Baada ya mjadala mkali Jana bunge la kenya
lilipitisha mswaada wa kuitaka kenya kujiondoa katika mkataba wa Roma
unaounda mahakama ya kimataiafa ya uhalifu wa jinai- ICC.
Hatua hii inakuja wakati Naibu rais William Ruto
akijiandaa kuelekea Katika makao makuu ya mahakama hiyo mjini Heague
Uholanzi kukabiliana na kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu.
Baadhi ya wabunge wa upinzani nchini Kenya waliondoka kwa hasira bungeni wakati mjadala huo ulipokuwa unaendelea.
Wabunge hao waliondoka baada ya kusema kuwa
kamwe hawataungana na upande wa serikali kuunga mkono hoja hii ya
kujiondoa kutoka katika mahakama ya ICC. Ni kutokana na kuwa upinzani una idadi ndogo zaidi ya wabunge bungeni.
Wengi waliounga mkono hoja hiyo walikuwa wabunge
wa muungano tawala wa Jubilee unaoongozwa na vigogo Rais Uhuru Kenyata
na naibu wake William Ruto.
Naibu kiranja wa wabunge wa upinzani bungeni
Jakoyo Midiwo, alisema kuwa wabunge wa upande wa serikali wanaotetea
hoja hii ya kujiondoa Hague watakuja kujuta.
Mjadala huu unatokana na hatua ya Rais Uhuru
Kenyatta na naibu wake William Ruto kukabiliwa na kesi za uhalifu dhidi
ya binadamu katika mahakama hiyo wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi
mkuu mwaka 2007-2008.
Hatua hii ya wabunge pia inakuja ikiwa imesalia
chini ya wiki moja kabla ya kuanza kwa kesi dhidi ya naibu Rais wa
Kenya Williiam Ruto kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2008.
Ruto anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu.
Rais Uhuru Kenyatta pia anatarajiwa kufika katika mahakama hiyo mwezi Novemba kwa kesi dhidi yake.
Wawili hao wanashtakiwa kwa kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi mwishoni mwa mwaka 2007.
Msemaji wa ICC ameambia BBC kuwa kesi hiyo
itaendelea hata ikiwa Kenya itajiondoa kwenye mkataba wa Roma
uliopelekea kuanzishwa kwa mahakama hiyo.
Hii ni hatua ya dharura inayochukua serikali
kujitoa katika Mkataba wa Roma wa mahakama hiyo ulioidhinishwa na Umoja
wa mataifa mnamo tarehe 17 July, mwaka1998.
Kenya inataka kutoa mfano wa kuwa nchi ya kwanza
Afrika kuchukua hatua hiyo licha ya kwamba uamuzi huu hautoathiri kwa
namna yoyote kesi zinazoendelea sasa katika mahakama ya ICC.
Mahakama hiyo ya kimataifa imesema kwamba kesi hizo zitaendelea hata iwapo Kenya itajitoa.
Imesema itaichukua Kenya kiasi ya mwaka mmoja
kabla ya kukubaliwa ombi hilo la kutaka kujiondoa katika mkataba wa Roma
na hilo litaathiri tu kesi zitakazozuka baada ya muda huo.
Haya yanajiri wakati makamu wa rais William Ruto
anatarajiwa kuondoka Kenya kueleka Hague Uholanzi wiki ijayo kukabiliwa
na mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadaamu katika mahakama hiyo ya ICC,
kesi inayoanza tarehe 10 mwezi huu.
Wote wameshtakiwa kwa kuhusika katika ghasia
zilizojiri baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.Kesi dhidi ya rais Uhuru
Kenyatta inatarajiwa kuanza tarehe 12 mwezi Novemba.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment