Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe akihutubia katika moja ya mikutano yake ya hadhara.
JESHI la Polisi nchini na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa,
wanaonekana kuanza mkakati maalumu wa kukidhoofisha Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA) kwa kuwaandama viongozi wake kuhusu ushahidi wa
mlipuko wa bomu jijini Arusha na mpango wa kutaka kuanzisha kambi ya
mafunzo ya ukakamavu kwa vijana kwa ajili ya ulinzi.
Kutokana na mlipuko huo wa bomu Juni 15 mwaka huu, eneo la Soweto
jijini Arusha ulioua watu wanne na kujeruhi wengine zaidi ya 60 katika
mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani, CHADEMA
ilitangaza kuanza mpango wa kutoa mafunzo kwa vijana wake kwa ajili ya
kulinda mikutano na viongozi wake.
Hata hivyo, msimamo huo wa CHADEMA ulitafsiriwa tofauti na Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Jeshi la Polisi linaloongozwa na IGP Said Mwema, na
Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa wakidai hatua hiyo ni kinyume
cha sheria za nchi, katiba na sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992.
Kauli hizo zilipokelewa kwa mtazamo tofauti na wadau wa siasa nchini
wakihoji jeshi hilo na Tendwa walikuwa wapi kwa kutoionya CCM yenye
kikundi cha vijana cha Green Guard ambacho kinapewa mafunzo ya kijeshi
kwa ajili ya shughuli za chama.
Licha ya vyombo vya habari kuonyesha picha kadhaa za mafunzo ya
kikundi hicho cha CCM kikiwa na vijana wenye silaha, polisi na Tendwa
wamekuwa na kigugumizi cha kuzungumzia jambo hilo badala yake
wameendelea kuwatisha viongozi wa CHADEMA kuachana na mpango huo.
Katika suala hilo, Tendwa amekuwa na kauli za kujikanganya huku naye
akikwepa kuizungumzia Green Guard wakati viongozi waandamizi wa polisi
nao wamekuwa na ndimi mbili zinazokinzana kwenye suala hilo ambalo
wamelibebea bango wakitaka kufifisha tukio la mlipuko wa Arusha.
Jumamosi iliyopita, gazeti hili lilichapisha barua iliyoandikwa na
ofisi ya Tendwa kwenda kwa CHADEMA yenye kumb. Na RPP/CHADEMA/72/32
ikikiruhusu chama hicho kuanzisha vikundi vya ulinzi na usalama kama
ilivyo katika katiba yao.
Ofisi hiyo ya msajili kupitia kwa Naibu Msajili, Sisty Nyahoza, jana
ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikikana kuwahi kutoa ruhusa kwa
CHADEMA au chama chochote cha siasa kufanya mafunzo ya ukakavu au
mafunzo ya kutumia nguvu ya aina yoyote kwa wanachama wake au mtu
yeyote.
Hata hivyo, katika hali ya kuonyesha kuwa Tendwa anaibeba CCM, licha
ya kutoa vitisho kwa CHADEMA kuwa atawachukulia hatua za kisheria endapo
watashindwa au kukataa kutii agizo la kutoanzisha makambi hayo,
hakusema chochote kwa chama tawala ambacho kinaendesha kambi za
kujihami.
Julai 9 mwaka huu, CHADEMA kupitia kwa Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe,
walisema kufuatia mlipuko wa bomu Arusha, chama hicho kinakusudia
kuanzisha kambi za mafunzo kwa vijana watakotumika kulinda viongozi
katika shughuli zake kutokana na Jeshi la Polisi kushindwa kuchukua
hatua stahiki.
Siku chache baadaye, Mbowe alivamiwa usiku wa manane nyumbani kwake na
askari kadhaa wakidai kuwa walitaka awapatie ushahidi wa video ya
mauaji aliyodai kuwa nayo ikiwaonyesha baadhi ya polisi walivyoshiriki
kwenye tukio la mlipuko wa bomu Arusha.
Baada ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa kufichua tukio
hilo kwenye mkutano wa hadhara kesho yake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kinondoni, Camilius Wambura alidai hana taarifa za askari wake kufika
nyumbani kwa Mbowe kumkamata.
Jeshi hilo kisha liligeuza hoja na kumtaka Mbowe ajisalimishe kwa
ajili ya mahojiano kuhusu kauli yake ya kuhusu chama kutaka kuanzisha
makundi ya mafunzo ya ukamamavu kwa vijana wao.
Julai 17 mwaka huu, Mbowe aliandikiwa barua akiamrishwa awasilishe
ushahidi wa video aliyodai kuwa nayo, ikiwaonyesha baadhi ya polisi
walivyoshiriki kwenye tukio la mlipuko wa bomu Arusha.
Wakati Mbowe akiamriwa kufanya hivyo kabla ya juzi saa nane mchana,
jeshi hilo halijawahi kuwahoji Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu
Nchemba na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye
ambao walinukuliwa wakidai wana ushahidi kwamba CHADEMA walijilipua
wenyewe.
Juni 20 mwaka huu, Mkuu wa Mafunzo na Operesheni wa jeshi hilo, Paul
Chagonja aliwaeleza wanahabari kuwa Mbowe anapaswa kuwa mkweli na kuacha
kuuchezea umma kwani alichowaeleza polisi ni tofauti akisema hana
ushahidi huo wa mlipuko wa bomu bali alielezwa na wafuasi wake.
Lakini katika hatua ya kushangaza, Chagonja huyo huyo ndiye amemwamuru
Mbowe tena kupeleka ushahidi huo polisi akitamba kuwa baada ya kukaidi
kufanya hivyo, polisi inao makachero wake wanaojua jinsi gani ya
kuendelea na kazi hiyo.
Muda aliopewa Mbowe umemalizika bila kuwasilisha ushahidi huo, akidai
kuwa hawezi kwenda kinyume na msimamo wa chama kwani walikwishamwandikia
Rais Jakaya Kikwete, wakimtaka aunde tume huru ya majaji ndipo
watapeleka ushahidi wao huo na mwingine.
Mbowe alisema kuwa jeshi hilo ni watuhumiwa, hivyo kamwe hawawezi
kupeleka ushahidi huo kwao, na kukitaka chombo hicho cha dola kufungua
kesi mahakamani ili CHADEMA wapeleke ushahidi huo huko.
Jana, Mbowe alijisalimisha tena polisi kama alivyokuwa ameamriwa,
lakini hakupeleka ushahidi huo, na jeshi hilo lilimwamuru tena kupeleka
ushahidi huo kwa maandishi Ijumaa wiki hii.
Via Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment