Baadhi ya maafisa waelekezi wa semina hiyo kutoka kushoto ni Hamis Lupenja Afisa Mwandamizi wa elimu kwa walipa kodi-TRA toka makao makuu, Pili Mwinchande Afisa Mtendaji TCCIA na Sigsimund Kafuru Kaimu Afisa elimu kwa walipa kodi -TRA Temeke

Serikali imeshauriwa kusaidia katika kupunguza gharama za mashine za elektroniki za kutolea risiti na kuwapunguzia mzigo wafanyabiashara ambao wamedai hawana uwezo wa kununua mashine hizo.

Wakiongea wakati wa semina ya elimu kwa walipa kodi iliyofanyika Temeke jijini Dar es Salaam wafanyabiashara hao wamesema wengi wako tayari kulipa kodi lakini wameshindwa kumudu gharama za mashine za kutolea risiti  ambazo zimetajwa kuwa na bei kubwa.

Wafanyabiashara hao wameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya utafiti wa kina kujua sababu za wananchi wengi kukwepa kodi na kuandaa mazingira ya watu kuvutika katika kulipa kodi na kuchangia katika maendeleo ya nchi.

Hata hivyo Afisa Mwandamizi wa Idara ya elimu kwa walipa kodi wa TRA, Hamis Lupenja, amesema suala la kupunguza asilimia ya malipo ya kodi na TRA kununua mashine na kuzisambaza kwa wananchi ni suala la kisera zaidi hivyo ni vigumu kufanyika kwa sasa.

Naye Kaimu Afisa elimu kwa walipa kodi TRA- Temeke, Bwana Sigsimund Kafuru, amesema kuna faida kubwa ya kutumia mashine za elektroniki kwani inasaidia kutunza kumbukumbu na kurahisisha mfumo wa jinsi ya kulipa kodi.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top