Wadadisi wanasema wapiga kura wengi watajitokeza kupiga kura
Raia wa Rwanda milioni sita leo wanapiga kura kuwachagua wabunge katika mfumo wa vyama vingi vya kisiasa. Rwanda inasifika sana kwa kuwa na wanamama wengi kwenye nyadhifa za uongozi wa kitaifa.
Uchaguzi huu usio na upinzani mkubwa ni kama kupiga muhuri tu uongozi wa chama cha RPF chake Rais Paul Kagame ambacho kimekuwa uongozini tangu kumalizika kwa mauaji ya Kimbari mwaka 1994.

Inasemekana kuwa wapiga kura wengi huenda wakajitokeza licha ya kuwa kampeini za uchaguzi hazikufanywa kwa kishindo pamoja na kukosekana kwa upinzani mkubwa kwa chama cha RPF.

Shughuli ya kupiga kura ilionekana kuwa tulivu , foleni zikiwa zimepangwa vyema huku vipaza sauti vikisikika kuwaambia wananchi kutosahahu kadi zao za kujitambulisha wakati wakienda kupiga kura.

Mwishoni mwa wiki, tukio pekee la kutishia usalama lililoripotiwa ni shambulizi la maguruneti, katika soko moja mjini Kigali, mji ambao unasifika kwa usalama wake barani Afrikia.

Tangu kutokea kwa shambulizi hilo, hakuna mtu yeyote aliyekiri kuhusika nalo, lakini serikali ililaumu waasi wenye uhusiano na kundi la waasi la (FDLR), ambao huendesha harakati zao maeneo ya mpakani na Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Kundi hilo linajumuisha waasi wa zamani wa kihutu wanaolaumiwa kwa mauaji ya Kimbari ya mwaka 1994 ingawa waliondoshwa na waliokuwa wanachama wa waliokuwa wanajeshi waasi wa RPF.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top