HOFU ya vikundi vya kigaidi vya Al-Shabaab na Al-Qaeda kuwapo
nchini imeanza kujidhihirisha baada ya Jeshi la Polisi mkoani Mtwara
kuwakamata vijana 11 wakichukua mafunzo ya kigaidi mlimani wakiwa na CD
zinazoonesha mauaji mbalimbali ya vikundi hivyo.
Tukio hilo linakuja zikiwa ni siku chache tangu Rais Jakaya Kikwete
kuviagiza vyombo vyote vya dola kuchukua tahadhari ya kuimarisha ulinzi
maeneo yote nchini kufuatia shambulizi la kigaidi lililotokea nchi
jirani ya Kenya na kuua watu zaidi ya 67 na wengine 175 kujeruhiwa.
Magaidi ambao hadi sasa wanajitambulisha kuwa wafuasi wa kundi la
Al-Shabaab la nchini Somalia, ndio wamekuwa wakijigamba kutekeleza
shambulizi hilo katika jengo la biashara la Westgate jijini Nairobi kama
shinikizo la kuitaka Kenya iondoe jeshi lake nchini Somalia.
Vijana hao wanaodaiwa kujihusisha na mafunzo ya ugaidi walikamatwa
wilayani Nanyumbu, mkoani Mtwara, katika Mlima wa Mkoliongo wakiwa na
vifaa mbalimbali zikiwamo CD 25 za mafunzo hayo.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi wa
mkoa huo, Zelothe Stephen, alisema kuwa vijana hao walikamatwa wakiwa na
CD zilizoonesha mauaji ya Osama Bin Laden, Idd Amin Dadaa wa Uganda na
mafunzo ya Al-Shabaab.
Itakumbukwa kuwa Osama ndiye muasisi na kiongozi wa kundi la kigaidi
la Al-Qaeda linalodaiwa kutekeleza mashambulizi kadhaa duniani, likiwamo
lile la balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya mwaka 1998.
Kiongozi huyo alisakwa kwa udi na uvumba na Marekani hadi alipouawa
mwaka juzi akiwa mafichoni nchini Pakistan, lakini vitendo vya kigaidi
bado vimeshika kasi.
Kamanda Stephen alitaja CD nyingine walizokutwa nazo vijana hao kuwa
ni ‘Zinduka Zanzibar’, zinazoonesha namna ya kuua, kuandaa majeshi na
nyinginezo zinazohusisha mafunzo ya kigaidi ya Al- Shabaab.
Pia alitaja vitu vingine kuwa ni ‘solar power’, ‘DVD play’, visu,
mapanga, betri, jiko la mkaa, baiskeli tatu, mfuko wa mbaazi, jiko la
mafuta na nembo yenye nanga ya meli.
“Ni mapema mno kuwaelezea kwa undani, ila mafunzo yao yanaendana na
Al-Shabaab na tutafanya uchunguzi kubaini mambo mbalimbali ikiwamo nani
yuko nyuma yao,” alisema.
Stephen alieleza kuwa vijana hao wanakadiriwa kuwa na umri kati ya
miaka 18-39, ambapo kiongozi wa kundi lao alifahamika kwa jina la
Mohamed Makai.
Alisema kuwa vijana hao wamefikishwa mahakamani na kujibu tuhuma za
kukutwa na vitu hivyo na kujifunza mafunzo hayo kinyume cha sheria.
Pia alisema kuwa upelelezi wa kina unaendelea kwa kushirikiana na
makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam pamoja na mikoa mingine.
Kamanda huyo alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa
mbalimbali zinazohusisha masuala ya uvunjifu wa amani, kwani usalama ni
wa Watanzania wote.
0 comments:
Post a Comment