Hatimaye Barack Obama, Rais wa Marekani anatembelea tena bara la Afrika. Hii itakuwa ni mara ya pili Obama kutembelea Bara hili alikotoka baba yake baada ya ziara yake ya kwanza mwaka 2009. Mwaka huo alitembelea Ghana na Misri ilhali mwaka huu anatembelea Senegali, Afrika Kusini na Tanzania. Ziara hiyo iliyoanza tarehe 26 mwezi Juni, imemfikisha Tanzania tarehe 1 Julai na kuondoka siku ya pili yake.

Uchaguzi wa Obama kuwa Rais wa Marekani ulipokolewa kwa shangwe Afrika nzima. Wakati Waziri wa mambo ya nje wa Nigeria alilia kwa furaha, nchi ya Kenya ilitangaza siku ya mapumziko na Rais wa zamani wa Afrika Kusini ndugu Nelson ‘Madiba’ Mandela alisema ‘ushindi wa Obama unawafanya Waafrika wathubutu kuota ndoto (Jarida la The Economist).

Hapa Tanzania kulikuwa kuna shamra shamra za kila namna na magazeti yaliweka vichwa vya habari kana kwamba ni Rais wa Tanzania aliyechaguliwa. Waafrika walikuwa na matumaini makubwa sana na bwana Obama. Yamefikiwa?

Ni vema ifahamike kuwa Barack Obama ni Rais wa Marekani na siku zote atalinda maslahi ya Marekani tu. Kuwa na matumaini makubwa kwamba labda yeye angeliweza kuiweka Afrika mbele sana ilikuwa ni kujifurahisha tu nafsi. Maslahi ya Marekani ni ya kipaumbele kuliko kitu kingine chochote kwa Rais Obama. Kwa wengi Obama amekuwa kama amewavunja moyo.

Tanzania inapokea kiongozi wa Taifa kubwa duniani wa pili sasa ndani ya kipindi cha miezi 3 tu. Kwanza alikuja Rais wa China na sasa wiki hii anakuja Rais wa Marekani. Maneno ya mtaani na kwenye mabaraza ya majadiliano ni kwamba viongozi hawa wanakuja kugombea maliasili tulizo nazo kama gesi asilia na madini. 

Nadhani haya ni maneno ya kusema katika kupiga soga maana kunyonywa kwa rasilimali hakuhitaji Rais wa Marekani aje Tanzania. Makampuni yote makubwa yanayochimba dhahabu hapa nchini ni makampuni ya nje na marais wao hawakuja ili waweze kupata mikataba minono ya kuvuna utajiri wetu. 

Katika kitalu namba 2 cha utafutaji wa mafuta na gesi huko Bahari Kuu kampuni ya kimarekani ya ExxonMobil ina ubia na kampuni ya Norway ya StatOil. Kampuni hiyo haikusubiri Rais wa Marekani aje ili wapate mikataba.

Kuna makampuni mengi sana ya kichina yanajenga barabara zetu hapa nchini yakiwa na mikataba minono sana. Kule Mchuchuma na Liganga kuna kampuni ya kichina inajiandaa na uchimbaji wa chuma na makaa ya mawe. Makampuni yote haya hayakusubiri Rais wao aje.

Hoja inayojengwa hapa ni kwamba ujio wa Marais mbalimbali nchini ni ujio wa kujijenga kidiplomasia na wakati mwingine kama sehemu ya kutuma ujumbe fulani kwa dunia. Nchi inayotembelewa pia inaweza kuona kuwa diplomasia yake inaheshimiwa na mataifa yanayoitembelea.

Hata hivyo hii haiondoi ukweli kwamba Obama anakuja kwa ajili ya maslahi ya nchi yake kama ilivyo kwa wachina walivyokuja. Tumesikia Rais Obama ataambatana na mamia ya wafanyabishara kutoka Marekani kwa ajili ya kupata fursa za kuwekeza nchini. 

Pia tutasikia matangazo kuhusu msaada wa pili wa Millenium Challenge ambapo Wamarekani wanaendelea kumwaga pesa nchini kusaidia miundombinu lakini pia kushawishi kuungwa mkono na nchi zetu kwenye maamuzi fulani fulani jumuiya za kimataifa.

Tumesikia Obama atakwenda kutembelea mitambo ya kampuni ya Symbion. Hii ni mitambo ambayo miaka 4 iliyopita ilipigiwa kelele kuwa ni mitumba na hivyo TANESCO wasiinunue. 

Hawakununua na badala yake kampuni hiyo ya kimarekani ikainunua, wakaingia mkataba na TANESCO kuwauzia umeme unaozalishwa na mitambo hiyo hiyo chakavu. Wakati tunasuburi kulipa takribani Tshs 105 bilioni kwa Dowans baada ya kutubwaga kwenye kesi, tunasubiri kuona wanasiasa watakaokwenda kumsindikiza Obama kwenye matembezi hayo ya kutembelea mitambo chakavu.

Kampuni kubwa ya kutengeneza mitambo ya kuzalisha umeme ya GE imetangaza kuingia ubia na kampuni ya Symbion kuzalisha umeme nchini. Takribani 400MW zitazalishwa kutoka Mtwara na kuingizwa kwenye gridi ya Taifa. 

Pia sehemu kubwa ya umeme utakaozalishwa Mtwara tayari umepata soko kwenye kiwanda cha kuzalisha udongo ulaya (simenti) cha bwana Dangote kule Mtwara. Mtendaji Mkuu wa GE bwana Jeff Immelt ametangaza kuwa kampuni yake itauza mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi mingi zaidi Afrika Mashariki kuliko Marekani katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Ni biashara tu!

Nishati naona ni kipaumbele kikubwa sana kwa ziara ya Rais Obama. Kwa nchi kama yetu yenye watu asilimia 21 tu wenye umeme, ni dhahiri kipaumbele hiki watu wengi watakiiunga mkono.

Hata hivyo Obama ni lazima asimame kidete kuhakikisha kuwa kampuni za nchini mwake zinazopata miakataba hapa nchini ziweke wazi mikataba hiyo na kulipa kodi inavyostahili. 

Makampuni ya mafuta kutoka Marekani hayana historia nzuri duniani na hivyo ni lazima tulisisitize mapema kabisa. Uwazi wa mikataba na uwezo wa kupambana na ukwepaji kodi ni muhimu sana katika vita dhidi ya Ufisadi na ubadhirifu.

Rais Obama atambue kuwa iwapo Tanzania ingekuwa inakusanya nusu ya kodi zinazokwepwa na makampuni makubwa yanayotumia mbinu kali, basi tungehitaji misaada ya Marekani na hapa nchini angekuja kama mbia wa kweli na sawa katika dunia. 

Hivyo ni vema aungane na Waziri Mkuu wa Uingereza kuhakikisha kuwa makampuni makubwa hayatumii ‘tax havens’ kukwepa kodi katika nchi kama Tanzania. Uwazi wa mapato yao na kilicholipwa kwa Serikali ni vema usisitizwe sana na Obama mwenyewe ili makampuni yao yasikie na yaache kupora utajiri wa Afrika kiujanja ujanja.

Mwisho ni vema kama Rais Obama ataomba radhi kwa ushiriki wa Marekani kwenye mauaji wa Waziri Mkuu wa kwanza wa Kongo Patrice Lumumba. 

Hivi Tanzania inahangaika zaidi ya uwezo wake kupeleka majeshi huko mashariki ya Kongo kulinda amani. Waafrika wengi tunaamini kuwa mauaji ya Lumumba ilikuwa ni kama laana kwa Taifa lile na hivyo limekuwa ni taifa la vurugu na vita licha ya utajiri mkubwa ulioko nchini humo.

 Nyaraka za CIA zinaonyesha dhahiri kuwa Rais wa Marekani wa wakati huo Lyndon Johnson aliagiza kuuwawa kwa mwanamapinduzi Patrice Lumumba. Kuwaomba radhi Waafrika na hasa Wakongo kuhusu mauaji ya Lumumba ni jambo litakaloweza kusaidia sana kurejesha amani Kongo.

Karibu Afrika, Karibu Tanzania ndugu Barack Hussein Obama.
Fb 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top