Rais Kikwete akiwa na mgeni wake Rais Obama wa Marekani
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewashukuru wananchi
kwa kushiriki kikamilifu na kufanikisha kwa kiwango cha juu kabisa matukio ya
kitaifa ya karibuni ikiwamo ziara ya siku mbili ya Mheshimiwa Barack Obama,
Rais wa Marekani na mkewe Mama Michelle Obama.
Matukio mengine
yaliyofanyika nchini na ambayo yamepata mafanikio makubwa kwa sababu ya mchango
na ushiriki mzuri wa wananchi ni pamoja na Mkutano wa Kimataifa wa Smart Partnership International Dialogue
2013 na Mkutano wa Wake wa Marais wa siku mbili ulioanza leo, Jumanne,
Julai 2, 2013 mjini Dar Es Salaam.
Miongoni mwa wageni
maarufu wanaoshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Mheshimiwa George W. Bush,
Rais wa zamani wa Marekani na mkewe Mama Laura Bush pamoja na wake wa marais wa
Afrika Kusini, Ethiopia, Mozambique, Ghana, Sierra Leone na Uganda.
Vile vile, Rais
Kikwete amewashukuru viongozi na wasimamizi wote wa matukio na shughuli hizo
kwa kutoa uongozi thabiti ambao hatimaye umewezesha matukio hayo kumalizika
vizuri na malengo yaliyokusudiwa kufikiwa.
Aidha, Rais Kikwete
amevishukuru vyombo vya habari vya hapa nchini kwa mchango wao mkubwa wa
kuwahabarisha na kuwaelimisha wananchi kabla, wakati na baada ya matukio
yenyewe kuwa yamemalizika kwa yale yaliyomalizika.
Pia, Rais Kikwete
amezishukuru taasisi na vyombo vyote vya Serikali, vikiwamo vyombo vya ulinzi
na usalama kwa kufanya kazi bila kuchoka ili kufanikisha shughuli hizo.
Rais
pia amezishukuru taasisi za kibiashara na makampuni binafsi kwa mchango wao
katika kufanikisha shughuli hizi akisisitiza kuwa ushiriki wa wafanyabiashara
na taasisi za kibiashara katika shughuli hizo ni dalili njema kuwa ushirikiano
wa sekta za umma na sekta binafsi umeanza kufanya kazi vizuri katika Tanzania.
“Napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru
wananchi wote, na hasa wakazi wa Dar Es Salaam, kwa mchango wenu mkubwa katika
kufanikisha matukio haya muhimu ya kitaifa. Kwa pamoja tumeonyesha ukarimu wetu
wa jadi kwa viongozi na wageni ambao wameshiriki katika matukio hayo.”
Rais
amewaambia wananchi: “Tumeonyesha uvumilivu na utulivu mkubwa
wakati wote wa matukio hayo. Natambua mazingira yanayojengeka tunapokuwa na
ugeni mkubwa wa nje lakini bado tumeonyesha ukomavu wa hali ya juu kama taifa.
Nawashukuru sana nyie wananchi kwa kufanikisha yote haya kwa sababu bila
ushiriki wenu pengine matokeo ya shughuli hizo yangekuwa tofauti. Najivunia
sana ushiriki wenu katika shughuli zote hizi za kitaifa. Mumeijengea nchi yetu
heshima kubwa.”
Kwa
viongozi na wasimamizi wa shughuli hizo, Rais Kikwete amesema: “Uongozi
wenu umejidhihirisha waziwazi wakati wa matukio haya. Nawashukuruni nyote na
hasa viongozi wa Dar es Salaam ambao walikuwa wenyeji wetu wakati wote wa
shughuli hizi. Najua haikuwa kazi rahisi hata kidogo. Natambua kuwa wakati
mwingine tulifanya kazi chini ya shinikizo kubwa lakini nawashukuru sana kwa kufanikisha
haya yote.”
Kwa
vyombo vya habari, Rais Kikwete amesema: “Nawashukuru wamiliki, wahariri na waandishi
wa habari wa vyombo vyetu vya habari kwa mchango wenu wa kiwango cha juu katika
kufanikisha yote haya. Asanteni sana. Ninaamini kuwa tutaendeleza uzoefu
uliojengeka katika wiki moja ya matukio haya kwa manufaa ya nchi yetu na watu
wetu.”
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar
es Salaam.
2 Julai, 2013
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment