Rais Jakaya
Mrisho Kikwete amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Sudan Mheshimiwa
Omar Bashir kufuatia kuuawa na kujeruhiwa kwa askari wa Tanzania, walioko
katika ulinzi wa kimataifa wa amani katika jimbo la Darfur na kumtaka Rais
Bashir kuchukua hatua za haraka kuwasaka na kuwakamata waliohusika na kitendo
hicho kiovu na kuwafikisha mbele ya sheria haraka iwezekanavyo.
Katika
mazungumzo yao, Rais Omar Bashir amekubaliana na Rais Kikwete na kumuahidi
kuwasaka hadi kuwakamata wale wote
waliohusika na kuwachukulia hatua za kisheria.
Rais Bashir
amemueleza Rais Kikwete kuwa binafsi anaamini kuwa waliohusika ni wahalifu na hivyo
kuahidi kuwa lazima watasakwa hadi kukamatwa kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.
Rais Bashir
amempa pole Rais Kikwete kwa tukio hilo la kusikitisha ambapo wanajeshi wa
Tanzania wameenda nchini Sudan kulinda Amani na Usalama wa wananchi wa Sudan.
Mapema Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa(UN) Bw. Ban Ki Moon alimpigia Rais Kikwete na kumpa
pole kwa mkasa huo mkubwa na wa kusikitisha ambao umewatokea wa Tanzania hao
wakati wakiwa katika kutekeleza jukumu lao la kulinda amani nchini Sudan.
Hadi sasa
hakuna kikundi chochote ambacho kimekiri kuhusika na shambulio hilo ingawaje
kumekua na kutupiana lawama baina ya vikundi
vya kiserikali na vya waasi katika jimbo
la Darfur.
Mapigano baina
ya vikundi vya kikabila na koo mbalimbali zimesababisha mapigano na uvunjifu
mkubwa wa amani na usalama katika jimbo la Darfur kwa muda wa miaka 10 sasa, na
mara nyingi mapigano na tofauti zao hizo
zimesababisha vifo na uvunjifu wa amani kwa wananchi wa Sudan na wageni pia.
Mwishoni mwa
mwaka jana Wanajeshi wanne kutoka
Nigeria waliuawa karibu na El Geneina , Magharibi mwa Darfur ambapo pia inaelezwa
na Umoja wa Mataifa kuwa wanajeshi wapatao 50 wameuawa tangu kikosi hiki cha
Umoja wa Afrika kinachoundwa kwa pamoja
chini ya Umoja wa Mataifa (UNAMID) kianze operesheni yake mwishoni mwa mwaka
2007.
Taarifa za
Umoja wa Mataifa pia zinaeleza kuwa kabla ya mashambulizi yaliyofanyika dhidi
ya kikosi cha Tanzania jumamosi iliyopita, wanajeshi 6 wanaolinda Amani wameuawa
tangu oktoba mwaka huu ambapo pia inasadikiwa kuwa watu wapatao 300,000
wameyakimbia makazi yao.
Hata hivyo
kiini cha mgogoro huo unasadikiwa kuwa ni ugomvi wa ardhi na rasilimali
zilizoko katika jimbo hilo nchini Sudan.
Miili ya
maaskari hao saba wa Tanzania inatarajiwa kuwasili nchini ijumaa tarehe 19, Julai
kwa ajili ya maziko.
0 comments:
Post a Comment