Oprah Winfrey
Mwanamke maarufu zaidi duniani, Oprah Winfrey, amekumbana ana kwa ana na kile anachokiita kitendo cha Ubaguzi wa rangi nchini Switzerland baada ya muuza duka mmoja kukataa kumuuzia mkoba wa kike wa mkononi na kumwambia kuwa hangeweza gharama yake.
Oprah ambaye ametajwa katika vitabu vya Forbes
kama mwanamke mwenye ushawishi mkubwa wa kisiasa duniani na mmoja wa
watu tajiri zaidi amedai kuwa msichana aliyekuwa akiuza hapo dukani
alimdharau kutokana na rangi yake.
Uswis imejikuta katika kizungumkuti na wanaharakati wa haki za binadamu.
Wiki iliyopita nchi hiyo ilitangaza sheria
katika baadhi ya mabaraza yake ya miji kuwa wahamiaji wa nje
hawataruhusiwa kutangamana na raia wenyeji hasa katika maeneo ya umma
kama vile mabwawa ya kuogelea, uwanja wa michezo na hata kanisani.
Sasa madai haya ya Oprah yanatoa taswira mbaya zaidi ya jinsi hali ilivyo nchini humo kuhusu ubaguzi wa rangi.
Wanaharakati wa haki za binadamu wamesema kuwa
hii ni ishara ya kuwa na ubaguzi ule uliowahi kutokea kwa muda mrefu
huko Afrika Kusini.
Oprah amesema kuwa aliondoka dukani hapo
taratibu bila kufanya vurugu lakini amesikitika kuona kuwa bado ubaguzi
wa rangi unaendelea na kuenea.
Mwaka jana pekee Oprah alikuwa na fedha jumla ya
dola za Kimarekani milioni sabini na saba na amesifiwa kuwa
mfanyibiashara tajiri, ambaye pia anamiliki shirika lake binafsi la
utangazaji na anafadhili miradi mingi ya misaada katika pembe mbali
mbali za dunia.
Alipata umaarufu wake kutokana na kipindi chake cha Oprah Winfrey Show kilichooneshwa nchi nyingi.
Hata hivyo mwandishi wa BBC mjini Zurich anasema
kuwa kipindi hicho hakijawahi kupeperushwa katika runinga za
Switzerland na huenda sio wengi wanaofahamu Oprah ni nani huko.
Oprah alikwenda Uswis kuhudhuria harusi ya mwanamuziki Tina Turner.
Chanzo: BBCSwahili
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment