Licha ya Watanzania wawili, Agnes Gerald (Masogange) na Melisa
Edward kuachiwa huru, wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam waliobainika kushiriki kuwapitisha
wataendelea kuchunguzwa.
Mkurugenzi wa JNIA, Moses Malaki alisema jana kwa
simu kuwa wafanyakazi hao, wataendelea kushtakiwa kwa sababu walikiuka
maadili ya kazi yao.
“Hata kama hao waliowasaidia wameachiwa huru au
walichokibeba hakikuwa dawa za kulevya lakini kwa kuwa wafanyakazi hao
walivunja kanuni za kazi, wataendelea kushtakiwa kisheria,” alisema
Malaki.
Mkurugenzi huyo alisema uongozi wa uwanja huo wa
ndege una ushahidi wa kimazingira wa jinsi wafanyakazi hao
walivyoshiriki kuwasaidia kina Masogange kupitisha mzigo huo na kwa
ushahidi huo, watashtakiwa kwa kukiuka maadili ya kazi zao.
“Sheria za kazi zikisema usiongee na simu kazini,
wewe ukaongea, basi tayari umevunja kanuni. Hao wafanyakazi wameshiriki
kuupitisha mzigo huo na Mahakama ya Afrika Kusini haikuwaachia hao
wasichana huru kwa kuwa hawakuonekana na kosa, walihukumiwa na mmoja wao
amelipa faini ndiyo maana wapo huru. Mmoja wao alipatikana na kosa,”
alisema Malaki.
Malaki alisema uongozi wa uwanja wa ndege utawachukulia hatua wafanyakazi watakaobainika kushiriki kwa namna moja au nyingine.
Mahakama ya Kempton ya Afrika Kusini wiki
iliyopita ilimhukumu Masogange kifungo cha miezi 30 au kulipa faini ya
Randi 15,000 (sawa na Sh2.4 milioni). Alilipa na kuachiwa huru. Melissa
aliachiwa huru baada ya kuonekana hana hatia.
Baada ya Masogange na Melisa kukamatwa, Waziri wa
Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe aliagiza uchunguzi wa kina ufanyike
kwenye uwanja huo ili kujua namna wasichana hao walivyopitisha mzigo
huo.
Uchunguzi wa Mwakyembe kwa msaada wa kamera za
CCTV ulifichua tukio zima la Masogange na Melissa kupitisha mzigo wao
uwanjani hapo na jinsi baadhi ya wafanyakazi wa JNIA walivyoshiriki
kuwasaidia kuupitisha.
Baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo, Agosti 17,
mwaka huu, Dk Mwakyembe alitoa agizo la kufukuzwa kazi kwa wafanyakazi,
Koplo Juliana Thadei, Jackson Manyoni, Yusuph Daniel Issa, Koplo Ernest
na Mohamed Kalugwan.
Hukumu yaishangaza Tume
Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Tanzania imesema
imeshangazwa na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kempton ya Afrika
Kusini dhidi ya Watanzania hao na mazingira ya dawa hizo kubadilika na
kuwa kemikali.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Msemaji wa tume hiyo, Florence Mlay alisema, itatoa tamko rasmi
leo kuhusu hukumu hiyo, huku akisisitiza kwamba inashangazwa ni kwa
namna gani watuhumiwa hao wameachiwa huru kwa kutozwa faini ndogo huku
mzigo walioubeba ukigeuka kemikali badala ya dawa.
“Hatuwezi kuzungumza sana kuhusu hili lakini ni
lazima sisi kama tume tuangalie ni kwa nini ule mzigo awali ulionekana
ni dawa za kulevya aina ya methamphetamine na sasa zimegeuka kuwa ni
kemikali,” alisema Mlay.
Hata hivyo, Msemaji wa Kitengo cha Kusimamia
Makosa ya Jinai wa Afrika Kusini, Kapteni Paul Ramaloko alisema Mahakama
imeamua kuwa watu hao walibeba kemikali na si dawa za kulevya na
wanaheshimu uamuzi huo.
Alisema hata kama watuhumiwa hao wameachiwa huru
kwa faini au hukumu ndogo, jambo muhimu kwao ni kwamba angalau
walipatikana na hatia.
“Kazi yetu kubwa ni uchunguzi wa makosa ya jinai,
tuliwakamata watu hawa uwanja wa ndege kwa kosa la kubeba dawa za
kulevya. Mahakama imeona kuwa si dawa, bali ni kemikali na sisi hatuna
la kufanya zaidi ya hapo,” alisema.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment