Mauaji ya kihistoria yaliyotikisa Jiji la Nairobi, Kenya, yamechagiza mshtuko wa aina yake nchini Tanzania na sasa hofu imetanda ndani ya Dar es Salaam hususan kwenye majengo ambayo huchukua watu wengi kila siku.
 
Moshi mkubwa ukifuka kutoka katika jengo la Westgate, jijini Nairobi jana.
Kitendo cha Kikundi cha Al-Shabab kukiri kuhusika na utekaji wa Jengo la Westgate, Nairobi, Jumamosi iliyopita na kufanya mauaji ya kutisha, ukijumlisha na sababu walizotoa za uharamia huo, kwa pamoja inafanya Dar isiwe salama.

Al-Shabab, imetoa sababu ya kuivamia Kenya kwamba nchi hiyo imekuwa ikiingilia mipango yao ya ugaidi nchini Somalia.

Taarifa ya kikundi hicho chenye makao yake Somalia, imeeleza: “Kenya waondoe majeshi yao Somalia, wasipofanya hivyo, tutaendelea kufanya utekaji zaidi.”
Wananchi walionusurika katika shambuli hilo.
Sababu za kuvamiwa
Mosi; Mwaka jana, Kikundi cha Al-Shabab kiliitishia Tanzania kusitisha shughuli za burudani, vinginevyo kitateketeza kumbi zote za starehe nchini, hususan Dar.

Agizo hilo la Al-Shabab lilipuuzwa, hivyo kuiweka hai hofu kwamba kwa uthubutu waliouonesha Nairobi, wanaweza kuuendeleza Dar.

Pili; Tanzania inapita katika njia za Kenya katika ushiriki wa kurejesha amani kwenye mataifa yenye machafuko.

Tanzania inashiriki kurejesha amani Darfur, Sudan, DRC na kadhalika, hivyo imekuwa ikitazamwa kwa jicho baya na vikundi vya uasi katika nchi hizo.

Kikundi cha Janjaweed nchini Sudan, kinaweza kuthubutu kuingia nchini na kufanya utekaji, kutokana na hasira zake dhidi ya Tanzania kwa vile askari wa JWTZ, ndiyo kikwazo kwao kila wanapopanga uharamia wao.

Chuki ya waasi wa kikundi cha M23, DRC, dhidi ya Tanzania ipo wazi, kimekuwa kikielekeza vitisho vya dhahiri kwa serikali mpaka kuilazimisha itoe matamko kujibu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, mara kwa mara hutoa matamko kujibu maneno ya M23.

Bungeni wakati wa vikao vya bajeti mwaka huu, Membe alitumia muda mwingi kujibu waraka wa M23 ambao waliutuma nchini, wakieleza kuwa ni ujumbe kutoka kwa Mungu, wakiionya Tanzania kutopeleka majeshi DRC, vinginevyo itakiona cha moto.

Hata hivyo, baada ya majibu ya Membe, M23 walihamishia mashambulizi yao kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, wakiitishia Tanzania.

Baadhi ya ‘twiti’ za M23, siku moja baada ya Membe kusisitiza bungeni kwamba Tanzania itaenda DRC, mojawapo ilisema: “Membe usiwadanganye watu, mnakuja DRC kuweka petroli kwenye moto, hamji kutafuta amani.”

Twiti nyingine inasomeka: “Hatutishwi na scout (askari chipukizi), Tanzania leteni majeshi yenu halafu mtaona.”

Hatari kubwa zaidi ni kwamba M23, walitishia kuingia nchini na kufanya mashambulizi, wakitamba wana uwezo mkubwa wa kufanya hivyo.

Kutokana na hatari hiyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ‘alitwiti’, akionya kwamba M23 walikuwa ‘wanatwiti’ wakiwa Dar es Salaam, hivyo ni dhahiri kuwa kundi hilo lilikuwa limeshaingia nchini.

Kauli hiyo ya Zitto, ilikuwa inaweka wazi namna taifa letu lilivyo hatarini, kwani maadui wanaweza kuingia nchini na kupanga mashambulizi dhidi yetu bila sisi wenyewe kujua. 

Maeneo hatari
Kwa tathmini ya kile kilichotokea Nairobi, ndani ya Jiji la Dar wananchi wamehofia maeneo yenye watu wengi kwamba yanaweza kutekwa na kusababisha maafa kuliko yale ya Jengo la Westgate.

Pius Matilido, 41, mfabiashara aliyejitambulisha kwamba ni mfuatiliaji mzuri wa habari za kimataifa, alisema kuwa vyombo vya usalama vya Tanzania, viyaangalie majengo ya Mlimani City, Quality Centre, Soko la Kariakoo, Golden Jubilee Tower, Benjamin Mkapa Tower na mengine ambayo huchukua watu wengi kwa siku.

“Hata Millennium Tower na Ubungo Plaza ni ya kuyaangalia sana, magaidi hawashindwi kuingia nchini na kufanya uharamia kama Kenya,” alisema Matilido.

Kwa upande wa Nancy Nehemia wa Mwananyamala, Dar es Salaam, alisema kuwa anaona Tanzania haipo salama, hasa anapoangalia matukio ya ujambazi wanavyoteka magari na kuwapora abiria.

“Kama majambazi tu wanafanya Watanzania wasisafiri kwa amani, inakuwaje M23, Al-Shabab au Janjaweed wakija? Tukio la Nairobi ni shule kwa vyombo vya usalama kudumisha ulinzi wa nchi,” alisema Nancy.

Serikali imejipanga
Serikali kupitia kauli ya msemaji wa Jeshi la Wananchi Tanzania, Eric Komba ni kama imekaa mguu pande mguu sawa kutokana na tishio la ugaidi. 
“Tupo imara, tunadumisha ulinzi kama kawaida, tutawadhibiti magaidi,” alisema Komba.

Ni mauaji ya kihistoria kenya
Tukio la Al-Shabab kuvamia Jengo la Westgate na kuua raia ni la aina yake katika historia ya Kenya.

Al-Shabab ambao idadi yao ni kati ya 10 na 15, walivamia jengo hilo na kuteka raia waliokuwemo ndani kisha kuilazimisha Serikali ya Kenya kusalimu amri na kuondoa majeshi yake nchini Somalia.

Kadiri muda ulivyokuwa unasogea mbele, kikundi hicho kilikuwa kinaua raia kwa mafungu, huku kikitishia kuendelea na mauaji zaidi kama Serikali ya Kenya itaendelea kukaidi.

Kila walipoua raia, walimtupa nje ili kutoa ujumbe kwa serikali kwamba dhamira yao ipo hai katika kuilazimisha Kenya kuondoa majeshi yake Somalia.

Mpaka Jumapili jioni, jumla ya watu 59 walikuwa wamesharipotiwa kuuawa katika tukio hilo, huku wengine 175 wakiwa wamejeruhiwa.

“Kipaumbele chetu ni kuokoa watu wengi kadiri tuwezavyo,” Joseph Lenku ambaye ni Katibu wa Baraza la Mawaziri, akihusika na Mambo ya Ndani na Uratibu wa Serikali, aliviambia vyombo vya habari.

“Tumeshaokoa takriban watu 1000, tunaendelea na jitihada zaidi,” alisema Lenku.

Wakenya waungana
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, mpinzani wake mkuu, Raila Odinga, kwa pamoja walitoa matamko yanayofanana, yakitaka utulivu miongoni mwa raia.

“Kinachotia moyo ni kuona viongozi wote wa Kenya tumesimama pamoja katika kipindi hiki kigumu,” alisema Kenyatta katika mkutano na waandishi wa habari ambao Odinga pia alihudhuria.

Odinga alisema kuwa tukio la Westgate kutekwa siyo vita dhidi ya Waislamu, isipokuwa ni mapambano dhidi ya ugaidi, kauli ambayo Kenyatta aliiunga mkono.
 GPL

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top