubaliana kwa maeneo mengi isipokuwa machache ambayo
walikubaliana kwa pamoja wayapeleke bungeni ili wabunge nao wayajadili
na kuyapatia ufumbuzi.
Kwamba baada ya kamati kumaliza kazi yake, Waziri wa Katiba na
Sheria, Mathias Chikawe aliwasilisha muswada bungeni, akifuatiwa na
Gosbert Blandes kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Katiba, Sheria na Utawala, kutoa maoni ya kamati.
Baadaye Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu alitoa maoni yake.
Kuwa baada ya watu hao watatu kutoa maoni yao ilitarajiwa kuwa wabunge
wangeanza kujadili muswada.
“Naambiwa mambo hayakuwa hivyo. Badala yake kukazuka malumbano baina
ya Spika na baadhi ya wabunge wa upinzani wakitaka muswada usijadiliwe.
“Ilifikia wakati hoja hiyo ikabidi iamuliwe kwa kura ambapo
ilishindwa. Katika hali isiyotarajiwa, wabunge wote wa upinzani
wakatoka nje ya Bunge isipokuwa wawili,” alisema.
Rais alisema kitendo hicho kimewanyima wabunge wengi wa upinzani
fursa ya kutetea hoja zao walizozitoa kupitia hotuba ya msemaji wao, na
kwamba walijinyima nafasi ya kusema mambo mengine wakati wa mjadala na
Kamati ya Bunge zima.
Alisema uwa wabunge waliokuwepo waliendelea kuujadili muswada na kutoa hoja na mapendekezo ya kuuboresha.
“Walifanya hivyo wakati wa mjadala na wakati wa kupitia kifungu kwa
kifungu. Baadhi ya hoja na mapendekezo yalikubaliwa na mengine
yalikataliwa. Miongoni mwa yaliyokubaliwa ni kuhusu elimu ya mtu
atakayekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu na lile la ukomo wa uhai wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Kwa maoni yangu madai ya Kambi ya Upinzani yanazungumzika na hata
baadhi yangeweza kukubalika kama wabunge wake wangekuwepo bungeni na
kushiriki mchakato wote wa kujadili na kupitisha miswada bungeni.
“Baada ya kupoteza fursa yao halali, kutaka kupata ufumbuzi nje ya
Bunge ni jambo lisilowezekana. Haya ni masuala yanayohusu Bunge
ambayo hujadiliwa na kuamuliwa bungeni na si vinginevyo,” alisema.
Alisema kuandamana nchi nzima au kuchukua hatua za kutotii sheria
kama Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe anavyotaka, hakutaleta
mabadiliko wanayoyataka katika sheria hiyo.
“Naomba hekima ziwaongoze viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi na
zituongoze sote kutumia utaratibu tulioutumia mwaka 2012.
“Kulipotokea mazingira kama haya pande zote zilikaa pamoja na
kuzungumzia hoja moja baada ya nyingine na kukubaliana nini kifanyike
na kifanyike vipi. Baada ya kuridhiana hatua zipasazo za kisheria na
kanuni zilichukuliwa na kumaliza mzozo,” alisema.
Aliongeza kuwa kufanya kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo
huu na kutaliingiza taifa kwenye matatizo yasiyokuwa ya lazima.
“Tukikataa kufanya hayo Watanzania wanayo kila sababu ya kuhoji
dhamira zetu na kutilia shaka nia zetu. Watakuwa na haki ya kuuliza nia
ni hii yetu sote ya kupata katiba mpya kwa kutumia njia za kikatiba na
kisheria au tuna dhamira nyingine iliyojifisha?” alisema.
Rais Kikwete alisisitiza kuwa hawatengenezi katiba ya chama fulani
bali katiba ya nchi, katiba ya watu wa vyama vyote na wasiokuwa na
vyama ambao ndio wengi kuliko wote.
“Lazima tuongozwe na ukweli huo na tuwe na msimamo huo wakati wote.
Lazima tukumbuke kuwa si watu wote wanaostahili au kuwa na sifa, ambao
wataomba na kupata nafasi ya kuwa wajumbe, hivyo wale wachache
watakaobahatika lazima wawasemee wote,” alisema.
Ushirikishwaji wa Z’bar
Katika hilo, rais alisema kuwa alielezwa kwa kiasi gani Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar ilivyoshirikishwa na kutoa maoni yake
yaliyojumuishwa katika muswada.
“Hivyo basi napata tabu kuyaelewa madai kwamba Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar haikushirikishwa msingi wake nini! Labda kuna kitu
sikuambiwa,” alisema.
Alisema kuwa aliulizia kuhusu hoja ya kamati kutokufanya vikao
Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau, akaambiwa kuwa kanuni za Bunge
hazina sharti hilo, hivyo kamati haistahili kulaumiwa.
“Kama hivyo, nashauri kuwa suala hili lirudishwe bungeni ili wabunge
walizungumze na kulifanyia uamuzi muafaka. Vinginevyo watu wataendelea
kulaumiana isivyostahili,” alisema.
Alisema kuwa aliambiwa pia kuwa kulikuwa na hoja ya kutaka idadi ya
wajumbe wa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar iwe sawa kama ilivyo kwenye
Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Rais alifafanua kuwa ni kwa maelewano ya wote (consensus) na siyo kwa
kupiga kura. Ndiyo maana idadi imewekwa sawa ili sauti za pande zote
zisikike sawia.
Alisema kuwa Bunge Maalumu lina sharti la kufanya uamuzi kwa theluthi
mbili ya kura za kila upande kukubali. Bila ya hivyo hakuna uamuzi.
“Hivyo basi, katika Bunge Maalumu nguvu si uwingi wa kura ambazo
upande fulani unaweza kupata, bali ni ulinganifu sawa wa kura za kila
upande peke yake. Huu ndiyo msingi unaotumika katika Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania hivi sasa kwa lengo la kulinda maslahi ya
Zanzibar,” alisema.
Alisema kuwa anadhani inafaa ibaki ilivyo. Lakini kama wabunge
wataamua waongeze idadi, itakuwa kwa sababu nyingine siyo hiyo ya mfano
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Tume ya Warioba
“Katika orodha ya madai ya ndugu zetu wa upinzani, lipo suala la
uhai wa Tume ya Katiba. Wanataka usiishe wanapokabidhi rasimu ya pili
kwa Bunge Maalumu bali waendelee kuwepo mpaka mwisho wa mchakato.
“Nimeulizia ilikuwaje? Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani na
mapendekezo ya serikali wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na
Utawala. Limetokana na pendekezo la mbunge katika Bunge wakati wa
kupitia vifungu na kuungwa mkono na wabunge wengi.
“Kwa hiyo kuilaumu serikali si haki. Serikali inaweza kuwa mshirika
katika hoja hii. Nami naiona hoja ya wajumbe wa tume kuwa na wajibu
wakati wa Bunge Maalumu hasa wa kusaidia kufafanua mapendekezo ya
tume,” alisema.
Alihoji kuwa ushiriki huo uwe vipi? Je, ni wajumbe wote au baadhi yao na kusema kuwa hilo ni jambo linaloweza kujadiliwa.
0 comments:
Post a Comment