Waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron
Uingereza huenda ikaanzisha mashambulio dhidi ya utawala wa Syria, bila kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Hayo ni kwa mujibu wa ushauri wa wataalamu wake wa masuala ya kisheria.

Ushauri huo unasema, mashambulio hayo yatahitajika ikiwa yatatekelezwa ili kuzuia raia kuuawa, hata ikiwa wanachama wa kudumu wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Urussi na Uchina zikitumia kura zao za turufu kupinga mikakati za kijeshi dhidi ya utawala wa Syria.

Maafisa wa ujasusi nchini Uingereza wamemueleza Waziri Mkuu, David Cameron kuwa, kuna uwezekano mkubwa kuwa serikali ya Syria ilihusika na shambulio la kemikali wiki iliyopita mjini Damascus.

Wabunge wa Uingereza wanatarajiwa kujadili suala hilo katika kikao chao cha leo jioni.

Serikali ya Syria imekana madai ya kutumia silaha za kemikali katika shambulio mjini Damascus tarehe 21 mwezi huu, ambapo mamia ya watu waliuawa.

Lakini Bwana Cameron anaamini kuwa kuna ushahidi wa kutosha kutoka wa maafisa wake wa ujasusi na pia kutoka kwa wanainchi kuhusu ukatili unaofanywa na utawala wa sasa wa Syria.

Ofisi ya Waziri mkuu wa Uingereza, imechapisha ripoti hiyo, kuambatana na ushauri wa mkuu wake wa sheria Dominic Grieve, inayotoa idhini ya mashambulio ya kijeshi ili kuzuia utumiaji wa silaha za kemikali siku zijazo, kuambatana na sheria za kimataifa.

Umoja wa Mataifa

Ban Ki-Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amesema atapokea ripoti kutoka kwa wachunguzi wake wa silaha, wanaochunguza ikiwa silaha za kemikali zilitumika nchini Syria.

Mamia ya watu wanaripotiwa kuuawa kwenye shambulio hilo, lililofanyika karibu na mji mkuu wa Damascus wiki iliyopita.

Rais wa Marekani Barack Obama, amesema hajaamua kuhusu mpango wa kuishambulia Syria kijeshi.

Mataifa mengine pia yanajadili hatua watakayo chukua na Uingereza imekuwa ikishinikiza baraza la Usalama la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha azimio litakalihakisha raia wamelindwa nchini Syria.

Rais wa Syria Bashar al-Assad amesema taifa lake litajilinda kutokana na shambulio lolote kutoka kwa mataifa ya kigeni.

Syria kujilinda asema Assad

Awali Kiongozi wa chama cha Upinzani cha Labour, nchini Uingereza, Ed Miliband, amesema bunge la nchi hiyo halipaswi kuamua ikiwa itaidhinisha mzozo wa Syria kutatuliwa Kijeshi.

Milliband ameyasema hayo muda mfupi kabla ya bunge la Uingereza kupiga kura ikiwa Uingereza itaishambulia Syria, kufuatia madai ya kutumia silaha za kemikali mjini Damascus.

Waandishi wa habari wanasems serikali ya Uingereza inahofia huenda ikapoteza kura hiyo na hivyo kukosa idhini ya kuingilia mzozo huo wa Syria.

Milliband amesema wamejifunza mengi kutokana na maamuzi yaliyochukuliwa miaka ya zamani kama ule wa kuivamia Iraq.

Amesema jamii ya kimataifa inapaswa kuipa jopo maalum na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa nafasi ya kufanya kazi yao.

Serikali ya Uingereza imesema ina habari za kijasusi kuhusu Syria na itachapisha ripoti hiyo na ushauri wa kisheria kabla ya mjadala huo 
BBCSwahili
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top