Polisi wa Kenya akimuokoa mtoto, baada ya kundi la watu waliokuwa na
silaha kuvamia duka kubwa la bidhaa katika jengo la Wastgate, jijini
Nairobi, jana na kuwaua zaidi ya 20 na wengine kuwajeruhi.
Zaidi ya watu 39 wameuawa na wengine 150
kujeruhiwa baada ya watu wenye silaha kuliteka jengo lenye maduka la
Westgate, jijini Nairobi, Kenya.
Tukio hilo lilitokea jana mchana ambapo watu
waliokuwa wakizungumza lugha ya kigeni, inayodhaniwa kati ya Kiarabu au
Kisomali, kuvamia jengo la ghorofa na kushambulia watu kwa risasi.
“Hawakuwa wakizungumza Kiswahili. Walikuwa
wakizungumza kwa lugha kama vile Kiarabu au Kisomali, lakini sina hakika
sifahamu lugha hizo,” alisema mmoja wa mashuhuda aliyefanikiwa kutoka
ndani ya jengo hilo na kujitambulisha kwa jina moja la Jay.
Shuhuda mwingine aliyejitambulisha ni mfanyakazi
wa Ubalozi wa Uholanzi jijini Nairobi, Rob Vandijk, alisema tukio hilo
lilitokea wakati akipata chakula cha mchana ndani ya njengo hilo.
Alisema watu hao waliingia ndani ya jengo la maduka hayo na kuanza kushambulia watu kwa risasi.
Katibu Mkuu wa Chama cha Msalaba Mwekundu, Abbas Guled alisema: “Ninachoweza kusema tuna takriban maiti 20. Majeruhi ni wengi.”
Katika hotuba iliyorushwa moja kwa moja baadaye,
Rais Uhuru Kenyatta alithibitisha kuwa zaidi ya watu 39 walikufa katika
shambulizi hilo la kinyama, na wengine 150 kujeruhiwa.
"Vyombo vya usalama vinafanya kila jitihada
kuthibiti eneo hili na kuwakamata waliohusika," alisema Mr Kenyatta,
akiongeza kuwa naye pia amepoteza wanafamilia katika tukio hilo.
Polisi Waingia
Taarifa zingine zilisema kuwa polisi waliwasili eneo la tukio dakika 30 baada ya watu hao kuvamia jengo hilo.
Kamanda wa Polisi wa Kenya, Inspekta Jenerali
David Kimaiyo alisema kwamba polisi walifika katika jengo hilo baada ya
kupata taarifa, ambapo nao walianza kujibizana kwa risasi na magaidi hao
waliokuwa hapo ndani.
Alisema
watu hao wanaosadikiwa ni magaidi walikuwa
wakijaribu kuiba pesa katika jengo hilo, kabla ya polisi hawajatokea na
kuanza kurushiana risasi.Helikopta za polisi zilionekana zikilizunguka
jengo hilo kwa juu kuhakikisha hakuna mhalifu yeyote ambaye anaweza
kutoroka.
Mashuhuda walisema kwamba walikuwa wakipata
chakula cha mchana jirani na jengo hilo, ghafla wakashuhudia milio ya
risasi kutoka katika eneo hilo.
Polisi walifanikiwa kuingia katika jengo hilo
baada ya kukaa kwa muda mrefu kuangalia namna ya kuingia kwa sababu
hawakujua watu hao walikuwa wamejificha eneo gani.
Baada ya polisi kuingia katika jengo hilo watu
waliokuwa ndani walipata fursa ya kutolewa, huku polisi wengine
wakiendelea kuwatafuta wahalifu hao.
Al-Shabab Yanena
Wakati shambulizi likiendelea jana jioni,
wanamgambo wa kikundi cha Kiislamu cha Al-Shabab waliviambia vyombo vya
habari kupitia Twitter kuwa wamehusika na tukio hilo.
“Tulishaionya serikali ya Kenya kuwa dhahama
itaikumba kama isipoondoa vikosi vyake kutoka Somalia,” Al-Shabab
waliandika kupitia akaunti yao ya Twitter inayoitwa @HSM_Press.
Wanamgambo hao waliongeza kuwa wamefanikiwa kuua
watu wengi kuliko idadi inayotajwa na serikali ya Kenya, huku wakibeza
jitihada za uokoaji.
Kutokana na malalamiko kutoka kwa waathirika wa tukio na vyombo mbalimbali vya usalama, FastCompany inaripoti kuwa Twitter ililazimika kuifunga akaunti hiyo jana usiku.
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment