SIKU chache baada ya serikali za Tanzania na Thailand kutiliana
saini mkataba wa kubadilishana wafungwa na kutekeleza sheria ya vifungo,
raia wa Tanzania amebambwa na dawa za kulevya nchini humo.
Mtanzania huyo aliyefahamika kwa jina moja la Kileo, alikamatwa
Jumanne wiki iliyopita katika kisiwa cha Macau akiwa amemeza dawa hizo
aina ya cocaine akielekea China.
Kwa mujibu wa maofisa wa polisi wa Thailand, dawa hizo zinakadiriwa
kufikia kilogram 1.091, zikiwa na thamani ya dola za HongKong 900,000.
Waziri Mkuu wa Thailand, Yingluck Shinawatra, akiwa ziarani nchini
alitiliana saini na serikali kubadilishana wafungwa, jambo ambalo baadhi
ya wadadisi wa mambo walidai ni hatua ya kuwanusuru vigogo waliofungwa
huko kwa makosa ya kujihusisha na biashara hiyo.
Katika mkutano na waandishi wa habari Jumamosi wiki hii kwenye makao
makuu ya polisi, msemaji wa polisi nchini Thailand alisema wanamshikilia
Kileo (37) aliyekamatwa Jumanne majira ya saa 5:30 asubuhi kwenye eneo la kukagua
mizigo katika uwanja wa ndege.
“Polisi walimsimamisha baada ya kumtilia shaka na kumweka katika kamera za X-ray ndipo wakabaini kuna kitu tumboni.
Alisema kuwa baada ya kubaini kuwa ana kitu kisicho cha kawaida
tumboni alichukuliwa na kupelekwa kwenye hospitali ya Conde de Sao
Januario kwa uchunguzi zaidi.
Kwa mujibu wa gazeti la ‘The Macau Post Daily’ la nchini humo
lililochapisha habari hiyo, polisi walisema kuwa mshukiwa huyo
aliwaambia kuwa alichukuliwa ili kusafirisha dawa hizo kutoka mji
mmojawapo ulioko Tanzania mapema mwezi huu.
Taarifa zaidi zilisema kuwa mtuhumiwa huyo awali alipanda ndege kwenda
Ethiopia kisha akaenda Thailand mahali alipomeza dawa hizo na baadaye
akapanda ndege hadi kisiwa cha Macau ili kuelekea Guangzhou mahali
ambapo alitarajiwa kuonana na mchora mpango wa sakata hilo.
Mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani akikabiliwa na makosa ya kusafirisha dawa za kulevya.
Polisi walisema kuwa Kileo aliwaeleza kwamba alilipwa dola za Marekani 7,000 kukubali kumeza na kusafirisha dawa hizo.
Hii ni mara ya pili ndani ya wiki mbili kwa raia wa Tanzania
kushikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumeza na kusafirisha dawa za
kulevya.
Mtuhumiwa mwingine alitokea kusini mashariki mwa Afrika na kisha
kukamatwa na polisi baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Thailand Julai
10 mwaka huu.
Mtuhumiwa huyo pia aliwaeleza polisi hao kuwa alipita akiwa amemeza dawa za kulevya na kuzisafirisha kupitia njia ile ile.
Polisi bado wanachunguza kama watuhumiwa hao walichukuliwa na kundi lilelile linalosafirisha dawa ya kulevya.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment