KAMATI YA MTIGINJOLA YATUPA MAOMBI YA ‘REVIEW’

KAMATI ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inayoongozwa na Idd Mtiginjola imetupa maombi ya kufanyia marejeo (review) uamuzi wake kama yalivyowasilishwa mbele yake na waombaji watano.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za TFF, Dar es Salaam jana mchana (Februari 18 mwaka huu), Mtiginjola ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo amesema wamepitia Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi za TFF na kubaini kuwa hakuna Ibara yoyote inayotoa fursa ya review kwa uamuzi ambao wameshaufanya.

Amesema Kanuni za Mwenendo wa Madai (CPC) katika mahakama za kawaida zinaruhusu Hakimu aliyefanya uamuzi katika kesi kufanya marejeo, lakini katika masuala ya mpira wa miguu hakuna fursa hiyo, hivyo hawawezi kujitungia kitu kipya kwani kazi yao ni kufanya uamuzi kwa kutafsiri Katiba na kanuni walizopewa na mamlaka ya uteuzi (TFF).

Waombaji watano waliokuwa wakitaka Kamati hiyo ifanyie marejeo uamuzi wake kutupa rufani zao ni Jamal Emil Malinzi aliyeenguliwa kugombea urais wa TFF na Hamad Yahya aliyeondolewa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board).

Wengine ambao waliomba kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na Kanda zao kwenye mabano ni Eliud Peter Mvella (Iringa na Mbeya), Farid Salim Nahdi (Morogoro na Pwani) na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu).


SIMBA YAINGIZA MIL 134/-, AZAM MIL 34/-
Kikosi cha Timu ya Simba

Kikosi cha Timu ya Azam


PAMBANO la Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na Libolo FC ya Angola lililofanyika jana (Februari 17 mwaka huu) limeingiza sh. 133,795,000 wakati lile la Kombe la Shirikisho kati ya Azam na El Nasir ya Sudan Kusini lililochezwa juzi (Februari 16 mwaka huu) limeingiza sh. 34,046,000.

Watazamaji 22,469 walikata tiketi kushuhudia mechi ya Simba kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000. Simba ilipoteza pambano hilo kwa bao 1-0.

Mgawo wa mechi hiyo ulikuwa kama ifuatavyo; gharama za waamuzi sh. 24,926,500, gharama za tiketi sh. 7,410,000, asilimia 15 ya uwanja baada ya kuondoa gharama za waamuzi na tiketi ilikuwa sh. 15,218,775, asilimia 10 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 10,145,850 na asilimia 75 iliyokwenda klabu ya Simba ni sh. 76,093,875.

Mechi ya Azam iliyomalizika kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 ilishuhudiwa na watazamaji 13,431 kwa viingilio vya sh. 2,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000. Mgawo katika mechi hiyo ulikuwa kama ifuatavyo;

Gharama za tiketi sh. 4,779,000, asilimia 15 ya uwanja baada ya kuondoa gharama za tiketi ilikuwa sh. 4,390,050, asilimia 10 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 2,926,700 na asilimia 75 iliyokwenda Prime Time Promotions (Azam) ni sh. 29,267,00.

PONGEZI KWA UONGOZI MPYA SPUTANZA, FRAT
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Wachezaji Mpira wa Miguu Tanzania (SPUTANZA) na wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) uliochaguliwa wiki iliyopita.

Uongozi wa FRAT ulichaguliwa Februari 13 mwaka huu mjini Morogoro wakati wa SPUTANZA ulichaguliwa Februari 17 mwaka huu katika uchaguzi uliofanyika Kigamboni, Dar es Salaam.

Waliochaguliwa kuongoza SPUTANZA na hawakuwa na wapinzani ni Musa Kissoky (Mwenyekiti) na Said George (Katibu Mkuu) wakati Ali Mayai aliwashinda Isaac Mwakatika na Hakim Byemba katika nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.

Kusianga Kiata na Charles Mngodo walichaguliwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya SPUTANZA. Katika uchaguzi huo uliohudhuriwa na wapiga kura 17, Mhazini na nafasi moja ya mjumbe wa Kamati ya Utendaji zitajazwa baadaye kutokana na kukosa wagombea.

Kwa upande wa FRAT viongozi waliochaguliwa ni Said Nassoro (Mwenyekiti), Charles Ndagala (Katibu Mkuu) na Kamwanga Tambwe (mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF).

Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza vyama hivyo unaonesha jinsi wapiga kura walivyo na imani kubwa kwao, na TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya FRAT na SPUTANZA.

Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba zao pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yao.

Pia tunatoa pongezi kwa kamati za uchaguzi za FRAT na SPUTANZA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi umeendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.






TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top