Mke wa Rais wa Marekani, Mama Michelle Obama,
amempongeza Mke wa Rais Mama Salma Kikwete kwa
kazi kubwa anayoifanya ya kutoa elimu bure kwa watoto wa kike
ambao ni yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi .
Mama Obama
alizitoa pongezi hizo wakati wa majadiliano baina yake na Mama Laura Bush
kwenye mkutano wa Wake wa Marais Wa Afrika uliofanyika katika hoteli ya
Serena jijini Dar es Salaam.
Mama Obama
alisema kuwa wake Wa Marais wana kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa wanawasaidia
wanawake na watoto hasa katika upatikanaji wa elimu na mahitaji mengine
muhimu.
Akiongea
wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Mama Kikwete alisema kuwa wake wa Marais
waliohudhuria mkutano huo wanawawakilisha wanawake wa Afrika ambao
wanahitaji kusaidiwa katika mambo ya afya, elimu na ujasiriamali.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) alisema kuwa katika mkutano huo washiriki watapata nafasi ya
kubadilishana ujuzi wa kazi na kutembelea hospitali ya Kansa ya Ocen
Road, kituo cha Mabinti na hospitali ya CCBRT ambako watajionea jitihada kubwa
zinazofanywa na watanzania za kuisaidia jamii inayowazunguka.
Alisema
kuwa baada ya kumalizika kwa mkutano huo anaamini kuwa washiriki watarudi
katika nchi zao na kuweza kukubaliana na Serikali zao pamoja na wadau wao
wengine kuwekeza zaidi kwa wanawake ili kuimarisha Bara la Afrika.
Mkutano
huo wa siku mbili uliandaliwa na Taasisi ya Rais mstaafu wa Marekani,
George Bush, na kuhudhuriwa na baadhi ya Wake wa Marais wa Afrika na Mke wa
Waziri mkuu mstaafu wa Uingereza, Cherie Blair.
Mada kuu ilikuwa wekeza kwa wanawake imarisha Afrika lengo likiwa ni kuimarisha upatikanaji
wa Afya kwa wanawake, upatikanaji Wa elimu na uchumi katika Afrika.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment