Padri wa Parokia ya Mpendae ya Kanisa Katoliki Zanzibar, Anselmo
Mwang’amba amesema kuwa alimwona mtu aliyemwagia tindikali na
kumsababishia majeraha na kueleza kuwa anashangaa kuona polisi
hawajamkamata hadi sasa.
Akizungumza jana katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, kwenye Wodi namba 16, Kibasila alipolazwa, Padri Mwang’amba
alisema baada ya kumwagiwa tindikali, alimwona mtu huyo akikimbia
kuelekea katika nyumba moja jirani.
“Kwa kuwa mimi nilikuwa na taharuki na maumivu,
sikuweza kuendelea kumfuatilia, ila dereva aliyenikimbilia kunipa msaada
aliniambia kwamba alimwona mhusika akikatiza kwenye uchochoro hadi
alipoingia kujificha kwenye nyumba iliyopo jirani na eneo hilo,”
alisema.
Alisema majeraha aliyoyapata wakati akitokea
katika duka la huduma za mawasiliano ya mtandao la Shine Shine saa 10.15
jioni, ambayo yanamsababishia maumivu makali, hayawezi kumfanya
aikimbie Zanzibar, kwa kuwa hata Yesu Kristo wakati alipokuwa katika
kazi za utumishi duniani alipata mateso makali kuliko yake.
“Nilisomea upadri nikiwa Zanzibar kuanzia mwaka
1976 hadi mwaka 1981 nilipopata upadrisho kamili. Niko huko kwa kazi ya
Mungu wala si mwanadamu, kwa hiyo nikitoka hapa narejea hukohuko,
siogopi, ingawa miaka hiyo nilipokuwa naanza kazi hii hakukuwa na mambo
kama haya,” alisema.
Aliwataka Wakristo wanaoishi Zanzibar kuendelea
kuwa na umoja na upendo pamoja na kuwa makini kwa usalama wao licha ya
matukio magumu yanayowakuta ikiwamo vitisho na kuchomwa moto kwa
makanisa.
Pia aliunga mkono shinikizo la kutimuliwa kazi kwa
Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Mussa Ali Mussa kutokana na kushindwa
kuwakamata watu wanaomwagia watu tindikali.
“Huyu bwana alishindwa hata kunijulia hali wakati
nikiwa hospitali huko Zanzibar, tofauti na nilipokuja Bara ambako
Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Kamanda wa Polisi wa Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova walifika kunijulia hali na
kuzungumza nami hospitali.
“Kwa hali hii, naona kwamba tukio langu ni la
kupangwa na litazungumzwa sana lakini baada ya muda halitashughulikiwa.
Atajeruhiwa mwingine tena lakini hatua za dhati za kudhibiti ukatili huu
usiendelee hazijachukuliwa. Mimi ni padri wa tatu kufanyiwa ukatili,”
alisema.
Mapadri wengine ni Ambros Mkenda aliyepigwa risasi na kujeruhiwa wakati Padri Evarist Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi.
Al-Shabaab wanaswa Zenji
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Zanzibar limewakamata watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa kikundi cha kigaidi cha Al-Shabaab cha Somalia.
Kamishna Mussa alisema watu hao wamekamatwa baada ya operesheni
ya kuwasaka watu wanaofanya vitendo vya hujuma kwa kutumia tindikali na
kudhibiti matumizi holela ya uingizaji na usambazaji wa kimiminika hicho
visiwani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar
jana, Kamishna Mussa alisema watu 15 wamekamatwa na wanaendelea kuhojiwa
na kwamba baadhi yao wanahusishwa na tukio la kumwagiwa tindikali,
Padri Mwang’amba.
“Wapo waliokamatwa na tindikali iliyozimuliwa na wapo wenye tindikali isiyozimuliwa,” alisema Kamishna Mussa.
Alisema watu watakaobainika kuingiza tindikali huko Zanzibar wakiwa hawana vibali halali watachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema katika operesheni hiyo iliyoanza Septemba
14, mwaka huu kwa kushirikiana na taasisi nyingine ikiwamo Ofisi ya
Mkemia Mkuu wa Serikali, imewalenga waagizaji wa tindikali, wasambazaji,
wauzaji na watumiaji holela.
Alisema hadi jana, karibu lita 29 za tindikali
zimekamatwa zikiwa zimehifadhiwa katika madumu ya lita moja katika
maeneo tofauti na kusema tindikali imekutwa katika maeneo mengi ya
Zanzibar.
Hata hivyo, hakusema wafuasi hao wanaodaiwa kuwa
ni wa Al-Shabaab walikamatwa katika mazingira na eneo gani. Pia hakutaja
majina yao lakini alisema wamekamatwa wakiwa katika mipango ya kwenda
kupigana Somalia.
Kuhusu madai ya matukio ya tindikali kushamiri
visiwani Zanzibar bila ya watuhumiwa kukamatwa na kufikishwa mahakamani,
Kamishna huyo alisema kazi ya polisi ni kukamata na kuchunguza na
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Zanzibar kazi yake ni kufungua kesi na
kushtaki kwa niaba ya Jamhuri.
Pia alisema jalada la kumwagiwa tindikali,
aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar, Rashid Ali Juma
limefungwa baada ya kukosekana kwa ushahidi wa watu waliohusika na
shambulio hilo.
Akizungumzia kesi ya Katibu wa Mufti, Sheikh
Fadhil Soraga alisema uchunguzi wake umekamilika muda mrefu na jalada
lake lipo kwa DPP huku watuhumiwa wa kesi hiyo wakiwa nje kwa dhamana.
“Watu watatu wanashikiliwa kwa tukio la kuwamwagia
tindikali raia wawili wa Uingereza, Kate Gee na Kristie Trup na
uchunguzi wake uko mbioni kukamilika.
“Napenda tuelewe kuwa upelelezi ni kitu kimoja na
kuzuia uhalifu usitokee ni kitu cha pili. Kazi yetu ni kuchunguza na
kufikisha watu mahakamani ni kazi ya Mkurugenzi wa Mashtaka. Ila wajibu
wa kuzuia uhalifu usitokee ni kazi ya taasisi za Serikali, polisi na
wananchi,” alisema Mussa ambaye aliambatana na Naibu Mkurugenzi wa
Makosa ya Jinai Zanzibar, Yusuf Ilembo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mjini Magharibi, Mkadam Khamsi Mkadam.
Kutwa nzima ya jana, jitihada za kumpata DPP Ibrahim Mzee Ibrahim zilikwama. Hakuwa tayari kupokea simu wala kujibu ujumbe mfupi wa maandishi (SMS), kila alipoandikiwa maswali.
MwananchiKutwa nzima ya jana, jitihada za kumpata DPP Ibrahim Mzee Ibrahim zilikwama. Hakuwa tayari kupokea simu wala kujibu ujumbe mfupi wa maandishi (SMS), kila alipoandikiwa maswali.
0 comments:
Post a Comment