Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akihutubia wananchi wa wilaya ya Bunda waliofika kusikiliza mkutano huo.

Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Ndugu Abdulrahman Kinana anaendelea na ziara yake na sasa ameingia katika Mkoa wa Mara na tayari ametembelea shughuli za utekelezaji wa ilani ya uchaguzi katika wilaya ya Bunda.
 
Katika ziara hiyo Katibu Mkuu alianza kwa kupokea taarifa ya hali ya kisiasa wilayani hapo na kisha kutembelea mradi wa maji ambao umekuwa ukilalamikiwa muda mrefu kuwa unachukua muda kukamilika, katika mradi huo amekuta hatua ya kwanza kuwekwa kwa bomba kubwa umeanza ,pia alipata nafasi ya kutembelea jimbo la Mwibara ambapo alishiriki katika ujenzi  wa madarasa ya chuo cha ufundi stadi Namibu na kutembelea shule ya Sekondari Mwibara katika kata ya Kibara pamoja na kutembelea kiwanda cha Mara Coooperative 1984.

Ziara hiyo wilayani Bunda ilihitimishwa kwa mkutano wa hadhara ambao ulijaza umati si wa kawaida.
 
Katika Mkutano huo Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye alisema  tangia Kinana amechaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM Mabalozi karibia nusu wamekuwa wakifika ofisini kumpa pongezi bila kificho na kuonyesha kufurahishwa kwao kwa uteuzi huo “Nawashangaa watani zetu kukomalia suala la balozi wa China wakati huu wakati ambao tumefanikiwa kupata ufumbuzi  wa matatizo ya wakulima wa Pamba”,
 
Aliendelea kusema mabalozi wamekuwa wakishiriki kwenye shughuli mbalimbali za CCM ikiwemo kuwa wageni waalikwa kwenye mikutano mikuu ya CCM na hiyo yote haijawahi leta maneno, Akasema msajiri wa vyama ameshauriwa vibaya kuhusu hili.
 
Katibu Mkuu wa CCM Taifa Ndugu Abdulrahman Kinana ameendelea kusisitiza juu ya madai ya walimu nchi nzima kulipwa kwa wakati bila kuwa ya malimbikizo,alisema tatizo hili la muda mrefu na Rais alishatolea maagizo  lakini halitekelezwi akasema kama Katibu Mkuu wa Chama anatoa miezi sita walimu wawe wamelipwa madai yao na kama halitofanyika yeye kama Katibu Mkuu atalipeleka kwa wabunge wa CCM kasha wapitishe azimio Bungeni la kufukuzwa kazi wahusika.
 
Katibu Mkuu alisema “ watu wamekaa mjini wanalipwa vizuri, magari mazuri na suti wamevaa lakini hawajali wenzao wanajilipa posho kila kikao”.
 
Katibu Mkuu alisisitiza kuwa anamuomba Waziri Mkuu azuie vikao wakati wa kazi na vikao vyote vifanyike baada ya muda wa kawaida wa kazi kumalizika.
 
Alisisitiza yeye ni Katibu Mkuu wa CCM anayefanya kazi kwa vitendo na amedhamiria kuhakikisha chama kinafanya kazi nzuri ya kuiongoza serikali.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top