Rais Jakaya Kikwete
WAZIRI wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe amemtisha Rais
Jakaya Kikwete akisema kuwa endapo hatasaini muswada wa sheria ya
marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013, atakuwa
ameingia kwenye mgogoro na Bunge.
Muswada huo uliopitishwa hivi karibuni na wabunge wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) pamoja na Augustine Mrema wa TLP (Vunjo), unapingwa
vikali na vyama vya upinzani pamoja na makundi mbalimbali ambayo sasa
yanamshinikiza rais asiusaini kuwa sheria.
Makundi hayo ambayo yamepata msukumo wa vyama vitatu vya CHADEMA, CUF
na NCCR-Mageuzi ambavyo wabunge wake walikataa kuujadili muswada huo
wakipinga uchakachuaji uliofanyika wa kuongeza vifungu na
kutoishirikisha Zanzibar, tayari yametishia kwenda kortini ikiwa
watapuuzwa.
Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Chikawe
alisema kuwa ni vyema makundi mbalimbali yakaacha kumlaghai Rais
Kikwete ili asiusaini muswada huo.
Kwa mujibu wa Chikawe, iwapo Rais Kikwete ataliafiki suala hilo la
wapinzani na makundi mengine, na kuacha kutia saini muswada huo,
atakuwa ametengeneza mgogoro na mhimili wa Bunge kutokana na chombo
hicho kukamilisha kazi yake.
Alisema kuwa taratibu zote zilifuatwa kuhusiana na kupitishwa kwa
muswada huo, na kudai kushangazwa na baadhi ya makundi yanayopiga
kelele.
“Hao wanaolalamikia juu ya jambo hilo hawatendi haki kwani sheria
zote zilifuatwa na hayo mapendekezo wanayotoa ya kutaka Rais Kikwete
asitie saini sio sahihi hata kidogo, huko ni kutaka ‘kumblack mail’ na
kumsababishia mgogoro na Bunge,” alisema.
Waziri Chikawe alisema kuwa ameshangazwa na baadhi ya matamshi
yanayotolewa juu ya kuwepo kwa fujo au kumwagika damu na kusema jambo
hilo haliwezi kufanikiwa kama halijapangwa.
“Fujo zinapangwa, hivyo wale wanaotaka kumwaga damu ni vyema
wakajitaja na kusema kuwa ‘sisi tutamwaga damu’ kwa kuwa naamini damu
haiwezi kumwagika yenyewe,” alisema.
Waziri huyo alisema kuwa ni vyema wale wanaotaka kuzunguka kwa
wananchi na kufanya udanganyifu juu ya suala hilo, wangekubali
kuwasilisha hoja hizo ndani ya Bunge na si mahali kwingine.
Kuhusu Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kutopeleka muswada huo kwa
wananchi wa Zanzibar, Chikawe alisema kuwa utaratibu uliotumika ni
hisani tu, kwani hakuna sheria inayotaka muswada wa aina yoyote
kupelekwa kwa Watanzania.
“Utaratibu wa kupitisha muswada huo sio huo tu, bali zipo njia nyingi
ambapo anaweza kuandika anayohitaji na kuwasilisha kwa kamati ya Bunge
na wapo waliofanya hivyo,” alisema.
Chikawe aliongeza kuwa inawezekana Kamati ya Katiba na Sheria ikawa
na sababu za kushindwa kuwafikia wananchi wote, lakini kwa upande wao
walipokea maoni ya Serikali ya Zanzibar yaliyotolewa Mei 27, mwaka huu.
Alisema kuwa moja ya pendekezo lililotolewa na Serikali ya Zanzibar
ni juu ya kuongezwa kwa siku 20 kati ya 70 zinazotakiwa kutumiwa na
Bunge Maalumu la Katiba.
Chikawe alisema kuwa ni vyema yale yanayoenda kutolewa kwenye mkutano
wa wapinzani kesho katika viwanja vya Jangwani, yangepelekwa bungeni
kwa kuwa hata wakitoa katika viwanja hivyo haitasaidia.
0 comments:
Post a Comment