Dk. Shukuru Kawambwa
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk. Shukuru Kawambwa amezidi kuandamwa huku mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), akisema atapambana naye aweze kung’oka katika wizara hiyo. 
 
Mbunge huyo ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana kumtaka waziri huyo ajiuzulu kwa kushindwa kulipa madeni ya walimu.

Lugola alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kibara wilayani hapa mbele ya Kinana.

Mbunge huyo alisema kama Kawambwa angekuwapo angemwambia Kinana aondoke naye ili akalime kwao.

Lugola ni miongoni mwa wabunge wa CCM wanaojulikana kwa msimamo wao wa kuipinga na kuikosoa Serikali ndani ya Bunge ikiwamo kusaini saini 70 za kung’oa waziri Mkuu kwa kushindwa kuwawajibisha mawaziri wake.

Alisema Dk. Kawambwa ameshindwa kutatua kero za walimu hali inayowafanya wabunge wengi wa CCM kushindwa kufanya mikutano na walimu katika shule za majimbo yao ya uchaguzi.

“Ndugu Katibu Mkuu endelea na moto wako huo, leo kama ungekuja na Waziri Kawambwa ningemtimua na hata kukwambia ondoka naye hapa akalime kwao Bagamoyo kwa sababu ameshindwa kulipa madeni ya walimu ambayo yamekuwa kero kubwa.

Mbunge huyo pia alitupa kijembe kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akisema kuwa wakati chama hicho kikihangaika na kuruka kwa chopa na kunywa keki na soda, wabunge wa CCM wanakesha katika majimbo yao kuhakikisha wanaharakisha shughuli za maendeleo.
Mtanzania

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top