MADAI ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), Eliezer Feleshi, kuwa Dk. Steven Ulimboka ameficha ushahidi wa kutekwa kwake, yamepingwa vikali na wanasheria wakisema anaficha uovu.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari juzi mbele ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Saidi Mwema, DPP alisema kuwa polisi wameshindwa kuwakamata watekaji na watesaji wa Dk. Ulimboka kutokana na kutopata ushirikiano wake.

Dk. Ulimboka ambaye ni Mweyekiti wa Jumuia ya Madaktari, alitekwa na kuteswa vibaya kisha kutupwa katika msitu wa Mabwepande nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam usiku wa kuamikia Juni 26, 2012.

Wakizungumza na Tanzania Daima kuhusu utetezi wa DPP, wanasheria hao Mabere Marando, Profesa Abdallah Safari na Method Kimomogoro walisema kuwa amedhalilisha taaluma ya sheria.

Marando alisema DPP amejiunga na jeshi la polisi kuficha uovu unaotokea nchini kwa kile alichoeleza kwamba jukumu la polisi ni kupeleleza tukio kabla ya kumfikiria muathirika awe sehemu ya taarifa ya upelelezi huo.

Alisema kwa kauli ya DPP ni wazi kuwa kama Dk. Ulimboka angepoteza maisha katika tukio hilo, basi wapelelezi wasingekuwa na kazi ya kufanya.

“Hii kwangu ni kauli ya ajabu na sijawahi kufikiria mtu kama Feleshi anaweza kuungana na polisi kuficha ukweli. Jukumu lake ni kutoa maelekezo ya vitu vinavyotakiwa kwa ajili ya kesi, siyo naye anaanza kulalamika!” alisema.

Kuhusu polisi, Marando alisema kwa sasa hawafanyi kazi ya kitaalamu zaidi ya kutegemea kumkamata mhalifu na kisha kumtesa ili atoe maelezo wanayoyataka.

Alisema hali hiyo ndiyo imesababisha takriban asilimia sabini ya kesi zilizo mahakamani kuwa na maelezo ya ‘onyo’ badala ya kufanyiwa kazi kitaalam.

Marando aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo mtuhumiwa anapokuwa na mwanasheria mzuri mara nyingi anashinda kesi na serikali kubaki kuaibika na kutoaminika mbele ya wananchi.

Alisisitiza kuwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka, alipaswa kutoa maelekezo ya kiutendaji kwa jeshi la polisi kwa ajili ya kupata ushahidi wa uhakika.

“Watuambie walifanya nini kumtafuta Dk. Ulimboka, si wana wachunguzi? Kwa nini wasiende nyumbani kwake wakapate huo ushahidi wanaoona haukutolewa?” alihoji.

Marando alisema Dk. Ulimboka alishamtaja ofisa wa Ikulu aliyeshiriki katika kumteka, hivyo lilibaki jukumu la polisi kumkamata mtuhumiwa aliyetajwa na kufanya gwaride la utambuzi.

Alisema hali hiyo ya kumtaka Dk. Ulimboka aende katika ofisi za polisi kutoa maelezo mengine huenda ikawa ni mtego mwingine wa kumdhuru baada ya kumtaja mtu wa serikali anayehusika na kadhia hiyo.

Naye Prof. Abdallah Safari alifafanua kuwa kisheria suala la kutafuta ushahidi ni la serikali yenyewe.

Alisema kuwa tayari Dk. Ulimboka alishawaonyesha njia na kwamba serikali ilipaswa kuanzia alipoishia kwa kuwakamata wote waliotajwa ili kupata ushahidi zaidi.

Mwanasheria mwingine kutoka jijini Arusha, Method Kimomogoro, alisema kuwa Dk.Ulimboka alishatoa maelezo yenye kujitosheleza juu ya mhusika aliyemteka.

Alisema DPP Feleshi ni wazi kwa sasa anachagua matukio ya kufanyiwa kazi na kwamba watu wenye mawazo huru wanapopata tatizo ofisi yake haioni haja ya kushughulika nao.

Alitolea mfano mauaji ya mwandishi wa habari Daudi Mwangosi, kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa CHADEMA kata ya Usa River mkoani Arusha na mwanachama mwingine Mbwana Masudi aliyeuawa Igunga mkoani Tabora.

Pia alitaja mauaji ya kijana Ally Nzona wa mkoani Morogoro aliyepigwa risasi na polisi kwenye maandamanao ya CHADEMA kuwa ni uthibitisho tosha wa namna ofisi ya DPP na jeshi la polisi wanavyofanya kazi kwa ubabaishaji.

Kimomogoro alisema jambo la kusikitisha ni kuona watu wenye mawazo huru ya kuikosoa serikali wanavyokamatwa makundi makundi kama wahalifu kwa wakati mmoja.

Alisema inashangaza kuona kundi la askari lililomzunguka Mwangosi kabla ya kuuawa kwake likiwa halijaguswa hadi leo.

Aliongeza kuwa DPP kwa nafasi yake kwa umma alipaswa aonyeshe dhamira kutenda kitaalamu na si kama mwanasiasa jambo alilosema si jema kwa mustakabali wa taifa.

Wakati wanasheria hao wakikosoa kauli ya DPP, jeshi la polisi limeendelea kushikwa na kigugumizi kueleza kama lilishawahi kuwahoji watu waliotajwa na Dk.Ulimboka.

Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso, alipoulizwa jana, alitaka aandikiwe maelezo katika karatasi na yafikishwe ofisini kwake.

“Kwa sasa nashughulikia kutoa taarifa ya Sheikh Ponda, hayo maswali yako yaandae kwa maandishi kisha utaniletea hapa ofisini,” alisema Senso.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top