Mashujaa wa Tanzania waliopigana Vita vya Kagera, watakumbukwa leo katika kilele cha sherehe hizo zitakazofanyika kwenye Kambi ya Kaboya mkoani Kagera.
 
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Phabian Massawe alisema jana kuwa maandalizi yote yamekamilika na Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika shughuli hiyo itakayoambatana na uwekaji wa mashada ya maua kuwakumbuka mashujaa hao. Mashujaa wa Tanzania wanakumbukwa leo baada ya kumpiga Fashisti Nduli Idd Amin, wakati wa Vita vya Kagera vilivyopiganwa mwaka 1978 na 1979.
Katika mapambano hayo, wapiganaji wa Tanzania wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliyachakaza majeshi ya Nduli Amini wa Uganda.
Mbali na hayo, Rais Kikwete anatarajiwa kuzindua Wilaya mpya ya Kyerwa iliyomegwa kutoka Wilaya ya Karagwe, pamoja na kuzindua mradi wa kuzalisha umeme wa Kaishozi.
Massawe aliwaambia waandishi wa habari: “Tutumie sherehe hizi kuhakikisha mazingira ya Mkoa wa Kagera yanaendelea kuwa safi na ninawaomba pia wananchi kuhakikisha wanadumisha amani na utulivu kama siku zote na kuwakaribisha kwa upendo wageni wote watakaofika mkoani kwetu.
“Pamoja na wageni wengine wa Kitaifa na Kimataifa wakiwamo mabalozi na marais wa nchi jirani, ninawaomba wananchi kuwa tayari kuwapokea wageni wetu kwani pia ni fursa kwa mkoa kujitangaza kwa ajili ya uwekezaji,” alisema.
Awali maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa Tanzania yalikuwa yakifanyika kila Septemba Mosi, lakini tarehe hiyo ilibadilishwa na kuwa Julai 25 kwa kuwa ndiyo tarehe waliyopokewa mashujaa hao waliopigana vita vya Kagera.
Hii ni mara ya pili kwa Mkoa wa Kagera kuandaa sherehe hizo. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2009.
Sherehe hizo zitahudhuriwa pia na Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein na baadhi ya mawaziri akiwamo, Prof Anna Tibaijuka (Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Harisson Mwakyembe (Uchukuzi), Hawa Ghasia (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), Sospeter Muhongo (Nishati na Madini), John Maghufuli (Ujenzi), Mathias Chikawe (Katiba na Sheria), Tersa Huvisa (Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira). 
mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top