Mkuu wa Majeshi ya ulinzi,Jenerali Davis Mwamnyange  
Mpiganaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, JWTZ Khatibu Mshindo aliuawa kwa kupigwa bomu juzi na waasi wa M23 kwenye Mji wa Goma ulioko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya kuzuka mapigano makali.
 
Wakati Mshindo ambaye alikuwa miongoni mwa askari wa Tanzania wanaounda Jeshi la Umoja wa Mataifa akifikwa na mauti, wapiganaji wengine 10 walijeruhiwa.
Askari wa Tanzania na wale wa Afrika Kusini wako DRC kwa kazi ya kulinda amani ambapo Malawi bado haijapeleka majeshi yake.
Meja Mshindo alikuwemo katika kikosi cha vifaru na alikuwa kwenye Kambi ya 83KJ iliyoko Kiluvya Dar es Salaam.
Kuuawa kwa askari huyo kumekuja ikiwa ni siku 47 tangu kuuawa kwa askari saba wa Tanzania waliokuwa wakilinda amani kwenye Mji wa Darfur Sudan na Kikundi cha Janjaweed.
Msemaji wa JWTZ, Meja Erick Komba alikiri kutokea kifo hicho na kusema: “Jana (juzi) Agosti 28, Wanajeshi wetu wakiwa katika eneo lao la ulinzi waliangukiwa na bomu katika eneo hilo na kusababisha majeruhi.
“Wakati wanapelekwa hospitali kwa matibabu, kwa bahati mbaya mwanajeshi wetu mmoja, Meja Khatibu Mshindo alifariki dunia. Majeruhi wengine wanaendelea na matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.”
Habari zaidi kutoka Congo zinaeleza kuwa mwili wa marehemu Meja Mshindo ulisafirishwa jana kupelekwa Entebbe, Uganda ambako ungefanyiwa matayarisho ya mwisho na tayari kwa kuletwa nyumbani.
Katika hatua nyingine, Askari wawili wa Umoja wa Mataifa, mmoja akiwa Mtanzania na mwingine raia wa Afrika Kusini walijeruhiwa kwa bomu eneo la Munigi huko Congo.
Bomu hilo lilirushwa na waasi wa M23 kuelekezwa kwa askari wa Umoja wa Mataifa waliokuwa wakikagua maeneo mbalimbali karibu na Mji wa Goma.
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon amelaani mashambulizi na mauaji hayo ya askari huyo wa Tanzania na kusema: “Ninatoa pole kwa Watanzania na familia ya mpiganaji huyu na ninalaani kwa nguvu zote mauaji haya na majeruhi kwa walinzi wa amani.”
Msemaji wa UN, alisema Majeshi ya UN kwa kushirikiana na yale ya Serikali, yalianzisha mapigano makali dhidi ya waasi wa M23 kwenye eneo la Kibati Kaskazini mwa Goma, kwenye Mji wa Kivu ya Kaskazini.

 Majeshi ya UN na Fardc yalitumia helikopta, vifaru na askari wa miguu kutekeleza mashambulizi hayo yaliyojibiwa na waasi. Kwa mujibu wa msemaji huyo, mapigano bado yanaendelea.
mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top